Eneo la ustawishaji wa sayansi na teknolojia la Zhongguancun lililoko kaskazini magharibi mwa Beijing linasifiwa kuwa ni "Silicon Valley" ya China. Katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, watu waliodharamia kuendeleza shughuli za teknolojia za hali ya juu za China walikusanyika huko na kuanzisha shughuli zao, mwanzoni kazi zao zilikuwa ni kuunda sehemu mbalimbali za kielektroniki zilizoagizwa kutoka nchi za nje na kuziuza. Wakati huo hawakuwa na uwezo wa utafiti na uvumbuzi. Lakini hivi sasa eneo la Zhongguancun limekuwa eneo kubwa zaidi la ustawishaji wa sayansi na teknolojia nchini China, na asilimia zaidi ya 90 ya bidhaa zinazotengenezwa huko zimefikia kiwango cha kimataifa.
Mwandishi wetu wa habari aliwahi kuambiwa kuwa, ukiingia kwenye ofisi ya utafiti ya kampuni yoyote kwenye eneo hilo la Zhongguancun, hakika utashangaa kusikia miradi ya utafiti inayofanyika kwenye ofisi hizo, kwa kuwa miradi mingi hiyo inaenda sambamba na kiwango cha juu duniani.
Msemo huo ulithibitishwa mwandishi wetu wa habari alipokwenda kwenye kampuni ya teknolojia ya Hanwang. Kwa mujibu wa mhandisi wa kampuni hiyo Bw. Zhang Haopeng, hivi sasa kuna aina nyingi za simu za mkononi zenye uwezo wa kuandika maneno ya kichina, na asilimia zaidi ya 80 ya simu hizo zinatumia teknolojia ya kutambua maandishi ya kichina iliyovumbuliwa na kampuni hiyo. Bw. Zhang Haopeng alimwonesha teknolojia mpya iliyovumbuliwa nao. Alisema:
"tukipiga picha kadi ya utambulisho kwa kutumia kamera ya simu ya mikononi, basi baada ya sekunde kadhaa simu hiyo itaweza kutambua maneno ya kichina kwenye kadi hiyo na kuyahifadhi."
Teknolojia hiyo ilivumbuliwa mwaka jana na kampuni hiyo kwa kujitegemea. Hivi sasa makampuni mengi maarufu ya simu za mikononi yanataka kununua teknolojia hiyo.
Tangu kampuni hiyo ianzishwe kwenye eneo hilo miaka ya 90 ya karne iliyopita, ilikuwa inalenga uvumbuzi wa teknolojia. Lakini mwanzoni kampuni hiyo pia iliwahi kufanya makosa. Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Liu Yingjian alisema:
"tuliwahi kuanzisha miradi 43 kwa pamoja, lakini mwishoni tulilazimika kuiacha baadhi ya miradi. Kwa sababu baadhi ya miradi tulikuwa tunaipenda lakini wateja wetu walikuwa hawaipendi; nyingine ni kwa kuwa utafiti wake uligharimu fedha nyingi na wateja hawakuweza kumudu. Muhimu zaidi ni kuwa miradi mingi kama hiyo imevuka uwezo wa kampuni hiyo."
Uwekezaji usio na mpango si kama tu ulipunguza kiasi cha mafanikio ya utafiti kuwa asilimia 5 tu, bali pia ulifanya kampuni hiyo ikumbwe na hali mbaya ya kiuchumi. Baada ya kupita kwenye kipindi hicho kigumu, viongozi wa kampuni hiyo waliona kuwa makampuni yenye uwezo wa uvumbuzi yanahitaji zaidi mkakati wa kisayansi ya maendeleo. Hivyo kampuni hiyo ilipunguza miradi yake kutoka 43 hadi miradi 6 na kuweka mkazo katika miradi hiyo yenye mustakbali mzuri zaidi. Kwa hivyo, asimilia 50 ya miradi ya utafiti imefanikiwa.
Imefahamika kuwa katika miaka iliyopita, kampuni ya teknolojia ya Hanwang iliendelea kushikilia kutumia asilimia 10 ya pato la mauzo katika utafiti. Hivi sasa kampuni hiyo imepata maendeleo makubwa katika teknolojia za kutambua maandishi ya kichina, usimamizi wa kisasa wa mawasiliano na simu za kisasa za kompyuta, na kuwa na hakimiliki za teknolojia hizo. Hali ya jumla ya teknolojia za kampuni hiyo imefikia kiwango cha juu nchini China na kote duniani.
