Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-18 15:54:52    
Mawasiliano kati ya wanawake wa China na nchi za Afrika yaimarika siku hadi siku

cri

Mawasiliano ya kirafiki kati ya wanawake wa China na nchi za Afrika ni sehemu moja muhimu ya sera ya kidiplomasia ya China kwa Afrika. Katika muda wa nusu karne iliyopita tangu China na nchi za Afrika zianzishe uhusiano wa kibalozi, mawasiliano kati ya wanawake wa China na wa nchi za Afrika yamepata maendeleo makubwa. Kutokana na hali ilivyo sasa, mawasiliano ya wanawake wa China na wa nchi za Afrika yanaimarika na kuelekea kwenye ngazi tofauti, sekta nyingi na njia mbalimbali.

Wachina na waswahili wote wana msemo unaosema: "Milima haikutani, binadamu hukutana". Ingawa China na nchi za Afrika ziko mbali kijiografia, lakini mawasiliano ya kirafiki kati ya wanawake wa pande hizo mbili yalianzia enzi na dahari. Mwezi Julai mwaka 1954, shirikisho kuu la wanawake la China liliualika ujumbe wa wanawake wa chama cha ANC cha Afrika ya Kusini kuitembelea China, jambo hilo lilionesha vya kutosha uungaji mkono wa wanawake wa China kwa wanawake wa Afrika waliopigania ukombozi. Baada ya mkutano wa wanawake wa Asia na Afrika kufanyika mwezi Februari mwaka 1958 huko Cairo nchini Misri, mawasiliano kati ya wanawake wa China na Afrika yalikuwa yanaimarika siku hadi siku. Marehemu Zhou Enlai aliyekuwa waziri mkuu wa China aliwahi kukutana na baadhi ya viongozi wanawake wa Afrika walipofanya ziara nchini China.

Jambo linalostahiki kutajwa ni kwamba, baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji wa mlango, China imepata maendeleo makubwa ya kiuchumi, na nguvu yake imeimarika siku hadi siku, kazi ya kufanya mawasiliano kati ya wanawake wa China na wa nchi za nje imepata maendeleo ya haraka, ambapo mawasiliano kati ya wanawake wa China na wa nchi za Afrika pia yanaongezeka siku hadi siku. Mwaka 1995, mkutano wa nne wa wanawake wa dunia wa Umoja wa Mataifa ulifanyika hapa Beijing, taarifa ya Beijing na mpango wa utekelezaji uliopitishwa kwenye mkutano huo umeleta athari kubwa kwa nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Afrika. Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lililoanzishwa mwaka 2000 kutokana na mapendekezo ya China na nchi za Afrika, limeweka mazingira mazuri ya kuzidisha ushirikiano kati ya wanawake wa China na nchi za Afrika. Katika miaka ya karibuni, shirikisho kuu la wanawake la China kila mwaka linapokea ujumbe kadhaa wa wanawake kutoka Afrika, pia linatuma ujumbe wa ngazi ya juu wa wanawake kutembelea nchi za Afrika ili kutafuta kwa pamoja usawa, maendeleo na amani. Ujumbe wa wanawake wa China ulipofanya ziara katika nchi za Afrika ulikaribishwa kwa ukarimu na wanawake na mashirika ya wanawake ya Afrika.

Amani na maendeleo ni mambo makubwa mawili yanayofuatiliwa duniani. Zikiwa nchi zinazoendelea, China na nchi za Afrika zote zinakabiliwa na majukumu ya kustawisha uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wao. Ili kuwaunga mkono wanawake wa Afrika wajiendeleze, na kuyasaidia mashirika ya wanawake ya nchi za Afrika yaendeshe vizuri shughuli zao, shirikisho kuu la wanawake la China kila mwaka linatoa kadiri iwezekanavyo misaada ya vifaa na teknolojia zinazohitajiwa sana na mashirika ya wanawake ya Afrika, kama vile kompyuta, mitambo ya kurudufu, vyerehani, mitambo ya kusaga nafaka, vifaa vya kusomea kwa wanafunzi, vitu vya matumizi ya kimaisha na dawa?ili kuwasaidia wanawake wa nchi za Afrika kuboresha mazingira yao ya kazi, kuinua uwezo wao wa kuzalisha mali, kuongeza mapato na kupambana na maradhi.

Tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1999, huko Conakry, mji mkuu wa Guinea, wanawake zaidi ya 300 wakiwemo mke wa rais, mke wa waziri mkuu, waziri wa wanawake na maofisa wa kiserikali wa nchi hiyo walikusanyika kwenye sherehe ya ufungaji wa semina iliyoandaliwa na kikundi cha ushonaji nguo na utarizi kilichotumwa na shirikisho kuu la wanawake la China. Wanawake walioshiriki kwenye semina hiyo wakiwa wamevaa nguo walizoshona wenyewe, na kushika vyeti waliokabidhiwa na mke wa rais, walitiwa moyo sana hata wakitokwa machozi ya furaha. Waziri wa wanawake wa nchi hiyo alisema: "Wachina husema, 'kukufundisha kuvua samaki ni bora zaidi kuliko kukupa samaki '. Shirikisho kuu la wanawake la China si kama tu limetupa samaki, bali pia limetufundisha namna ya kuvua samaki. Wachina ni marafiki zetu wa daima."

Hadi sasa shirikisho kuu la wanawake la China limeshatoa misaada mara zaidi ya 80 kwa wanawake wa nchi zaidi ya 40 za Afrika, si kama tu limeimarisha uhusiano kati ya shirikisho hilo na mashirika ya wanawake ya nchi zinazopewa misaada, bali pia limezidisha maelewano na urafiki wa kindugu kati ya wanawake wa China na nchi za Afrika.

Hivi sasa shirikisho kuu la wanawake la China limeanzisha uhusiano na mashirika ya wanawake zaidi ya 100 ya nchi 46 za Afrika, kutokana na maendeleo ya uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi kati ya China na nchi za Afrika, mawasiliano kati ya wanawake wa China na wa Afrika bila shaka yataongezeka siku hadi siku, ambayo yatasaidia kuongeza athari za China katika nchi za Afrika, na kuzidisha urafiki kati ya watu wa China na wa nchi za Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-18