Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-17 16:04:19    
Maisha ya hivi sasa ya watoto yatima waliopoteza wazazi wao kwenye tetemeko kubwa la ardhi la Tangshan miaka 30 iliyopita

cri
Tarehe 28 Julai miaka 30 iliyopita, tetemeko kubwa la ardhi liliikumba Tangshan, mji wa kaskazini ya China. Maafa hayo yalisababisha vifo vya watu laki 2 na elfu 40, na kuwafanya watoto zaidi ya elfu 4 wapoteze wazazi wao. Hivi sasa miaka 30 imepita, je, watoto yatima hao wanaendelea vipi? Katika kipindi cha Tazama China cha wiki iliyopita, watoto yatima kadhaa walieleza jinsi walivyonusurika kwenye maafa hayo. Leo tunawaletea maelezo kuhusu maisha yao baada ya tetemeko la ardhi. Karibuni.
Feng Huang Yuan ni mtaa mmoja wa makazi ya hali ya juu huko Tangshan, ambao unajulikana kama "mtaa wa matajiri". Nyumba ya Bibi Xu Weiwei iko mtaani humo. Katika nyumba hiyo yenye mita 160 za mraba, kuna televisheni kubwa aina ya LCD, jokofu yenye milango miwili na mapambo mazuri, hayo yote yanaonesha utajiri wa mwenye nyumba. Ukutani imetundikwa picha ya wanafamilia watatu wanaotabasamu. Kwenye picha hiyo binti wa Bibi Xu Weiwei amekua vizuri na ana urefu unaolingana na mama yake.
Bibi Xu Weiwei alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi sasa anaendesha kampuni moja ya matangazo ya biashara, na mume wake anafanya kazi katika kampuni ya taxi. Binti yao anasoma katika shule ya sekondari huko Dalian, mji wa pwani ulio karibu na mji wa Tangshan.
"Kulikuwa na kipindi ambapo nilishughulikia kazi zote za matangazo ya biashara mjini Tangshan. Mimi huwa nabanwa na kazi na mume wangu pia ana shughuli mbalimbali kazini, familia yetu inaishi kwa kuwa na pilikapilika nyingi. Binti yangu ana tabia nzuri, anafahamu kuwa nabanwa na kazi, kwa hiyo anajiamulia shughuli zake."
Katika mahali ilipokuwepo nyumba ya Xu Weiwei iliyobomolewa katika tetemeko la ardhi, sasa ni barabara kuu mjini Tangshan, ambapo kando ya barabara hiyo kuna majumba ya ghorofa yaliyopangwa vizuri na msongamano wa watu, vile vile kuna mabango ya matangazo ya biashara yaliyotengenezwa na kampuni ya Xu Weiwei yanayong'ara wakati wa usiku.
Mtoto yatima mwingine Bibi Dang Yuxin sasa anafanya kazi katika shirikisho la walemavu la mji wa Tangshan. Kazi yake ni kuwahudumia walemavu na kutekeleza sera nafuu zilizotungwa na serikali kwa ajili ya walemavu. Anafurahia kazi hiyo. Alisema  "Ulemavu wa watu wengi hapa mjini Tangshan ulitokana na tetemeko la ardhi. Walipoambiwa kuwa mimi nilipoteza wazazi wangu kwenye tetemeko hilo la ardhi, walijiona kuwa karibu zaidi na mimi kutokana na kukumbwa na maafa ya namna moja. Kwa hiyo wanapenda kunielezea shughuli zao."
Mume wa Bibi Dang Yuxin anafanya kazi katika kampuni ya huduma ya kutoa joto ya mji wa Tangshan, mwanaye aitwaye Long Long anapendeza sana. Dang Yuxin alieleza kuwa ana pato la uhakika, anaishi kwa furaha, na anafanya kazi yenye maana. Anaridhika na maisha ya hivi sasa na kutarajia kuwa yatakuwa mazuri zaidi kadiri siku zinavyokwenda.
