Mkipata nafasi ya kutembelea sehemu ya kaskazini mwa China, huenda mtapita kwenye mji wa kisasa wa Tangshan. Mji wa Tangshan una mfumo kamili wa mawasiliano mepesi na maeneo ya ustawishaji wa teknolojia ya kisasa. Mazingira bora ya miundo-mbinu yamevutia uwekezaji wa makampuni mengi ya kimataifa, na mazingira bora ya maisha yanawaletea furaha wakazi wa mji huo. Lakini tetemeko kubwa la ardhi lililotokea miaka 30 iliyopita liliuteketeza kabisa mji wa Tangshan.
Tetemeko kubwa la ardhi ambalo halikuwahi kutokea katika karne kadhaa zilizopita duniani, lilitokea tarehe 28 mwezi Julai mwaka 1976 katika mji wa Tangshan, umbali wa kilomita 150 kutoka Beijing, mji mkuu wa China, ambalo nguvu yake ilikuwa kama mara 400 ya bomu la atomiki lililolipuka kwenye kisiwa cha Hiroshima, Japan. Wimbi la hewa lililotoka kwenye kina cha kilomita 16 chini ya ardhi, liliteketeza kabisa mji wa Tangshang uliokuwa na idadi ya watu milioni 1, ambapo watu laki 2.4 walikufa na wengine laki 1.6 walijeruhiwa, hasara ya kiuchumi ya moja kwa moja iliyosababishwa na maafa ya tetemeko la ardhi ilizidi Yuan bilioni 10. Mwalimu mstaafu bibi Wang Guiqin aliyeshuhudia tetemeko kubwa la ardhi la Tangshan alisema, wakati huo karibu kulikuwa hakuna hata jengo moja zima mjini Tangshan:
"Kabla ya kutokea tetemeko la ardhi, tulikuwa tumekaa kwenye nyumba yetu. Nyumba yetu ilibomoka wakati wa kutokea tetemeko la ardhi, ghorofa tuliyokaa ilianguka chini kabisa, sisi tulijipenyeza na kutoka nje kwenye tundu moja, wakati ule mvua ya rasharasha ilikuwa inanyesha, mtoto wangu alikuwa na umri wa miaka miwili, tulijisitiri kwa majani ya alizeti."
Katika miaka 30 iliyopita baada ya kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi, pato la wakazi wa mji wa Tangshan liliongezeka kwa haraka. Wastani wa pato la mkazi wa mji wa Tangshan katika mwaka 2005, uliongezeka mara 40 kuliko ule wa mwaka 1975, kabla ya kutokea kwa tetemeko la ardhi. Baada ya kompyuta na zana za kuimarisha afya za watu, hivi sasa nyumba na magari vimekuwa vitu vipya vinavyonunuliwa sana na watu wa huko. Kwenye maonesho ya pili ya kimataifa ya magari yaliyofanyika mjini Tangshan, magari 410 yalinunuliwa na watu katika siku 5 za maonesho. Uchunguzi uliofanywa unaonesha kuwa, mjini Tangshan mtu mmoja kati ya kila watu watano amenunua gari.
Tangshang ni moja ya miji iliyofungua mlango kwenye sehemu ya pwani ya China, katika miaka ya karibuni mji huo umepiga hatua kubwa katika kuvutia mitaji ya nchi za nje. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, Tangshan ilitumia mitaji ya nchi za nje dola za kimarekani milioni 310, zikiwa ni ongezeko la 30% kuliko kipindi kama hiki cha mwaka uliopita, na kuchukua nafasi ya kwanza mkoani Hebei. Mkurugenzi wa ofisi ya uwekezaji ya idara ya biashara ya mji wa Tangshan Bw. Chai Hongsheng alisema, kuendeleza mambo ya viwanda kwa kutumia ubora wa raslimali za mkoa huo na kuvutia wafanyabiashara wa kigeni, ni njia muhimu iliyochangia kuleta maendeleo kwenye mji wa Tangshan katika miaka ya karibuni. Alisema,
"mji wa Tangshan una viwanda vingi vya kazi nzito, vikiwemo vile vya kuzalisha chuma, chuma cha pua, vifaa vya ujenzi na mitambo. Tulivutia uwekezaji wa makampuni mengi ya kimataifa kwa njia ya kufanya ubia, ushirikiano na kuhamisha umilikaji wa hisa, tumejenga uhusiano wa ubia na ushirikiano pamoja na kampuni ya Panasonic na kampuni ya Toyota za Japan, kampuni ya Danone ya Ufaransa, kampuni ya Anheuser-Busch ya Marekani na kampuni ya Cheung Kong (Holdings) Limited. Katika sekta ya chuma na chuma cha pua, tunashikilia kufungamanisha utumiaji wa mitaji ya nchi za nje pamoja na marekebisho ya muundo wa sekta ya chuma na chuma cha pua, kujenga kiwanda cha chuma na chuma cha pua cha ubia na kuinua kiwango cha teknolojia na uwezo wa ushindani wa bidhaa za viwanda vya chuma na chuma cha pua."
Katika miaka ya karibuni, uchumi wa mji wa Tangshan uliongezeka kwa kasi. Mwaka 2005 jumla ya thamani ya uzalishaji mali ilifikia Yuan bilioni 202.7, ambapo kodi zilizokusanywa zilifikia Yuan bilioni 22.6. Ofisa anayesimamia mambo ya uchumi wa serikali ya mji wa Tangshan alisema, katika siku za baadaye mji wa Tangshan utaendelea kuharakisha ufunguaji mlango, na wakati unapokuza uchumi wa mji pia utaboresha maisha ya wakaziwake.
|