Tarehe 5 Agosti, meli ya uvuvi ya Korea ya Kusini "Dong Won 628" ambayo ilitekwa na kundi la watu wenye silaha nchini Somalia kwa muda wa miezi minne, ilifika salama kwenye bandari ya Mombasa nchini Kenya. Japokuwa mabaharia 25 wa meli hiyo wakiwemo wachina watatu walikumbwa na mahangaiko na usumbufu mkubwa katika muda huo, lakini waliona furaha kubwa walipolakiwa na kupewa salamu za pole na wanadiplomasia, wajumbe wa wachina wanaoishi Kenya na wajumbe wa mashirika ya China waliokuwa wakiwasubiri kwenye bandari ya Mombasa.
Alfajiri ya saa kumi na nusu ya siku hiyo kwa saa za huko, meli hiyo ilifika salama kwenye bandari ya Mombasa. Balozi wa China nchini Kenya Bw. Guo Chongli na balozi wa Korea ya Kusini nchini Kenya waliikaribisha meli hiyo. Bw. Guo alisema,
"leo ni siku ya furaha, nafurahia kuuwakilisha ubalozi wa China na wachina wote hapa kuwakaribisha na kuwapongeza wenzetu watatu kurudi hapa salama ."
Wachina hao watatu ni Bwana Jin Hongji, Bwana Li Taiming na Bwana Yuan Zhengnan, wote ni wa kabila la wakorea. Walieleza kuwa tarehe 4 Aprili mwaka huu, meli yao ya uvuvi baada ya kutekwa kwenye eneo la baharini karibu na Somalia, mabaharia wote waliwekwa chini ya ulinzi mkali na watu wenye silaha wa Somalia waliokuwa na bunduki, walinyang'anywa vitu vyote, na walipaswa kukaa ndani ya meli kwa miezi minne, walikuwa hawana vyakula vya kutosha, hivyo walikula mara mbili tu kwa siku. Walipokutana na wenzao wachina kwenye bandari ya Mombasa na kupewa vitu vya matumizi ya kimaisha, walijiona kama wamerudi nyumbani.
Bw. Guo Chongli alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, viongozi wa serikali ya China walifuatilia sana usalama wa mabaharia hao, waliagiza juhudi zote zifanyike kuwaokoa mateka hao. Akisema:
"Baada ya kutekwa nyara kwa mabaharia hao, ubalozi wa China nchini Kenya ukifuata maagizo ya kamati kuu ya chama cha Kikomunisti cha China na wizara ya mambo ya nje ya China uliwasiliana mara kwa mara na rais, waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia, na waziri wa mambo ya nje wa Somalia. Uliwasiliana na shirika la uokoaji la kimataifa, shirika la mabaharia la kimataifa, na mashirika husika ya Kenya kuhusu namna ya kuwaokoa mabaharia hao waliotekwa nyara. Pia ulishirikiana na ubalozi wa Korea ya Kusini ulioko nchini Kenya kuchukua hatua za aina mbalimbali ili kuwaokoa mabaharia hao mapema iwezekanavyo. Nafurahi kuwa juhudi hizo zimepata mafanikio."
Mabaharia waliotekwa nyara na kundi la watu wenye silaha la Somalia wote walifurahi sana baada ya kuokolewa. Walitoa shukrani zao za dhati kwa kufuatiliwa vilivyo, wakisema,
"Tunawashukuru sana wenzetu wote waliokuwa na wasiwasi na kufuatilia usalama wetu, asanteni sana. Sasa jambo la kwanza tunalotaka kufanya ni kurudi nyumbani na kukutana na familia yetu."
|