Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-04 18:35:02    
Sekta ya televisheni nchini China yaingia katika kipindi cha ushindani mkubwa

cri

Hivi sasa, televisheni imekuwa sehemu muhimu ambayo haiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya wananchi wa China, kwa kutazama televisheni watu wanaweza kufahamu mambo mengi makubwa ya nchini na ya nchi za nje, na kwa kutazama televisheni wanapata burudani za kila aina. Pamoja na aina za uenezi wa habari zinavyoendelea haraka na kuwa nyingi, sekta ya televisheni nchini China inakabiliwa na shinikizo kubwa la ushindani.

Hivi sasa nchini China kuna kituo kimoja cha televisheni cha taifa yaani CCTV na vituo 31 vya mikoa. Katika miaka 2005 na 2006 sekta ya televisheni imekabiliwa na ushindani mkubwa zaidi, na vituo mbalimbali vya televisheni vinajitahidi kubuni vipindi vipya na vimejitokeza vipindi vingi vinavyowavutia watazamaji. Naibu mkuu wa Idara Kuu ya Redio na Televisheni ya China Bw. Hu Zhanfan alieleza,

"Katika miaka ya hivi karibuni, vituo vya ngazi mbalmbali vya televisheni vinajitahidi kubuni vipindi vipya ili kuwavutia watazamaji, na teknolojia za urushaji wa matangazo zimebadilishwa kuwa bora zaidi, shughuli za biashara na za kazi zimepata uzoefu na maendeleo makubwa. Hali ya ustawi ya utangazaji wa televisheni imetokea nchini China."

Kituo Kikuu cha Televisheni cha China CCTV ni kituo pekee cha taifa. Kituo hicho kinashikilia uenezi wa itikadi muhimu na utamaduni katika miaka yote iliyopita, na vipindi vyake kadhaa kama "Taarifa ya Habari", "Mazungumzo kuhusu Matatizo Yanayofuatiliwa", vimekuwa ni vipindi vinavyotazamwa na kila familia. Vipindi vya kituo hicho vinatiliwa maanani sana, kwa mfano, vipindi vyote vinavyotangazwa katika idhaa ya CCTV-1 lazima viwe na mvuto mkubwa na wakati wote na vinapimwa kwa "idadi ya watazamaji" ili kuhakikisha vipindi vinavyorushwa ni bora. Mwaka 2005, CCTV ilitangaza moja kwa moja "safari ya chombo cha anga Shenzhou No. 6", matangazo hayo yalipata watazamaji wengi kuliko matangazo mengine. Mwaka 2006 mashindano ya soka ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza yalitangazwa na kuoneshwa moja kwa moja. Kwa mujibu wa uchunguzi, kwa wastani watu milioni 650 walitazama mashindano hayo kwa siku nchini China. Ili kukidhi haja tofauti za watazamaji, CCTV inajitahidi kuboresha vipindi kwa aina zake, mkuu wa kituo hicho Bw. Zhao Huayong alieleza,

"Ili kuridhisha watazamaji wenye hali tofauti na wanaopenda mambo tofauti tumeimarisha vipindi kwa namna nyingi. Tokea mwaka 1999 hadi 2004 CCTV imekuwa na idhaa 15 na idhaa moja ya mchanganyiko. Licha ya idhaa hizo 16 pia imeanzisha idhaa 10 za kulipia, kwa jumla idhaa hizo zimekuwa na vipindi 400 ambavyo vinapatikana katika nchi na sehemu 120 duniani.

Vipindi vya burudani ni vipindi vinavyovutia watazamaji wengi na matangazo mengi ya biashara. Mapema katika mwaka 1997, kipindi cha "Bwawa la Furaha" kilipotangazwa na kituo cha televisheni cha mkoa wa Hunan mara kiliwavutia sana watazamaji. Kipindi hicho kilikusanya opera, nyimbo na dansi, na kimewashirikisha wachezaji wengi nyota na pia watu wa kawaida. Kuanzia mwaka 2005 kila mwaka kituo hicho kinatangaza kipindi chake cha "Maonesho ya Wanawake Hodari", kipindi hicho kinasifiwa sana na wataalamu na kinawavutia wafanya matangazo ya biashara wengi kuwekeza. Kuhusu hali hiyo, profesa wa Chuo Kikuu cha Qinghua Bw. Yin Hong alisema,

"Kipindi kama hicho ambacho kinafuatiliwa sana na watazamaji wengi kilibuniwa kutokana na athari ya vipindi vya televisheni vya nchi za nje. Hii ina maana kuwa sekta ya televisheni nchini China inajitahidi kujitafutia uhai na maendeleo kwa shinikizo la mazingira ya utandawazi wa duniani."

Aidha, prof. Yin alisema hali ya baadaye ambayo vituo vingi viliiga kipindi hicho, imeonesha kuwa uvumbuzi wa vipindi vipya nchini China bado ni dhaifu."

Kwenye televisheni nchini China watu pia wanaweza kuangalia vipindi mbalimbali kutoka nchi za nje, kwa mfano, matangazo ya moja kwa moja ya mashindano ya ligi ya soka nchini Ujerumani, Ufaransa na Italia, filamu, na picha za katuni na maonesho ya mambo mbalimbali. Hivi sasa matangazo ya vituo zaidi ya 30 vya nje ya China yameoneshwa nchini China.

"Espn Star Sports" ni kituo kinachoshughulikia matangazo ya michezo duniani, idara hiyo imekuwa na ushirikiano na China. Mkuu wa idara hiyo Bw. Jamie Davis alisema,

"Nafurahi kurudi tena nchini China, hapa nimeona mabadiliko makubwa ya matangazo ya televisheni, na vipindi vya vituo vya mikoa pia vimebadilika na kuwa vya aina nyingi. Hivi sasa tunachotaka kufanya ni kupanua upeo wetu na kutengeneza vipindi vingi vya televisheni kwa lugha ya Kichina na kuwaonesha watazamaji wetu wa China."

Pamoja na hayo, vipindi vya televisheni vya China pia vinapendwa na watazamaji wa nchi za nje. Kwenye biashara ya vipindi vya televisheni, kwa makubaliano kundi la matangazo ya televisheni mkoani Zhejiang litaliuzia shirika la Israel picha za katuni za watoto.

Sekta ya televisheni nchini China inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo na pia changamoto kubwa. Kwa upande mmoja maendeleo ya haraka ya uchumi nchini China yameiletea sekta hiyo fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina za uenezi wa habari zimekuwa nyingi, kwa mfano, televisheni kwenye mtandao wa internet, simu za mkononi zinaendelea haraka na makundi mengi ya televisheni ya nchi za nje yameingia kwenye soko la televisheni nchini China, hali kama hiyo imekuwa shinikizo kubwa kwa sekta ya televisheni na filamu nchini China. Ili kuongeza nguvu za ushindani sekta ya televisheni na filamu nchini China lazima iendeleze uvumbuzi bila kusita ndipo inapoweza kukidhi mahitaji ya watazamaji yanayoongezeka siku hadi siku, na kuwavutia wawekezaji wa matangazo ya biashara.