Je, unataka kuanzisha duka lako kwenye mtandao wa Internet? Hivi sasa hapa nchini China wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanavutiwa na mpango huo na baadhi yao wameanza kuutekeleza.
Tovuti moja ya China iitwayo Taobao inaongoza nchini China miongoni mwa tovuti zinazotoa huduma za kuandaa mazingira ya biashara kati ya watu binafsi. Habari zilizopatikana kwenye tovuti hiyo zinasema, kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni 22 waliojisajili kwenye tovuti hiyo, asilimia 40 ni wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu. Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanafunzi wengi zaidi wa vyuo vikuu vya China wamejiingiza katika shughuli za kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet.
Bw. Yang Zhongkui wa ofisi ya habari ya tovuti ya Taobao alipohojiwa, alisema "Tunawaunga mkono wanafunzi wa vyuo vikuu wajaribu kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet kwa masharti kwamba shughuli hizo za biashara zisiathiri masomo yao, kwani kwa upande mmoja shughuli hizo zinaweza kuwaongezea uwezo wa kushirikiana na watu wa hali mbalimbali wa jamii, na kuwapa mawazo ya kibiashara. Kwa upande mwingine hii ni njia ya kujiajiri."
Kijana Li Ao ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu kwenye Chuo kikuu cha lugha cha Beijing. Alisema "Rafiki yangu mmoja alianzisha duka kwenye mtandao wa Internet alipokuwa anasoma katika chuo kikuu, sasa shughuli zake zinaendelea vizuri, mwenyewe ameanzisha kampuni." Kijana huyo Li Ao alianzisha duka lake kwenye tovuti ya Taobao mwaka 2004, sasa ni miaka miwili imepita, anaonekana kuwa ni mfanyabiashara mwenye uzoefu mwingi.
"Kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet ni kitu kipya, ambapo wenye maduka hawatakiwi kulipa kodi na kuna hatari ndogo ya kibiashara." Bw. Li Ao alisema mtandao unaandaa mazingira mazuri kwa wanafunzi kuendesha maduka yao, kwa mfano shughuli hizo hazichukui muda mwingi wala juhudi kubwa, mwenye duka mwenyewe anaweza kushughulikia kazi zote.
Kijana huyo pia alitaja ubora mwingine wa kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet kuwa, biashara zinafanyika nyumbani, kwa hiyo wateja wanafurahia uharaka wa biashara hizo.
Wanafunzi wa vyuo vikuu kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet, mbali na kujipatia pato fulani la kuboresha maisha yao, jambo muhimu zaidi ni kuimarisha uwezo wao mbalimbali.
Xiao An ni kijana anayesomea mauzo ya soko katika Chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Wuhan, yeye pia ana duka kwenye mtandao wa Internet. Alieleza maoni yake kuwa anatumia ujuzi aliopata darasani katika shughuli za kuendesha duka kwenye mtandao wa Internet, kwa mfano kuingiza bidhaa kunatumia mbinu ya kufanya mazungumzo ya kibiashara, anatumia ujuzi wa mauzo ya soko katika matangazo ya kibiashara ya bidhaa zake, pamoja na ujuzi mwingine kama vile hesabu na mbinu za kuwasiliana na wateja. Hivi sasa kijana huyo ana uzeofu mkubwa katika kuendesha duka lake kwenye mtandao wa Internet.
Bw. Li Ao alisema katika mapumziko ya siku za joto, wanafunzi wenzake wengi walishiriki kwenye shughuli za kuanzisha na kuendesha maduka kwenye mtandao wa Internet. Alieleza matumaini yake kuwa biashara ya maduka hayo itapamba moto. Alisema hatasimamisha shughuli za duka lake baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, ana mpango wa kufanya kazi na kuendesha duka lake kwa wakati mmoja.
Wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanasema ili kufanikisha maduka yao kwenye mtandao wa Internet, inawabidi kuyapa maduka hayo majina yanayowavutia watu. Mbali na hayo wanafunzi wa vyuo vikuu wanawavutia wateja kwa matangazo ya kibiashara yenye uvumbuzi. Pia wanatangaza anuani na bidhaa za maduka yao kwenye BBS au vipindi vya mjadala, ili kuwavutia watu wanaotembelea tovuti.
Imefahamika kuwa sasa kuna maduka laki 5 na elfu 50 kwenye tovuti ya Taobao inayotoa huduma kwa wajasiriamali wenye nia ya kufanya biashara kwa kupitia mtandao wa Internet. Maduka hayo yanauza bidhaa zaidi ya milioni 30, na thamani ya biasahra kwa siku ni zaidi ya Yuan milioni 47, sawa na dola za kimarekani milioni 6. Na tovuti hiyo inatembelewa na watu milioni 110 kila siku.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-24
|