Kwa kusema kweli si watoto yatima wote walioendelea vizuri bila ya matatizo. Tangshan ni mji muhimu wa viwanda nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni viwanda kadhaa vya taifa vilivyo nyuma kimaendeleo viliuzwa au kuungana na vingine, katika zoezi hilo baadhi ya wafanyakazi wa viwanda hivyo walipunguzwa kazi. Miaka mitano iliyopita Bibi Zhang Lizhi alipunguzwa kazi kutoka kwenye mgodi mmoja wa makaa ya mawe, akapata ajira ya kuzoa takataka katika jengo moja.
Hivi sasa mwanamke huyo anaonekana na afya nzuri, isipokuwa mguu wake mmoja uliojeruhiwa kwenye tetemeko la ardhi umemfanya awe na ulemavu mdogo kwa kutembea.
 "Nina mtoto mwenye afya njema, mume anayenipenda, na familia yenye furaha. Aidha katika jamii sisi watoto yatima tunafuatiliwa na watu wengi. Kwa hiyo sina sababu ya kuona huzuni. Natamani kumlea mtoto wangu mpaka awe mzima, ili aweze kulitumikia taifa letu."
Nyumba ya Bibi Zhang Lizhi ni yenye ukubwa wa mita 20 za mraba tu. Sura ya sakafu ya chumbani ni ya saruji, televisheni na jokofu vilinunuliwa miaka 10 iliyopita alipofunga ndoa. Nje ya nyumba hiyo kuna chumba kidogo kinachotumika kama jiko, hakuna choo binafsi, inawabidi waende kwenye choo cha mtaani. Hata hivyo Bibi Zhang Lizhi anaridhika na maisha ya hivi sasa, hususan mwanaye anayesoma katika shule ya msingi anampa mama huyo furaha kubwa kutokana na tabia yake nzuri na uhodari wake katika masomo.
Mume wa Bibi Zhang Lizhi anaitwa Ye Haihua. Yeye ni mfanyakazi, na si hodari katika kuongea. Mke wake alipozungumza alikuwa amekaa kando na kusikiliza, uso wake ukionesha tabasamu. Bwana huyo alimwambia mwandishi wa habari, akisema  "Naona mke wangu ni mtu mwenye upendo na nia imara, ana uhusiano mzuri na wenzake."
Tarehe 28 Julai mwaka huu ilikuwa siku ya kuadhimisha miaka 30 tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mjini Tangshan. Bibi Zhang Lizhi alipanga kwenda kwenye kiwanja cha mnara wa kumbukumbu wa watu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi mjini Tangshan ili kuwaomboleza jamaa zake waliokufa kwenye maafa hayo.
Bibi Dang Yuxin pia alikuwa na mpango wa kwenda kiwanjani pamoja na mtoto wake, alisema angetaka kumwambia mtoto wake maelezo kuhusu bibi na babu zake. Xu Weiwei alitaka kukumbuka siku hiyo kwa njia nyingine, ambapo aliandaa harakati za kuadhimisha miaka 30 ya kutokea kwa tetemeko la ardhi kwa ajili ya kampuni moja. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika maandalizi yake angeadhimisha siku hiyo kwa ngoma na nyimbo kwani hivi sasa lengo la harakati hizo si kuadhimisha miaka 30 ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, na wala sio kuadhimisha miaka 30 ya kupoteza jamaa, bali ni kupongeza maisha mapya ya watu wa Tangshan katika kipindi cha miaka hiyo 30 iliyopita.
Alisema  "Kitu tunachokumbuka ni mabadiliko ya Tangshan katika miaka 30 baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, ambapo maisha ya watu yameinuka. Tunapaswa kujitoa kutoka kwenye huzuni, kuchapa kazi na kujenga familia zetu na nchi yetu. Si vizuri kufikirifikiri tu mambo yaliyopita katika miaka mingi iliyopita."
Hivi sasa tukitembea barabarani mjini Tangsha, miongoni mwa wapita njia mbalimbali, labda wapo watoto yatima waliopoteza wazazi kwenye tetemeko la ardhi miaka 30 iliyopita, baadhi yao wamekuwa wamiliki wa kampuni, wengine ni maofisa wa serikali, wafanyakazi wa viwandani, au wajasiriamali. Utawaona wakiwa watulivu, kwani watu wa Tangshan walionusurika kwenye maafa hayo wana matumaini zaidi juu ya maisha, na maisha yanayoendelea siku zote huleta matumaini.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-17