Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-21 15:16:56    
Mwongoza filamu Ning Hao

cri

Filamu ya "Hadithi ya Jade" iliyooneshwa hivi karibuni nchini China imeleta mapato mara tatu kuliko yuan milioni tano iliyowekezwa, mwongoza filamu hiyo Bw. Ning Hao alijulikana ghafla na kuwa mtu wa kuvutia sana wawekezaji wa filamu.

Filamu ya "Hadithi ya Jade" ni hadithi ya kuchekesha, ikieleza hali katika mji wa Chongqing wa China, ambayo kiwanda fulani cha vitu vya sanaa za mikono kilichokuwa karibu kufilisika kiligundua jade moja yenye thamani kubwa wakati nyumba ilipobomolewa. Ili kufufua kiwanda hicho uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuuza jade hiyo kwa mnada. Lakini baada ya habari ya ugunduzi wa jade hiyo kuenea, majambazi kutoka nchi za nje na wezi wa nchini waliitamani na walitumia kila njia kuiba wakiwa wanashirikiana na kugombana katika mapambano yao dhidi ya mkuu wa idara ya ulinzi ya kiwanda hicho. Baada ya mapambano ya wazi na ya kichini chini na udanganyifu wa jade ya kweli na ya bandia, majambazi na wezi hao walichezewa vibaya.

Filamu ya "Hadithi ya Jade" imewaeleza watu wa aina kadhaa vilivyo, kwa mfano mtu asiyesoma anaongea maneno ya wenye elimu ya juu mahali pasipofaa, na mazungumzo yao yanasemwa kwa lahaja ya mkoa Sichuan. Watazamaji wanachekeshwa toka filamu inapoanza. Mwongoza filamu hiyo Ning Hao alipoulizwa na waandishi wa habari kama wachezaji walipoigiza filamu hiyo walikuwa wanacheka sana, alisema, "Kwa kweli hatukucheka, kwani kabla ya kuiga tulikuwa tumefahamu tutaiga vipi na kusema maneno gani, mtu anapofanya kazi kwa makini hawezi kucheka."

Ning Hao ni mwongoza filamu mwenye bahati sana, alipata msaada wa fedha kutoka "Mfuko wa Waongoza Filamu Vijana wa Asia" ulioanzishwa na mwimbaji nyota wa Hong Kong, Liu Dehua, mwaka jana, alitumia fursa hiyo na amefanikiwa katika ushindani mkubwa wa filamu nchini China.

Ning Hao ana umri wa miaka 29, alizaliwa katika mji wa Taiyuan mkoani Shanxi. Alipokuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya chini alipenda sana kuchora picha, na pia aliwahi kuunda bendi moja ndogo, kutokana na hali yake hiyo mwalimu wake alisema alikuwa hashughuliki na kazi aliyotakiwa kufanyika. Kutokana na upendo wake wa uchoraji, Ning Hao hakuendelea na masomo ya sekondari ya juu, bali alijiunga na shule ya uchoraji picha. Mwaka 1996 alipohitimu shule hiyo alikabiliwa na tatizo la kuchagua kazi. Alisema, "Baada ya kumaliza shule ya uchoraji picha nilifanya kazi katika Kundi la Tamthilia la Mji wa Taiyuan, lakini niliondoka kutoka kundi hilo kabla sijamaliza mwaka mmoja kwa sababu nilinona siwezi kuwa na maendeleo ya kazi katika kundi hilo. Kabla ya kuondoka kutoka kwenye kundi hilo nilitafakari sana, nilipowaambia wazazi wangu nia yangu ya kutaka kuacha kazi ilikuwa ni vigumu kwao kunielewa, mwishowe baba yangu alinipa yuan elfu mbili na kusema, 'chukua hizi, uondoke'."

Mwanzoni wazazi wake walidhani atatembelea mahali pengine na atarudi baada ya kuishiwa na pesa, lakini hakurudi. Alikuja Beijing, alipanga chumba kimoja kilicho chini ya ardhi akaanza kupanga maisha yake ya siku za usoni. Baadaye alikwenda kujifunza upigaji picha kwa kamera, kuwapigia picha wachezaji nyota na kuongeza masomo katika Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing. Hivyo, hatua kwa hatua aliingia katika nyanja ya filamu. Mwaka 2002, filamu yake ya "Ardhi ya Majani" ilimvutia mwimbaji nyota Liu Dehua ambaye aliiwekeza kwenye filamu hiyo. Kutokana na uendeshaji mzuri wa filamu hiyo Liu Dehua alimworodhesha kwenye "Mfuko wa Waendeshaji Filamu Vijana wa Asia".

Kuhusu mafanikio ya filamu yake ya "Hadithi ya Jade" Ning Hao alisema, tumaini lake lilikuwa ni kutengeneza filamu ya burudani na kupata mapato mazuri kutoka mauzo ya tiketi. Alisema, "Baada ya kufahamu sekta ya filamu ilivyo kisiwani Taiwan nilichagua kupiga filamu hiyo. Naona kwamba sekta ya filamu lazima iwe na mapato ili ijiendeleze yenyewe bila kutegemea msaada wa serikali au mashirika fulani, ama sivyo sio tu filamu za kibiashara haziwezi kuendelea, hata mwishowe filamu za michezo ya sanaa ya China zitapoteza msingi na kutoweka. Kwa hiyo tunajitahidi kupiga filamu inayopokelewa vizuri katika soko la filamu, kama filamu uliyopiga ikidorora sokoni utawezaje kuishi?"

Hali ilivyo ni kwamba filamu ya "Hadithi ya Jade" ni filamu inayohitajika katika soko la filamu nchini China. Muda mfupi baada ya kuoneshwa kwa filamu hiyo, Kampuni ya Wakala wa Filamu ya Marekani imenunua haki ya kuonesha filamu hiyo kwa mkataba. Filamu nyingine atakayopiga ni "Gari Jekundu la Mashindano ya Mbio", ni filamu ya kuchekesha kwa kuonesha maisha ya kina yahe, sasa filamu hiyo imepata uwekezaji.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-21