Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-01 16:26:36    
Kwenda Afrika kutoa Msaada

cri

   

Alama ya harakati ya vijana wanaojitolea nchini China ni mkono wenye umbo wa moyo. Hii inamaanisha kuwa harakati hiyo inawapa watu wanaohitaji msaada mkono wa kuwasaidia, na moyo wa kuwapenda. Hivi sasa vijana wanaojitolea wa China hawawasaidii wachina tu, bali pia wanatoa misaada kwa watu wengine duniani.

Mpango wa kuwapeleka vijana wanaojitolea wa China kutoa huduma nchi za nje ulianzishwa mwaka 2002 na ofisi kuu ya Umoja wa Vijana wa Kikoministi wa China na shirikisho la vijana wanaojitolea la China. Vijana wanaojitolea wa China walichaguliwa na kupelekwa kwenye nchi maskini duniani, kwa njia ya kuandikisha hadharani, kujiandikisha kwa hiari na kupelekwa kwa mpango.

Kundi la kwanza la vijana wanaojitolea lilikwenda Barani Afrika mwaka 2005. Tarehe 4 mwezi Agosti mwaka huo, vijana 12 wanaojitolea kutoka Beijing, Shanghai, Chengdu, Yunnan na miji mingineyo, walikwenda Ethiopia wakiwa na moyo wa kuwasaidia watu wa Afrika. Wakatoa huduma kwa muda wa miezi 6. Huduma hizo zinahusu mafunzo ya matumizi ya gesi ya kinyesi, mafunzo ya lugha ya Kichina na michezo, matibabu na afya na ufundi wa kompyuta. Miongoni mwa vijana hao, watano walikuwa wanafunzi wa shahada ya pili, na mmoja alikuwa mwanafunzi wa shahada ya tatu.

Vijana wanaojitolea wa China walijionea maisha magumu ya watu maskini wa Afrika katika muda wa miezi 6 nchini Ethiopia. Waliwasaidia watu wa nchi hiyo kwa juhudi kubwa wakiwa na imani thabiti na moyo mwema, na kukuza urafiki kati ya China na Afrika. Vijana wanaojitolea wa huduma za matibabu wa China walitoa huduma za matibabu yenye umaalum wa kichina, ikiwemo tiba ya akyupancha. Mwanzoni wagonjwa wa Afrika hawakuelewa aina hiyo ya matibabu na walikuwa wakiiogopa. Kila siku ni watu wawili au watatu tu waliothubutu kupokea matibabu ya aina hiyo. Lakini baada ya muda mfupi, waligundua kuwa tiba ya akyupancha inaweza kutibu magonjwa yasiyotibika kwa matibabu ya kawaida. Wagonjwa wengi waliwaendea vijana wanaojitolea wa China kutibiwa. Hali hiyo iliwataka wachina kuongeza chumba kingine cha matibabu. Vijana wanaojitolea wa uendelezaji wa matumizi ya gesi ya kinyesi walitoa mafunzo husika kwa watu wa Ethiopia, wakifanya uchunguzi wa matumizi ya gesi hiyo nchini humo. Walitafsiri na kuandika vitabu vya matumizi ya gesi ya kinyesi kwa lugha ya Kiingereza, ili kuwafundisha wanafunzi wenyeji elimu husika. Mbali na hayo walitoa semina kuhusu elimu ya kompyuta na uhifadhi wa mazingira. Vijana hawa wanaojitolea wanaofundisha lugha ya Kichina walianzisha darasa la kwanza la kufundisha lugha ya Kichina. Baada ya kufundisha wanafunzi wa kawaida, pia walitoa mafunzo ya lugha ya Kichina kwa wafanyakazi wenyeji wa makampuni ya China nchini Ethiopia, watumishi wa serikali na walimu. Hata balozi wa Ethiopia aliyekuwa amepangiwa kwenda kufanya kazi nchini China pia aliwahi kufundishwa lugha ya Kichina na vijana hao.

Baada ya kazi vijana wanaojitolea wa China waliandika mambo waliyoyaona na kuyasikia walipokuwa nchini Ethiopia kwenye mashairi na shajara zao. Kijana mmoja aliandika kwenye shajara yake kwamba, kutokana na umaskini na maradhi, maisha ya watu wa Ethiopia hayafikii miaka 55. Hali ambayo ilimfanya aelewe zaidi maana ya kazi ya kujitolea na majukumu aliyobeba.

Bidii na michango waliyotoa vijana wanaojitolea wa China iliwafurahisha watu wa Afrika. Pande mbili zilifanya urafiki mkubwa. Baada ya kumalizika kwa muda wa miezi sita, kutokana na kupenda kazi ya kujitolea na watu wa Afrika, vijana wengine wa China waliomba kurefusha muda wao wa kuwepo nchini Ethiopia.

Huduma za kujitolea zilijenga daraja la kuunganisha watu wa China na Afrika. Kupitia kazi halisi vijana hao wanaojitolea wa China walifikisha urafiki mkubwa wa Wachina kwa watu wa Afrika. Sasa hivi kundi la kwanza la vijana wanaojitolea wamerudi nchini China baada ya kumaliza kazi kwa mafanikio, ambapo makundi ya pili na tatu yatapelekwa barani Afrika ili kuendelea na kazi za kirafiki.

Mkuu wa idara ya mawasiliano ya kimataifa ya ofisi kuu ya Umoja wa Vijana wa Kikoministi wa China Bw. Jiang Guangping alieleza kuwa, sasa harakati ya vijana wanaojitolea nchini China inaendelea kwa kasi, na vijana wengi zaidi watajiunga na harakati hiyo, na kutoa mchango kwa kazi ya kuleta amani na maendeleo duniani. Alisema ana imani kwamba, iko siku bendera za harakati ya vijana wanaojitolea ya China zitapepea kwenye sehemu zote zinazohitaji misaada barani Afrika na nchi nyingine duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2006-09-01