Kwa wachina wengi ghuba ya kaskazini nchini China ni mahali panapofahamika sana, lakini vilevile pia ni kama mahali pageni. Panafahamika kwa kuwa mahali hapo panatajwa kila siku mchana katika kipindi cha utabiri wa hali ya hewa cha televisheni; nikisema hapo ni mahali pageni kwa wachina ni kwa sababu sehemu hiyo iko mbali kwenye mpaka wa kusini magharibi mwa China, ambapo ni kama watu hawapafahamu kabisa. Lakini ghuba ya kaskazini sasa inafuatiliwa sana na watu baada ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na umoja wa nchi za kusini mashariki mwa Asia kuanza kufanyika. Katika kipindi hiki cha leo nitawafahamisha kuhusu ushirikiano wa kiuchumi unaopamba moto kila siku ipitayo kwenye ghuba ya kaskazini.
Ghuba ya kaskazini inazungukwa na ardhi za nchi mbili za China na Vietnam pamoja na kisiwa cha Hainan cha China, mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang wa Guangxi ulioko ndani kabisa wa ghuba ya kaskazini, ni moja ya sehemu wanayoishi kwa wingi watu wa makabila madogo madogo nchini China, mkoa huo unapakana na nchi 6 za umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki zikiwemo Malaysia, Indonesia na Brunei. Pamoja na maendeleo ya ujenzi wa eneo la biashara huria kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, ghuba ya kaskazini ambayo zamani ilikuwa haifahamiki sana, sasa imeanza kufuatiliwa na watu.
Hivi karibuni mkutano wa kwanza wa baraza la ushirikiano wa uchumi la ghuba ya kaskazini ulifanyika katika Nanning, mji mkuu wa mkoa wa Guangxi, maofisa wa serikali, wataalamu na wanaviwanda mashuhuri kutoka nchi za Brunei, Indonesia, Malaysia na China, walikuwa na majadiliano kuhusu suala la ushirikiano kwenye kanda ya ghuba ya kaskazini. Mkutano wa baraza la ushirikiano wa uchumi ulitoa taarifa ya mwenyekiti ikisema, kanda ya ghuba ya kaskazini ikiwa ni kitovu cha kuunganisha China na nchi za Asia ya kusini mashariki, inatakiwa kuimarisha ushirikiano katika shughuli za usambazaji wa bidhaa, uzalishaji mali, biashara na uwekezaji ili kuhimiza maendeleo ya kanda hiyo.
Naibu mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Asia Bw. Van Der Linden alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, Benki ya Maendeleo ya Asia ina shauku kubwa ya kuimarishwa kwa ujenzi wa miundo-mbinu ya kanda ya ghuba ya kaskazini
"Mustakabali wa ushirikiano wa kiuchumi wa ghuba ya kaskazini ni mzuri. Kwa mkoa wa Guangxi, Benki ya Maendeleo ya Asia imewekeza katika miradi ya ujenzi wa barabara, kwa mfano tumewekeza katika mradi wa ujenzi wa barabara ya mpakani inayotoka Nanning kwenda Vietnam, barabara ile siyo kuwa ni muhimu tu kwa mkoa wa Guangxi, bali pia ni muhimu sana kwa kuziunganisha China na Vietnam. Kwa hiyo Benki ya Maendeleo ya Asia inapenda kuwekeza kwenye mpango wa maendeleo ya barabara na forodha ili kuhimiza maendeleo ya kanda ya ghuba ya kaskazini."
Barabara aliyotaja Bw. Van Der Linden ni barabara ya kasi ya Nanyou inayoenda kwenye lango la Urafiki lililopo mpakani kati ya China na Vietnam kutoka Nanning, mji mkuu wa mkoa wa Guangxi. Barabara hiyo ilianza kutumika kutoka mwezi Novemba mwaka jana. Barabara hiyo ya kwanza inayounganisha China na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki, ingawa urefu wake haujafikia kilomita 180, lakini muda wa kusafiri kati ya sehemu hizo mbili umepunguzwa kwa nusu kuliko muda uliokuwa ukitumika hapo awali. Kitu muhimu zaidi ni kuwa barabara hiyo imefungua njia inayoenda kwenye sehemu ya Asia ya kusini mashariki na inaisogeza China karibu na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki.
