Hekalu la Chongsheng la sehemu inayojiendesha ya kabila la wabai la Dali mkoani Yunnan, kusini magharibi ya China ni hekalu la kale lililojengwa zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Hivi karibuni serikali ya huko imekarabati hekalu hilo na kufanya sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha kwenye hekalu hilo. Baada ya kukarabatiwa, sio kama tu Hekalu la Chongsheng linaonekana kuwa ni hekalu lenye heshima na fahari la kifalme, bali pia linabaki na mtindo wa kabila la wabai wanaoishi sehemu hiyo.
Siku hiyo saa 12 asubuhi, mwandishi wetu habari alipanda basi kwenda kwenye Hekalu la Chongsheng kushiriki kwenye sherehe kubwa ya kufungua mwangaza wa Buddha iliyoendeshwa pamoja na masufii wakuu 108 kutoka sehemu mbalimbali nchini China, pamoja na nchi mbalimbali za Asia ya kusini mashariki na Asia ya kusini. Alipofika kwenye hekalu hilo, mwandishi wetu wa habari alipanda ngazi ya hekalu, akipita Ukumbi wa Mfalme mbinguni, Ukumbi wa Buddha Ananda, Ukumbi wa Buddha Guanyin na kufika Ukumbi mkuu, kwenye kila ngazi lilitandikwa zulia Jekundu, kandoni mwa pande mbili za ngazi walisisimama waumini wengi wa dini ya kibuddha waliowakaribisha watu walishiriki sherehe, ambapo baadhi yao walivaa mavazi ya kidini, wengine walivaa nguo ya makabila madogomadogo, na baadhi yao walishika kengele zinazofanana na njuga au sanamu za samaki wa mbao za kugonga ambazo zote ni alama za waumini dini ya kibuddha. Bibi Zhang Furu kutoka Dali mkoani Yunnan aliposubiri sherehe ya dini alimwambia mwandishi wetu wa habari kwa furaha.
Niliamka mapema leo asubuhi, na kuja moja kwa moja kwenye Hekalu la Chongsheng kutoka Mji Xincheng kushiriki kwenye sherehe hiyo ya kufungua mwangaza wa Buddha, mimi napenda kutembea kwenye ukumbi wa hekalu hilo.
Hekalu la Chongsheng pia linaitwa Hekalu la Santa, maana yake ya kichina ni hekalu la minara mitatu. Hekalu hilo linakabiliana na Ziwa Erhai lenye maji safi, na nyuma ya hekalu hilo linaegemeana na Mlima Cangshan unaofunikwa na theluji. Kutokana na athari ya matetemeko ya ardhi na vurugu za vita za zama za kale, hekalu hili liliharibiwa vibaya, iliyobaki kikamilifu ni minara mitatu tu. Hekalu la Chongsheng lililojengwa upya si kama tu limebaki na mtindo wake wa zamani, hata vitu vilivyowahi kuhifadhiwa kwenye hekalu la zamani pia vimerudi na kutunzwa kwenye hekalu hilo. Kwa mfano, ngoma kubwa zaidi kuliko nyingine katika mahekalu ya China pamoja na michongo ya maandishi kwenye mbao yenye kimo cha mita 2 na urefu wa mita 117 zinazohifadhiwa ndani ya hekalu hilo, hivi sasa zimefunguliwa kwa watalii.
Bwana Wang Hai na mkewe walifunga safari kutoka Kunming mkoani Yunnan kufika Dali kutazama sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha, walipoona Hekalu la Chongsheng lililojengwa upya, walilisifu sana. Bwana Wang alisema:
Hekalu hilo kweli linaonekana kuwa ni hekalu lenye heshima ya kifalme, ambalo linaegemeana na milima na ziwa, kweli linawavutia watu zaidi. Ni mara yangu ya kwanza kuja hapa kutembelea hekalu hilo, naona hekalu hilo kweli lilijengwa kwa kiwango cha juu nchini China. Kwani niliwahi kwenda sehemu mbalimbali nchini, naona hekalu hilo linavutia watu zaidi kuliko mahekalu mengine.
