Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-07 16:40:46    
Sikukuu ya mwenge ya kabila la Wayi

cri

Mliosikia ni wimbo maarufu wa kabila la Wayi uitwao "Nyimbo za kienyeji zinazotoka mto wa Yuni". Kati ya makabila madogo mbalimbali ya China, kabila la Wayi linajulikana kwa kuwa na utamaduni maalumu na sikukuu za jadi. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alitembelea kijiji kimoja cha kabila la Wayi, na kushuhudia jinsi walivyosherehekea sikukuu ya mwenge ambayo ni sikukuu kubwa ya jadi ya kabila hilo kuliko nyingine.

Watu wa kabila la Wayi wanaishi katika mikoa ya kusini magharibi mwa China, ikiwemo Yunnan, Sichuan, Guizhou na Guangxi. Kizazi baada ya kizazi, Wayi wanajishughulisha na kilimo milimani na mabondeni. Watu wa kabila la Wayi wanaoishi katika mazingira yanayopendeza wana historia ndefu na utamaduni maalumu. Kabila la Wayi lina lugha na maandishi, muziki na ngoma za kabila hilo zinatofautiana na makabila mengine, na watu wa kabila hilo ni hodari katika ustadi mbalimbali za mikono, kama vile kutarizi, kuchonga na kuchora.

Mwandishi wetu wa habari alifika kijiji cha Malangzhi, mkoani Guizhou tarehe 24, Juni kwa kalenda ya Kichina. Siku hiyo ni sikukuu ya mwenge, ambayo ni sikukuu kumbwa kuliko nyingine ya kabila la Wayi. Aliona watu wenye furaha wakiwa hapa na pale. Wanaume wenye nguvu walikuwa wanashiriki kwenye shindano la mwereka, mashindano ya mbio za farasi na mchezo wa kupiganisha ng'ombe, huku wasichana waliovalia nguo za kikabila walikuwa wanaimba nyimbo za kienyeji na kucheza ngoma. Watoto walikuwa wanacheza miongoni mwa watu wazima, wakiburudishwa na siku hiyo ya furaha.

Msichana wa kabila la Wayi Dada Lan Aiju alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, moto ni ishara ya mwangaza inayothaminiwa na kabila hilo, kwa hiyo kati ya sikukuu mbalimbali za kabila la Wayi, sikukuu ya mwenge ni muhimu kuliko nyingine. Alisema "Kwetu sikukuu ya mwenge ni sikukuu muhimu kabisa ya jadi. Katika siku kadhaa kabla na baada ya sikukuu hiyo, watu wa kabila la Wayi wanakutana na kuandaa shughuli mbalimbali kuisherehekea sikukuu hiyo."

Kuna hadithi nyingi kuhusu sikukuu ya mwenge. Mzee Liu Yuanlong wa kabila la Wayi alielezea hadithi moja aliyosikia alipokuwa mtoto. Alisema "Zamani kulikuwa na mungu mmoja mkali mbinguni. Alipata amri ya mkuu wa mbingu kwenda ardhini kudai kodi nyingi sana kwa Wayi, kitendo hicho kilipingwa na Wayi, na kulitokea shujaa mmoja ambaye alimwua mungu huyo. Mkuu wa mbingu alikasirika sana na tukio hilo, alituma wadudu wabaya kula mazao ya mashambani. Wadudu walikuwa wengi kupita kiasi, walikuwa wanakula mazao ya mashambani kwa siku tatu mfululizo, kiasi kwamba mazao yanakaribia kwisha. Katika hali hiyo ya hatari, Wayi walitengeneza myenge, wakienda mashambani kuwachoma wadudu. Wadudu walikufa na mazao yakanusurika. Kwa ajili ili kuadhimisha tukio hilo, watu wanawasha mwenge kila mwaka inapofika siku hiyo, kwa lengo la kuondoa wadudu wabaya na kuomba mavuno makubwa."

Katika kijiji cha Malangzhi, kilele cha sikukuu ya mwenge kilifika, ambapo kila mmoja alikuwa anashika mwenge. Kwanza walipanga vizuri wakitembea kwa kuzunguka shamba mara moja, wakiomba mavuno makubwa. Kisha walijikusanya kwenye kiwanja, wakilimbikiza mienge hiyo kuwa moto mkubwa. Walizunguka fungu hilo la moto wakiimba na kupiga ngoma.

Mbali na nyimbo na ngoma za kupendeza, kabila la Wayi pia linajulikana kwa nguo zenye rangi mbalimbali, kwa hiyo sikukuu ya mwenge inaonekana kuwa ni maonesho ya nguo za kabila la Wayi. Ofisa wa huko anayeshughulikia mambo ya kikabila Bw. Shi Shude alieleza kuwa, awali kutokana na hali duni ya uzalishaji na maisha, kulikuwa hakuna shughuli mbalimbali katika sherehe ya sikukuu ya mwenge, na shughuli nyingi zinazofanywa hivi sasa ziliongezeka katika miaka ya hivi karibuni ambapo kiwango cha maisha cha Wayi kiliinuka.

Alisema,"Awali ilikuwa na sikukuu ya mwenge, lakini shughuli zilikuwa chache sana. Hivi sasa Wayi wamepata maendeleo, kwa hiyo sherehe ya sikukuu hiyo ya jadi ilikamilishwa hatua kwa hatua."

Hivi sasa sikukuu ya mwenge pia ni fursa kwa vijana kutafuta wapenzi wao. Licha ya kuwa sikukuu kubwa ya kuonesha michezo, utamaduni na mila za kabila la Wayi, sikukuu ya mwenge pia inawavutia wageni wengi.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-07