Takwimu za forodha zinaonesha kuwa, baada ya barabara hiyo ya kasi kuanza kutumika, bidhaa zilizoingia na kutoka kwenye lango la Urafiki ziliongezeka kwa 38% kuliko mwaka jana katika kipindi kama hiki. Mkurugenzi wa forodha hiyo bibi Chen Xiaoying alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa matunda ya Thailand, ambayo hayakuwahi kuonekana kwenye sehemu ya lango la Urafiki, sasa yamekuwa yanasafirishwa hadi sehemu za ndani za China kupitia huko tokea mwishoni mwa mwaka jana.
"Hapo zamani matunda yaliyoagizwa kutoka Thailand yaliingia China kwa kupitia baharini na ilihitaji muda mrefu wa kama zaidi ya wiki moja kuyasafirisha. Baada ya barabara hiyo kuanza kutumika, matunda ya Thailand yanasafirishwa kwa kupitia Laos na barabara hiyo ya kasi, muda unaohitajiwa ni kama kati ya siku 3 na 5 hivi."
Watu wengi wanaoishi kando ya barabara hiyo wanasema, baada ya barabara hiyo kuanza kutumika, biashara ya kimataifa ni kama inafanyika mlangoni. Barabara ya kasi ya Nanyou ni kama ufunguo wa kufungua mlango wa biashara kati ya China na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki, na wamepata nafasi nyingi za maendeleo ya uchumi. Naibu mkuu wa mkoa wa Guangxi Bw. Chen Wu alisema, mkoa wa Guangxi utaimarisha ujenzi wa barabara kati ya China na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki.
"tumekuwa na wazo moja: kuna njia za reli na barabara zinazounganisha Nanning na Hanoi, mji mkuu wa Vietnam, halafu kuna njia za kuunganisha Hanoi na Vientiane na Bangkok, kisha zinaenda kusini, kufika Kuala lampur na kufika hadi Singapore ili kuanzisha njia moja kubwa ya kuunganisha mji wa Nanning na Singapore, ambayo itanufaisha sana maendeleo ya uchumi ya nchi hizo."
Licha ya mawasiliano ya barabara, ujenzi wa usambazaji wa bidhaa kwenye bandari za miji mbalimbali iliyoko pembezoni mwa ghuba ya kaskazini unapamba moto hivi sasa. Bandari za Fangchen na Qinzhou za mkoa wa Guangxi zinajenga magati ya makontena na njia zenye kina kirefu za meli na kukamilisha mfumo wa uchukuzi kati ya bandari, njia za reli na barabara. Bandari ya Zhanjiang ya mkoa wa Guangdong inanuia kupanua uwezo wa kushughulikia mizigo hadi tani milioni 55 kutoka tani milioni 26 katika mwaka huu. Bandari ya Sai Kung na bandari ya Haiphong, ambazo ziko kwenye upande mwingine wa ghuba ya kaskazini, nazo zinaendelea kujengwa. Watu husika walikadiria kuwa katika muda wa miaka mitatu ijayo, uwezo wa bandari zilizoko kwenye ghuba ya kaskazini utafikia tani milioni 200, na kuundwa mfumo wa biashara unaohudumia nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki.
Ubora wa ushirikiano wa uchumi wa kanda ya ghuba ya kaskazini pia uko kwenye rasilimali za utalii. Hivi karibuni China ilisaini "Azimio la Ushirikiano wa Utalii wa Kanda ya Ghuba ya Kaskazini" pamoja na miji 9 ya Vietnam, na kutaka kujenga soko la utalii la kikanda lisilo na vizuizi. Hivi sasa njia safari za ndege kati ya bahari ya kaskazini ya China na ghuba ya Halong ya Vietnam imekuwa njia ya dhahabu ya maendeleo ya uchumi na ushirikiano wa utalii kati ya China na Vietnam.
Hivi sasa ushirikiano wa kiuchumi wa kanda ya ghuba ya kaskazini unaendelezwa moto moto kila siku ipitayo. Wachambuzi wanaona kuwa katika siku za baadaye ushirikiano wa kiuchumi wa kanda ya ghuba ya kaskazini utaongeza umuhimu wa njia ya uchukuzi wa baharini, kuimarisha ushirikiano wa usambazaji bidhaa wa bandari na usawazishaji wa sekta za uzalishaji bidhaa ili kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya China na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-05
|