Mapango ya Mogao yanaitwa pia ni Mapango ya Qianfodong, maana yake ya kichina ni mapango elfu moja ya Buddha, mapango hayo ni mabaki ya utamaduni wa dini ya kibudha yanayojulikana duniani. Mapango hayo yako kwenye Mlima Mingsha ulioko katika sehemu yenye umbali wa kilomita 25 kutoka kusini mashariki ya Mji Dunhuang mkoani Gansu, China. Mapango hayo yalitobolewa kuanzia mwaka 366.
Ilisemekana kuwa mtawa mmoja alipotembea kwenye sehemu hiyo, aliona Mlima Mingsha ulionesha mwanga wa dhahabu, alijihisi kuwa kumbe hii ni sehemu takatifu ya Buddha, hivyo alitoboa pango la kwanza la sanamu za Buddha. Baada ya miaka mingi ya enzi kadhaa, ilipofika mwaka 1368, kulikuwa na mapango karibu elfu moja, na kuanzia mwaka huo watu walikuwa hawatoboi tena mapango katika sehemu hiyo.
Mapango ya Mogao ni makubwa na madogo, sanamu za Budhaa ndani ya mapango hayo pia ni ndefu au fupi, na kubwa na ndogo. Mwaka 1987, Mapango ya Mogao yaliorodheshwa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa mali ya urithi wa utamaduni duniani.
Hivi sasa kutokana na mahitaji ya uhifadhi wa mabaki ya kale, mapango yasiyofikia 30 yanafunguliwa kwa watalii, hata katika mapango hayo, watalii wanapaswa kuongozwa na waongozaji wa utalii kuingia ndani ya mapango. Mwongozaji wa utalii Bi. Liu Hongli alituelezea kuwa, kwa kawaida, kutembelea mapango zaidi ya 10 kwa watalii kunahitaji saa 2 hivi, kama watalii wanataka kutembelea kwa makini mapango yote ya mawe yanayofunguliwa, inawabidi watembelee kwa siku nzima.
Bi. Liu Hongli alisema, kutembelea Mapango ya Mogao, waongozaji wa utalii huwa wanaweza kuwaongoza watalii kutembelea kwanza Pango No.96, kwani nje ya pango hilo kuna Jengo kubwa lenye ghorofa 9, ambalo ni jengo la alama la Mapango ya Mogao.
Katika pango la No.96 kuna sanamu kubwa ya kwanza katika Mapango ya Mogao, sanamu hiyo ni Budha Mile yaani Laughing Buddha, yaani Buddha anayecheka kimo chake ni mita 35.5, ambayo ni sanamu kubwa ya kwanza ndani ya pango duniani.
Pango No.96 lilitobolewa mwaka 695, sanamu za Buddha, kwa kuwa sanamu ya Budhaa ndani yake ilikarabatiwa mara kwa mara, hivyo sura yake siyo ile ya awali, lakini sanamu hiyo ya Buddha bado inaonekana kuwa na hali ya utukufu. Kama watalii wanataka kuelewa vizuri zaidi hali asili ya Mapango ya Mogao, kwa kuendelea wanaweza kutembelea Pango No.328, ndani ya pango hilo kuna sanamu 5 za Buddha zilizofinyangwa vizuri sana.
Sanamu ya Buddha iliyoko katikati ya mapango hayo ni Sanamu ya Buddha mkuu Sakyamuni aliyekaa juu ya kitako cha petali za yungiyungi, sura yake inaonekana kuwa na heshima kubwa. Upande wa kushoto wa sanamu ya Buddha Sakyamuni ni sanamu ya mfuasi wake mkubwa Jiaye, ambaye anaonekana kumtii sana Buddha Sakyamuni, na upande wa kulia wa sanamu ya Sakyamuni ni mfuasi wake mwingine Ananda. Na pia kuna sanamu nyingine mbili za Buddha, sura za sanamu hizo ni tofauti na zinawavutia sana watu.
Katika pango No.158, sanamu ya Buddha aliyelala pia inawavutia watu sana. Sanamu hiyo ina urefu wa mita 16, inasemekana kuwa ni sanamu ya Buddha Sakyamuni aliyefika hali ya nirvana, katika dini ya kibuddha, Buddha au watawa siyo watu wa kawaida, hawawezi kufa, bali waliweza kufika hali ya nirvana, maana walifika hali isiyo na tamaa na uchungu.
