Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-14 16:29:57    
Mtaalamu wa magofu ya mji wa Yin wa Enzi ya Shang, Yang Xizhang

cri

Hivi karibuni kwenye mkutano wa urithi wa utamaduni duniani uliofanyika nchini Lithuania, magofu ya mji wa kale wa Yin nchini China yamewekwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni duniani. Magofu hayo ni mabaki muhimu yanayoonesha utamaduni wa kale nchini China, na vitu vingi vilivyogunduliwa huko vinastaajabisha watu duniani.

Mto Huanghe unaoanzia kwenye Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet ni "mto mama" wa China. Kutokana na hali ya hewa nzuri sehemu za kati na za chini kwenye mto huo ni chanzo cha utamaduni wa mwanzo nchini China. Mji wa Yin ambao ulikuwa mji mkuu wa Enzi ya Shang iliyokuwepo kuanzia mwaka 1600 K.K. hadi mwaka 1046 K.K. una kilomita za mraba 24 kwenye kijiji cha leo cha Xiaotun nje ya mji wa Anyang mkoani Henan, sehemu ya kati ya Mto Huanghe. Tangu mwanzoni mwa karne iliyopita hadi leo wataalamu wa mambo ya kale wamefanya ugunduzi mara nyingi na wamegundua msingi wa kasri kubwa la kifalme, makaburi ya wafalme na makaburi ya watu wa kawaida karibu elfu moja yaliyopangwa kwa ukoo, na kutoka makaburi hayo wamegundua vipande vingi vyenye maneno kwenye gamba la kobe, vyombo vya shaba nyeusi, vya jade na vigae vya vyombo vya udongo. Vitu hivyo ni muhimu sana katika kuchunguza utamaduni wa kale wa China. Bw. Yang Xizhang ambaye amekuwa na umri wa miaka 70 ni mtaalamu mkubwa wa ugunduzi na utafiti wa magofu ya mji huo wa Yin.

Bw. Yang Xizhang alihitimu masomo yake ya utafiti wa mambo ya kale katika Chuo Kikuu cha Beijing miaka ya 50, mwaka 1958 alipokuwa na umri wa miaka 22 alijiunga na taasisi ya utafiti wa mambo ya kale katika Tasisi Kuu ya Sayansi ya Jamii ya China, taasisi hiyo ni idara yenye wataalamu wakubwa wa mambo ya kale nchini China, na ina vituo vyake katika kila sehemu inyayofanya utafiti wa mambo ya kale nchini China. Baada ya miaka minne Bw. Yang Xizhang alihamishiwa kwenye kituo cha mji wa Anyang na kushiriki kwenye kazi ya ugunduzi na utafiti wa magofu ya mji wa Ying, lakini hakufikiri kwamba tokea wakati huo angeishi huko kwa miaka zaidi ya 40, kazi hiyo ilimtenganisha yeye na familia yake, moja huko Anyang na nyingine Beijing. Lakini Bw. Yan Xizhang ambaye alikuwa na juhudi za kazi hakuwahi kulalamika hata kidogo. Alisema, "Kazi inanihitaji niwe kwenye magofu ya mji wa Yin, basi niifanye na nioneshe sura ya awali ya mji huo hatua kwa hatua."

Bw. Yang Xizhang ni mwenyeji wa mji wa Suzhou, kusini mwa China, chakula huko ni tofauti na cha mkoani Henan alikofanya kazi, na zaidi ya hayo kituo cha uchunguzi wa mambo ya kale kiko mashambani, maisha yalikuwa ni ya kawaida kabisa. Msichana wa mji wa Suzhou aliyemwoa mwaka 1963 hakutegemea kama angeishi naye katika sehemu mbili baada ya kuolewa, hata Yang Xizhang alipokuwa na umri wa kustaafu aliendelea kufanya kazi huko Anyang, alimwambia mke wake, "kazi ni nyingi, utafiti sijamaliza."

Watu wengi wanaona kazi ya Yang Xizhang haikuwa na mvuto, katika muda wa miaka zaidi ya 40 kila siku alikuwa anakabiliana na mashimo ya udongo, lakini alipofukua udongo alikuwa makini sana, kwani kipande kimoja cha gamba la kobe au kipande kidogo cha chombo cha udongo, pengine kitakuwa dalili ya mwanzo wa ugunduzi mkubwa. Mwaka 1990 Bw. Yang Xizhang alipata bahati hiyo.

Mwaka 1990, Bw. Yang Xizhang alisimamia kazi ya kufukua kaburi iliyopangwa namba 160, hakutegemea kama kwenye kaburi hilo alizikwa tajiri, kutoka kwenye kaburi hilo aligundua vitu 349, huu ulikuwa ni ugunduzi mkubwa katika mwaka huo chini China. Wenzake walimpongeza sana kwa kusema "umebahatika sana". Bw. Yang Xizhang alisema, mtaalamu wa mambo ya kale akigundua vitu vingi kutoka kwenye kaburi kubwa hakika kwake ni bahati, lakini makaburi ya makabwera pia yana utamaduni wake. Alisema, "Utamaduni pia unaweza kugunduliwa kutoka kwenye makaburi madogo. Kwa mfano, tulifukua makaburi karibu elfu moja mjini Anyang na baada ya kumaliza kuyafukua yote tuligundua kuwa makaburi hayo yalipangwa kwa ukoo. Kwenye vitabu vya kale kuna maelezo kuhusu muundo wa ukoo katika China ya kale, sasa maelezo hayo yamethibitishwa kutoka makaburi hayo."

Vitu vya kale vilivyogunduliwa lazima viwe na taarifa za matokeo ya utafiti ili wataalamu wengine wazitumie. Mpaka hivi sasa Bw. Yang Xizhang ametoa makala na maandishi mengi ya utafiti wake, aliwahi kuchapisha vitabu vyake vya "Maendeleo Muhimu ya Ugunduzi kutoka Magofu ya Mji wa Yin baada ya Mwaka 1980", "Utaratibu wa Makaburi ya Enzi ya Shang", na hasa kitabu chake cha "Akiolojia kuhusu Enzi za Xia na Shang Nchini China" ambacho kilipata tuzo ya kwanza katika nyanja ya elimu ya mambo ya kale nchini China. Bw. Yang Xizhang alisema, "Nimetumia miaka yangu yote kufanya ugunduzi, kufahamu na kutafiti magofu ya mji wa Ying katika msingi wa mafanikio ya watu wengine, na watu wa baadaye wataendelea katika msingi wa mafanikio yangu, naona nimetimiza tumaini la maisha yangu."

Bw. Yang Xizhang alisema, katika miaka zaidi ya mia moja ya ugunduzi kwenye magofu ya mji ya Yin jumla vimegunduliwa vipande vya magamba ya kobe laki moja na nusu, vyombo vya shaba nyeusi karibu elfu kumi na aina nyingi za vyombo vya udongo, jade na vyombo vya mifupa. Utafiti wa magofu ya mji wa Yin umekuwa elimu maalumu ikiwa ni pamoja na elimu ya mambo ya kale, historia na elimu kuhusu maandishi ya kale. Wataalamu kadha wa kadha wametoa mchango katika ugunduzi huo wa magofu ya mji wa Yin. Hivi karibuni magofu ya mji wa Ying yamewekwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni duniani, akiwa mtaalamu anaona faraja kwa kuona utamaduni wa magofu ya mji wa Yin umethaminiwa namna hii.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-14