Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-16 19:54:08    
Kinga na tiba ya ugonjwa wa kiharusi

cri

Kiharusi ni ugonjwa mkali wa mishipa ya damu kwenye ubongo unaohatarisha vibaya afya na maisha ya binadamu. Takwimu husika zimeonesha kuwa, kila mwaka watu milioni 1.5 wanapatwa na ugonjwa huo nchini China, na nusu kati yao wanakufa kutokana na ugonjwa huo, na watu wengi wanaopona wanapoteza uwezo wa kufanya kazi kwa viwango tofauti. Hali hiyo imesababisha mzigo mkubwa kwa familia na jamii.

Mzee Wang Qinmei mwenye umri wa miaka 65 ana afya njema na hakuwahi kupatwa magonjwa makubwa. siku moja asubuhi katika majira ya mchipuko mwaka huu, alienda sokoni kwa baisikeli kununua chakula kama kawaida, ghafla alijisikia kizunguzungu na akapoteza fahamu. Baada ya muda mfupi, alipata fahamu na kuomba msaada kutoka kwa wapita njia na akapelekwa hospitali.

Katika chumba cha huduma ya kwanza, daktari alithibitisha haraka ugonjwa uliompata mzee Wang. Daktari wa upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo katika hospitali ya 301 ya jeshi la ukombozi wa watu wa China Bw. Wang Jun alisema:

"baada ya kumfanyia upimaji wa CTA, tuligundua sehemu moja nyembamba katika mishipa mikubwa ya damu iliyoko shingoni, na asilimia 90 ya sehemu hiyo ya mishipa ya damu imezibwa. Hali hiyo ni ya hatari sana."

Tatizo la wembamba wa mishipa ya damu ya shingoni ni chanzo kikubwa cha ugonjwa wa kiharusi wa aina ya kukosa damu kwenye ubongo. Asilimia 60 ya wagonjwa wa ugonjwa huo wanatokana na tatizo la kuzibwa kwa mishipa ya damu ya shingoni. Pamoja na kuzidi kuziba kwa mishipa ya damu, dalili za ugonjwa huo zinaonekana kidhahiri na wazi zaidi, hatimaye zinasababisha kiharusi kibaya. Kwa kuwa asilimia 90 ya mishipa ya damu ya shingoni inakuwa imeziba, hali hiyo inaufanya ubongo ukose damu na oksijen, na dalili mbalimbali za ugonjwa huo zote zinasababishwa na tatizo hilo.

Mbali na kiharusi cha kukosa damu kwenye ubongo, aina nyingine ni kiharusi cha kutokwa damu kwenye ubongo. Chanzo kikubwa ni shinikizo kubwa la damu linalosababisha mishipa midogo ya damu kwenye ubongo ivimbe na kupasuka.

Kwanza, ugonjwa wa kiharusi unahusiana na umri na jinsia. Kwa kawaida, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55 wana hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kiharusi, na hatari ya kupatwa ugonjwa huo kwa wanaume ni asilimia 50 zaidi kuliko wanawake. Ya pili, ugonjwa huo ni wa kurithi. Aidha, magonjwa ya shinikizo kubwa la damu, kisukari, tatizo la moyo, tatizo la kuwa na uzito kupita kiasi, kuvuta sigara na kunywa pombe zote zinaweza kusababisha kiharusi.

Kwa kawaida, kuna dalili kadhaa zinaonekana kabla ya kutokea kwa kiharusi. Mkurugenzi wa idara ya upasuaji wa mishipa ya damu katika hospitali ya 301 ya jeshi la China Bw. Li Baomin alisema:

"kabla ya kutokea kwa kiharusi, mgonjwa hujisikia kizunguzungu, mwasho kwenye mikono na miguu, na kutoona vizuri. Baada ya muda, hisia hiyo itaisha au itarejea tena. Kama una dalili hizo, ni lazima uchukue tahadhari."

Bw. Li alisema, kama dalili hizo zinatokea mara kwa mara katika siku moja au mbili, na pia una shinikizo kubwa la damu au ugonjwa wa kisukari au ugonjwa wa kurithi, unapaswa kwenda hospitali mara moja kufanyiwa uchuguzi. Hivi sasa, ugonjwa wa kiharisi unaweza kuthibitishwa mapema na kwa usahihi.

Basi kama wagonjwa wakipatwa na kiharusi nyumbani au kwenye sehemu za hadhara tutafanyaje? Watalaamu wanaeleza kuwa, kiharusi kinatokea ghafla, wagonjwa wanaweza kupoteza fahamu, kuanguka, kutikisika au kushindwa kuongea. Watu huchanganyikiwa wakati hali hiyo ikitokea, na hata wanakuwa hawajui la kufanya. kwa kawaida, watawaamsha hata kuwatingisha wagonjwa. Vitendo hivyo vinaweza kuwadhuru wagonjwa hao, hata vinafanya hali yao iwe mbaya zaidi.

Kama mtu akipatwa kiharusi, kwanza jamaa zake wasihangaike, bali wanatakiwa kumtuliza mgonjwa, na ni afadhali wasimwamshe alipo, lakini wanatakiwa kumwita daktari mara moja. na ni bora walegeze nguo za ndani za mgonjwa, hatua hiyo inamsaidia mgonjwa kupumua bila tatizo. Kama mgonjwa akitikisika, hali hiyo ni mbaya, ni lazima wamshtue. Kwa kuwa wakati huo, mgonjwa anaweza kujiuma ulimi, hivyo ni afadhari wazibe mdomo wa mgonjwa kwa nguo. Wagonjwa wengi wa kiharusi wanatapika, ili kuzuia wagonjwa kama hao wasijizibie koo, ni bora kuwalaza shingo upande. Kama matapishi yakibaki mdomoni, ni lazima yatolewe mdomoni kwa vijiti, na kama mgonjwa huyo ana meno bandia, inapaswa kuyatoa ili yasije yakaingia kooni.

Zamani ugonjwa wa kiharusi ulikuwa unatibiwa kwa upasuaji, hivi sasa unatibiwa kwa matibabu yenye usalama, ufanisi na rahisi zaidi. Matibabu hayo ni kuingiza mrija mdogo kwenye mshipa mkubwa wa damu wa pajani na kuifikisha kwenye sehemu yenye tatizo mwilini na kutibu. Kwa kuwa kipenyo cha mshipa mkubwa wa damu ni milimita 15 hivi, na kipenyo cha mirija ni milimita 2 tu, hivyo mrija huo unaweza kupita kwenye mishipa ya damu bila tatizo. Mbali na hayo, kutokana na kuwa hakuna nevu za hisia ndani ya mishipa ya damu, basi wagonjwa hawasikii maumivu.

Mzee Wang Qinmei alitibiwa kwa matibabu hayo. Daktari aliweka chombo maalum cha kupanua mshipa wa damu ndani ya sehemu ya mshipa mkubwa wa damu wa shingoni kwake iliyozibwa kwa kutumia mirija. Mzee Wang alisema:

"Baada ya kuwekewa chombo cha kupanua mshipa wa damu, nilisikia damu inapita vizuri, ghafla hisia ya kizunguzungu iliondoka mara moja."

Matibabu hayo hayahitaji kuwapa wagonjwa nusukaputi ya mwili mzima. Wagonjwa wanaweza kutibiwa wakiwa na fahamu vizuri. Pia kwa kuwa matibabu hayo yanaleta majaraha madogo tu, basi wagonjwa wanaweza kutembea saa 24 tu baada ya matibabu. Hivi sasa, wagonjwa wengi zaidi wa kiharusi wanachagua matibabu hayo.