Mwili wa sanamu hiyo unaonekana kuwa sanamu hiyo ilifinyangwa vizuri, sura yake ina mvuto maalum hata ukiitazama hisia zako zinaweza kuguswa na heshima yake kubwa.
Mbali na sanamu za Buddha, michoro kwenye kuta pia ni sehemu moja muhimu ya sanaa ya Mapango ya Mogao. Michoro hiyo kwenye kuta ingawa imefifia kutokana na upepo na mchanga katika miaka mingi iliyopita, lakini rangi zake bado zinaonekana dhahiri, na michoro yenyewe inaonekana wazi. Michoro hiyo kwenye kuta nyingi ilieleza hadithi nyingi za dini ya kibuddha, na picha za malaika wanaoruka mbinguni inaonekana zaidi kwenye michoro hiyo, ambazo zinasifiwa sana na watu.
Katika dini ya kibuddha, kuna malaika wanaoruka mbinguni ambao wanaweza kuimba nyimbo, kucheza ngoma na kudondosha maua wakati wa mkutano wa dini ya kibuddha. Katika mapango zaidi ya 490 ya Mogao, karibu kila pango kuna michoro ya malaika wanaorukaruka mbinguni, ambao wameshika maua ya Yungiyungi, vinanda vya Pipa, wanaodondosha maua, na wanaopiga muziki, sura za malaika hao ni za aina mbalimbali tofauti, ambazo zinapendeza sana.
Mwalimu wa sanaa ya uchoraji katika Chuo kikuu cha Qinghua cha China Bi. Zheng Ni ametembelea Mapango ya Mogao mara kadhaa, alisema michoro ya malaika hao wanaoruka mbinguni kwenye kuta za Mapango ya Mogao inamvutia zaidi. Alisema:
Kwenye michoro hiyo malaika hao hawana mabawa, lakini wanaweza kuruka mbinguni na kucheza ngoma, hali ya hisia za upendo inaonekana katika michoro hiyo. Na michoro yenyewe, uchoraji wa malaika hao ulionesha ustadi mkubwa, ukiangalia kwa muda mrefu, hata unaweza kuona malaika hao waliochorwa ni kama wako hai. Michoro ya malaika wanaoruka mbinguni inastahili kuangaliwa na kufanyiwa utafiti na watu.
Kwenye michoro ya ukutani katika Mapango ya Mogao pia hutokea picha kuhusu wacheza dansi walioshika vinanda vya Pipa vya kichina, ambao kila mcheza dansi husimama kwa mguu mmoja, mguu wake mwingine unainuka juu, na mikono yake miwili inainuka na kupiga kinanda nyuma ya mgongo wake, kama vile wanaweza kucheza dansi kwa kufuata midundo ya muziki.
Mtaalamu wa utafiti wa mabaki ya kale wa Taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bwana Wu Xinhua anaona kuwa, miongoni mwa michoro kweli kuta za Mapango ya Mogao, picha za malaika wanaoruka mbinguni na wacheza dansi wanaopiga vinanda vya Pipa nyuma ya migongo yao zinastahili kufanyiwa utafiti na watu, kwani picha hizo zimetoa data zenye thamani kuhusu hali ya jamii ya zama za kale za China. Bwana Wu anaichukulia michoro hiyo ya kutani kuwa ni "maktaba ya ukutani". Akisema:
Kwa mfano maderaya yaliyofunikwa kwenye farasi wa kivita yalitumiwa katika nchi mbalimbali za Ulaya baada ya zama za kati, lakini maderaya hayo yalionekana katika michoro ya kutani katika Mapango ya Mogao kabla ya kutumika barani Ulaya. Aidha, desturi zile za maishani kama vile kupiga mswaki, hata zilionekana katika michoro ya kutani katika Mapango ya Mogao ya Dunhuang, picha mbalimbali zinaonesha kuwa watu wanatumia vidole vilivyochovywa kwenye vitu visivyojulikana kusafisha meno yao.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-14
|