Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-25 19:50:00    
Madaktari wa China wanaofanya kazi nchini Lesotho

cri

Lesotho ni nchi yenye vivutio vingi iliyoko kwenye uwanda wa juu kusini mwa Afrika. Katika miaka kumi iliyopita, madaktari wa China wanatoa huduma za matibabu kwa wananchi wa Lesotho wakionesha ustadi wao wa matibabu, maadili mema na moyo mkunjufu. Wakiwa wametoa mchango mkubwa kwa afya za watu wa Lesotho, na kwa vitendo halisi wameonesha urafiki wa watu wa China kwa watu wa Lesotho.

Lesotho ni moja ya nchi zenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi, asilimia 30 ya watu wa nchi hiyo wameambukizwa virusi vya Ukimwi, na asilimia 70 ya wagonjwa waliolazwa hospitali wana virusi vya Ukimwi. Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za nchi hiyo wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya ukimwi, lakini katika hospitali ya Kundu ambayo ni hospitali kubwa kabisa ya umma ya Lesotho, madaktari 15 wa China kila siku wanatekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wagonjwa bila ya kulegea.

Bwana Wan Naiming ni daktari wa mifupa, siku moja katika upasuaji mmoja wa dharura, msaidizi wake alipomkabidhi kisu cha upasuaji kwa bahati mbaya alikatwa mkononi. Katika kukabiliana na hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi, daktari Wan alizingatia kwanza mgonjwa aliyelazwa kwenye kitanda cha upasuaji, alifunga haraka jeraha lake kwa kitambaa na kuendelea na upasuaji. Baada ya operesheni mgonjwa huyo alipimwa na kuthibitishwa kuwa ana virusi vya Ukimwi, ambapo daktari Wan alipaswa kutumia dawa dhidi ya virusi vya Ukimwi, dawa hiyo ilileta athari mbaya kwa afya. Msaidizi wake alisikitishwa kutokana na kosa alilofanya, lakini daktari Wan alimfariji msaidizi wake badala ya kumlaumu. Lililomfurahisha ni kwamba baada ya miezi kadhaa iliyofuata, daktari Wan alipimwa virusi vya Ukimwi mara kadhaa, na kuondolewa uwezekano wa kuambukizwa virusi vya Ukimwi. Hivi sasa daktari Wan anaendelea kufanya kazi katika wodi za wagonjwa wa mifupa. Alipoulizwa kuhusu tukio hilo alitabasamu akisema: "Limeshapita, nikiwa daktari hakika nitakabiliwa na hatari za aina mbalimbali."

Bwana Wan si daktari pekee aliyekumbwa na majeraha la mkononi wakati wa kuwafanyia ugonjwa upasuaji. Madaktari wengine 7 wa China waliofanya kazi nchini Lesotho pia waliwahi kukatwa kwa kisu mikononi, lakini wote hawakurudi nyuma kutokana na hofu ya kukumbwa na maambukizi ya Ukimwi.

Kutokana na juhudi za madaktari wa China, hospitali ya Kundu kwa mara ya kwanza ilianzishwa idara ya akyupancha na idara ya uropoiesis, kukamilisha zaidi mfumo wa afya wa Lesotho. Kuanzishwa kwa idara ya akyupancha kuliwaletea watu wa Lesotho matibabu ya jadi ya Kichina yenye ufanisi. Tokea idara ya akyupancha ianzishwe mwaka 2003, baadhi ya magonjwa ambayo ni sugu ya matibabu ya kimagharibi yametibiwa kwa sindano za kichina, matibabu ya akyupancha yanapendwa sana na watu wa Lesotho, yamekuwa matibabu yanayokubaliwa na mfalme hadi wakazi wa kawaida wa nchi hiyo.

Chumba cha utoaji tiba ya akyupancha ya hospitali ya Kundu, kila siku kinajaa kwa wagonjwa wanaosubiri matibabu. Mgonjwa mmoja aliyekuwa anaumwa magoti alisema, baada ya kupewa matibabu ya akyupancha mara tatu tu, maumivu yake yametoweka kimsingi, akisema: "Akyupancha ya China ina ufanisi sana, natumai kuwa, madaktari wa China watafanya kazi hapa daima." Kijana mwingine aliyepewa matibabu kwa akyupancha alinyosha mikono yake kwa furaha akisema: "Matibabu ya akyupancha yana ufanisi wa ajabu, sasa naona nina nguvu ya uhai kama watoto walivyo."

Kwa miaka mingi madaktari wa China wamewasaidia watu wengi wa Lesotho kuondoa maumivu ya magonjwa wakiwemo wanafamilia wa mfalme, wa nchi hiyo. Mwezi Januari mwaka 2005 waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing alipofanya ziara nchini Lesotho, mfalme wa nchi hiyo Letsie III alimwambia kuwa wananchi wa Lesotho wanashukuru kwa dhati misaada inayotolewa na China, madaktari wa China wanajulikana sana nchini humo.

Mwezi Desemba mwaka 2005, waziri mkuu wa Lesotho Bwana Pakalitha Mosisili alipofanya ziara nchini China alitembelea mkoa wa Hubei uliotuma kikundi cha madaktari nchini Lesotho, kukutana na jamaa za madaktari wanaofanya kazi na madaktari waliowahi kufanya kazi nchini Lesotho. Bw. Mosisili alisema madaktari wa China wametoa mchango mkubwa kwa urafiki kati ya China na Lesotho, yeye mwenyewe pia aliwashukuru madaktari wa China. Alisema atafanya mambo halisi kwa madaktari wa China wanaofanya kazi nchini Lesotho kama vile kuwagharamia wake za madaktari hao kuwatembelea waume zao nchini Lesotho.

Madaktari wa China wamesema kuwa wanafanya mambo yote kutokana na utiifu wao kwa taifa lao la China na upendo wao kwa wananchi wa Lesotho. Wataendelea kufanya juhudi kama walivyofanya siku zote na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuimarisha urafiki kati ya wananchi wa China na wa Lesotho.