Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-25 14:55:27    
China ni rafiki mkubwa wa jumuiya ya SADC

cri

Tarehe 17 Agosti mwaka huu ujumbe wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC ulioko nchini China ulifanya mkutano wa kuadhimisha miaka 26 tokea jumuiya hiyo ianzishwe. Wanadiplomasia wa nchi wanachama wa SADC, ofisa husika wa wizara ya mambo ya nje ya China, wajumbe wa makampuni na waandishi habari wa vyombo vya habari vya China wapatao mia moja hivi walihudhuria mkutano huo. Mwenyekiti wa ujumbe wa SADC nchini China, ambaye pia ni balozi wa Mauritius nchini China Bwana Paul Chong Leung alitoa hotuba, ambapo kaimu balozi wa Botswana nchini China Bwana Gobe Pitso alitoa mhadhara kuhusu hali ya maendeleo ya SADC na ushirikiano kati ya jumuiya hiyo na China.

Bw. Paul Chong Leung alipongeza sana uhusiano wa kirafiki kati ya China na Jumuiya ya SADC. Akisema:

"Tangu jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika ianzishwe, serikali ya China imekuwa rafiki mkubwa wa jumuiya hiyo, China siku zote inafuatilia maendeleo ya jumuiya hiyo na kuhudhuria mikutano ya ngazi ya juu ya jumuiya hiyo kama nchi mchunguzi. Mwezi Desemba mwaka 2004, serikali ya China na SADC zilisaini kumbukumbu ya maelewano, ikisisitiza haja ya kufanya ushirikiano wa kunufaishana kati ya pande hizo mbili katika biashara, uwekezaji, uchumi, jamii na sayansi na teknolojia, pia imedhihirisha kuwa maelewano kati ya serikali ya China na SADC yanaimarika siku hadi siku."

Bwana Paul alisema katika miaka ya karibuni, China imepata ongezeko kubwa la uchumi, thamani ya biashara kati ya China na nchi za kusini mwa Afrika imeongezeka mwaka hadi mwaka. Alieleza matumaini yake kuwa, serikali ya China itaanzisha utaratibu rasmi wa kubadilishana maoni moja kwa moja kati yake na ujumbe wa SADC nchini China, ili kufuata vizuri zaidi kanuni za kumbukumbu za maelewano. Akisema:

"Tunajua kuwa China itazidisha ushirikiano kati yake na nchi za Afrika kwa kupitia baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika inatarajia kushirikiana na China katika miradi mingi ya kikanda. Jumuiya hiyo pia inapenda kufanya ushirikiano na makampuni ya China, na kuwakaribisha wanakampuni wa China watembelee nchi za kusini mwa Afrika, ili kufanya ukaguzi kuhusu fursa za kibiashara na vivutio vya utalii vya huko."

Kaimu balozi wa Botswana nchini China Bw. Gobe Pitso alisema, nchi wanachama wa SADC zitafuata kanuni za kumbukumbu ya maelewano iliyosainiwa kati ya SADC na Jamhuri ya Watu wa China, na kuimarisha ushirikiano kati yake na China katika sekta mbalimbali juu ya msingi wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika na mpango wa ushirikiano mpya wa maendeleo ya kiuchumi barani Afrika NEPAD. Akisema:

"Sekta muhimu za ushirikiano kati ya SADC na China ni uendelezaji wa nguvukazi, ujenzi wa miundo mbinu, kilimo, viwanda, na upashanaji habari, ambapo maendeleo ya nguvukazi ndiyo sekta inayowekewa mkazo zaidi."

Ofisa kutoka wizara ya mambo ya nje ya China Bi. Guan Ruoxuan alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya waziri wa mambo ya nje ya China Bwana Li Zhaoxing, alipotoa risala kwenye mkutano huo alisema, jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika si kama tu ni jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya kikanda, bali pia imeshiriki katika usuluhishaji wa migogoro ya kikanda. Hii inamaanisha kuwa jumuiya hiyo imeanza kutoa mchango mkubwa zaidi katika sekta za siasa, uchumi na mambo mengine. Serikali ya China siku zote inatilia maanani kukuza uhusiano wa kirafiki kati yake na SADC, hasa kwenye maendeleo ya uchumi. Akisema:

"Kama nijuavyo kuwa, kauli mbiu ya mkutano huo ni "biashara, uwekezaji na utalii" ambayo inaendana na mkutano wa tatu wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, pia imeonesha kuwa ushirikiano kati ya China na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika umeongezewa mambo mengi zaidi. Naona ushirikiano wa kunufaishana kati yetu utadumu kwa muda mrefu."

Bi.Guan alisema kati ya nchi wanachama 14 za SADC, nchi 9 zimekuwa nchi zinazoruhusiwa kuwapokea watalii kutoka China, ambazo ni Afrika ya kusini, Tanzania, Namibia, Lesotho, Zambia na Zimbabwe. Aliwashawishi wachina wenye hamu ya kufahamu hali halisi ya Afrika waende kwenye nchi hizo.

Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika ina nchi wanachama 14, ambazo ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika ya kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Madagascar. Shelisheli iliyojitoa kutoka kwenye jumuiya hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi sasa imeomba kurudi tena katika jumuiya hiyo.

Kwenye mkutano wa 26 wa wakuu wa jumuiya hiyo uliofanyika tarehe 17 mwezi Agosti, huko Maseru, Lesotho, wakuu wa nchi zote wanachama walijadili kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii, kuharakisha mchakato wa utandawazi wa sehemu hiyo na kupunguza umaskini, utekelezaji wa mpango wa ushirikiano mpya wa maendeleo ya Afrika NEPAD, namna ya kushughulikia maambukizi ya homa ya mafua ya ndege na ujenzi wa makao makuu mapya ya jumuiya hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-25