Katika historia, Hekalu la Chongsheng siku zote lilikuwa kituo cha shughuli za dini ya kibuddha katika sehemu ya kusini mwa China hata sehemu ya Asia ya kusini mashariki, ambapo waumini wa dini ya kibuddha wa Asia ya kusini mashariki walilichukulia hekalu hilo kama ni hekalu kuu la kibuddha. Kwenye sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha iliyofanyika kwenye Hekalu la Chongsheng, masufii wakuu wapatao 108 kutoka China, Korea ya kusini, Singapore, Indonesia, Japan, Thailand, Myanmar, Vietnam, Laos, na Cambodia walisoma msahafu wa dini ya kibuddha, na kuendesha shughuli mbalimbali za kidini ili kufungua mwangaza wa Buddha.
Kwenye sherehe ya kidini, mwandishi wetu wa habari aliona masufii wakuu walisoma msahafu wa dini ya kibuddha, huku wakitumia matawi ya misonobari kuchovya maji, halafu kunyunyiza maji matakatifu, baadaye wakafanya ishara kwa kupiga mara kadhaa angani, yote hayo yalimaanisha baraka na utakatifu. Baada ya kumalizika kwa kusoma msahafu wa dini ya kibuddha, masufii wakuu hao walizungusha kikoo kwa duara moja, ambapo ndipo sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha ilipomalizika vizuri.
Bibi Li Ying mwenye umri wa miaka 65 ni mwamini mtiifu wa dini ya kibuddha, ili kushiriki kwenye sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha iliyofanyika kwenye Hekalu la Chongsheng, alifika Dali kwa ndege siku mbili kabla ya sherehe kufanyika. Bibi Li alisema kwa furaha kuwa, anaona kuwa kwa kushiriki kwenye sherehe hiyo, anaweza kukutana na masufii wakuu wa China na nchi za nje, hii ni fahari kubwa kwa maisha yake yote. Alisema:
Nimewaona masufii wakuu wengi kutoka sehemu mbalimbali nchini China pamoja na mkurugenzi wa Shirikisho la dini ya kibuddha la China, hili ni jambo la fahari sana kwangu, pia nafurahi sana kukutana na masufii wakuu wengi na kupiga picha pamoja nao, mkutano huo kweli umetuvutia sana.
Watalii wengi walimiminikia kwenye Hekalu la Chongsheng, mwandishi wetu wa habari alipoangalia mandhari nzuri ya sehemu iliyo ya hekalu hilo, alikutana na mtalii mmoja kutoka Cyprus aitwaye Mike Jackson. Bwana Jackson alimwambia:
Naona Hekalu la Chongsheng ni zuri sana, nilipoona hekalu kubwa kama hili nilishangaa sana. Hii ni mara yangu ya kwanza kuja kwenye mji huu, lakini nimekuja China mara tano. Mke wangu ni mchina, aliniambia kuwa hekalu hili linavutia sana, hivyo nimekuja kutembelea hekalu hili, kweli nimevutiwa sana.
Bwana Jackson alisema, yeye na mkewe pamoja na mtoto wao mwenye umri wa miaka 6 walifika Dali kutalii. Baada ya kufika Dali, waliambiwa kuwa sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha itafanyika kwenye Hekalu la Chongsheng, hivyo walifika kwa haraka kwenye hekalu hilo. Alisema Hekalu la Chongsheng lilijengwa upya kwenye sehemu ile ile ya hekalu la awali, hili ni jambo zuri lililofanywa na serikali ya China kwa ajili ya waumini wa dini ya kibuddha. Ana imani kuwa baada ya kufanyika kwa sherehe ya kufungua mwangaza wa Buddha, Hekalu la Chongsheng la kale litang'ara kwa mara nyingine tena.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-04
|