Kwenye eneo la Zhongguancun pia kuna makampuni mengine mengi yaliyopata mafanikio kwa njia ya uvumbuzi kwa kujitegemea kama ilivyofanya kampuni ya teknolojia ya Hanwang. Ofisa husika wa kamati ya usimamizi wa eneo hilo Bw. Ren Zaiqi alieleza kuwa, kwa kiwango cha wastani cha kimataifa, gharama ya utafiti wa teknolojia mpya inachukua asilimia 3 hadi 5 ya mapato ya jumla. Hivi sasa kati ya makampuni 17,000 yaliyokusanyika kwenye eneo la Zhongguancun, gharama ya utafiti kwa makampuni mengi ya huko imezidi kiasi hicho. Alisema fedha zilizotengwa na makampuni hayo kwa ajili ya utafiti wa teknolojia mpya zilifikia yuan bilioni 22 mwaka jana. Bw. Ren Zaiqi alisema:
"eneo la Zhongguancun linaongoza katika fani mbili kubwa, yaani usanifu wa molectron (IC), zikiwemo usanifu wa bidhaa za kielektroniki za matumizi ya binafsi kama simu za mikononi, MP3 na MP4; ya pili ni matibabu na dawa za viumbe, eneo la Zhongguancun pia lina msingi imara wa kiteknolojia."
Imefahamika kuwa kampuni ya bidhaa za viumbe ya Kexing ya Beijing hivi sasa imekuwa inaongoza katika sekta ya matibabu na dawa za viumbe kwenye eneo la Zhongguancun. Mwanzoni mwa karne iliyopita, China ilikuwa haijafanikiwa katika utafiti wa chanjo ya kutokomeza nguvu ya virusi vya hepatitis A. watoto wa China waliweza kutumia chanjo za nchi za nje tu. Hali hiyo iliamsha hamu kubwa ya mkuu wa kampuni hiyo Bw. Yin Weidong kutafiti chanjo hiyo. Alidharamia kuwapatia watoto wa China chanjo ya hepatitis A ya hali ya juu iliyotengenezwa na China.
Baada ya juhudi za miaka mingi, Bw. Yin Weidong na kundi lake walifanikiwa kutengeneza chanjo ya kwanza ya hepatitis A mwaka 1999. Ili kutengeneza chanjo hiyo kwa wingi, walitumia fedha nyingi katika kuweka mpango wa uzalishaji kwa wingi. Kampuni hiyo ilijenga kituo kimoja cha uzalishaji wa chanjo hiyo kwa kufuata kanuni za kimataifa, pamoja na taasisi moja ya utafiti wa chanjo. Taasisi hiyo ilitoa mchango muhimu katika utafiti wa chanjo ya SARS na homa ya mafua ya ndege kwa matumizi ya binadamu. Bw. Yin Weidong alisema:
"mradi wa utafiti wa chanjo ya hepatitis A uliinua kiwango cha utafiti wa kundi letu, na kukamilisha zaidi msingi wetu wa kiteknolojia. Pia tulitumia raslimali hiyo katika utafiti wa chanjo nyingine."
Kampuni ya Kexing ilifanikiwa kutengeneza chanjo ya kwanza ya SARS duniani katika muda mfupi, kazi ya utafiti wa chanjo ya homa ya mafua ya ndege kwa matumizi ya binadamu pia inaenda sambamba na kiwango cha kimataifa. Bw. Yin Weidong alisema, wakati kampuni hiyo inawekeza fedha nyingi kwa kukabiliwa na hatari kubwa, uwezo wa uvumbuzi na ushindani wa kampuni hiyo pia umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa kweli mbali na makampuni makubwa kama hayo, kufuata njia ya maendeleo kwa uvumbuzi wa kujitegemea pia ni mkakati wa pamoja wa makampuni madogo na ya wastani. Mkakati huo si kama tu umesukuma mbele maendeleo ya makampuni hayo, bali pia umefanya eneo la ustawishaji wa sayansi na tekenolojia la Zhongguancun listawi zaidi na kuwa na ushindani mkubwa zaidi duniani.
|