Kuanzia tarehe 15 hadi 28 Agosti mwaka huu, mkuu wa shirikisho la wafanyabiashara binafsi kati ya China na Afrika Bwana Hu Deping aliongoza ujumbe wenye watu 28 kufanya ukaguzi wa kibiashara katika nchi nne za Afrika mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania, Msumbiji na Madagascar. Kabla ya kuondoka Beijing, Bw. Hu Deping alikutana na mabalozi wa nchi hizo nne walioko nchini China. Alisema urafiki kati ya China na Afrika ni wa enzi na dahari, hivi sasa wakati uhusiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika unapoimarika siku hadi siku, ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande hizo mbili una mustakabali mzuri. Alitumai kuwa wanakampuni binafsi wa China wanapoelekea nje wanaweza kuzingatia kwanza maslahi ya upande mwingine, kuzidisha waelewano kati ya watu wa pande mbili kwa kujumuisha utamaduni wa China barani Afrika, kukuza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kwenye msingi wa kuelewana na kuafikiana, ili kuandika ukurasa mpya wa urafiki kati ya China na Afrika.
Wajumbe wa ukaguzi wa kibiashara wa China walipotembelea nchi hizo nne walikaribishwa kwa ukarimu na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hizo nne ambao ni pamoja na rais wa Madagascar, makamu wa rais wa Tanzania na waziri mkuu wa Msumbiji. Bwana Hu Deping alitoa hotuba kwenye Chuo Kikuu cha Msumbiji kuhusu hali ya maendeleo ya uchumi wa makampuni binafsi ya China. Wajumbe hao pia walifanya kongamano na baadhi ya wafanyabiashara wa China walioko katika nchi hizo nne. Pia walitembelea sehemu ya maendeleo ya teknolojia mpya ya juu ya nchi hizo, reli ya TAZARA, eneo la biashara ya China nchini Tanzania na kadhalika. Ujumbe huo pia ulizipa nchi hizo nne dawa za Cotexin za kutibu malaria.
Tanzania ni nchi ya Afrika inayofahamika zaidi kwa watu wa China, hali kadhalika watu wa Tanzania wana hisia nzuri kwa watu wa China. Ujumbe huo wa ukaguzi ulipowasili nchini Tanzania, ulilakiwa na waziri wa viwanda na biashara wa Tanzania kwenye uwanja wa ndege. Makamu wa rais wa Tanzania Bwana Ali Mohamed Sheni alikutana na wajumbe wote. Kwenye mkutano huo, Bwana Sheni licha ya kutoa shukrani kwa msaada mkubwa uliotolewa na serikali ya China kwa Tanzania, pia alisisitza kuwa ujumbe huo wa China umekwenda Tanzania katika wakati mwafaka sana. Kwa sababu hivi sasa Tanzania inatekeleza mpango wa maendeleo utakaokamilika mwaka 2025. Kutokana na mpango huo ifikapo mwaka 2010, ongezeko la uchumi la Tanzania litafikia asilimia 10 kwa mwaka, na utekelezaji wa mpango huo unahitaji uwekezaji mkubwa kutoka nje, hivyo makamu wa rais wa Tanzania alisema ujumbe wa ukaguzi wa kibiashara wa China umechagua fursa nzuri kutembelea Tanzania.
Sekta za nishati, ujenzi wa barabara, uchimbaji wa madini na kilimo za Tanzania zinahitaji sana uwekezaji kutoka nje. Wanakampuni wa ujumbe huo waliona kuwa hivi sasa hali ya ujenzi wa miji na barabara ya Tanzania inafanana na hali ile ya China kabla ya miaka 20 iliyopita. Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa nishati, hasa utoaji wa umeme. Makampuni mengi yanalazimika kufanya uzalishaji kwa siku nne tu kwa wiki. Kiwanda cha nguo cha urafiki kati ya China na Tanzania hata kilianzisha kituo chake chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kilowatt 1500 ili kuhakikisha uzalishaji wake.
Kilimo pia ni seka muhimu inayowavutia sana wanakampuni wa China. Tanzania inakabiliwa na upungufu wa mboga na nafaka. Kwa kawaida, upungufu wa nafaka nchini Tanzania ni tani laki sita, kama mwaka huu wenye ukame, upungufu huo wa nafaka unaweza kuwa zaidi ya tani milioni moja. Tena teknolojia ya kilimo ya China inafaa sana kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, hivyo sekta ya kilimo ina fursa nyingi kwa uwekezaji wa wafanyabiashara binafsi wa China.
Kampuni ya sayansi na teknolojia ya Lantian ya Shenzhen ina hakimiliki maalum, inaweza kutumia moshi na mabaki yaliyotumiwa katika kiwanda cha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe yawe rasilimali za kutengeneza PVC na saruji. Hakimiliki hiyo imetumiwa kwa mafanikio katika mikoa ya Guizhou na Sichuan nchini China. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bwana Han Zhijun alipoambiwa kuwa, Tanzania ina upungufu mkubwa wa umeme, alifikiri uwezekano wa kuanzisha kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe. Kama mradi huo unaweza kutekelezwa, uwekezaji wa mradi huo utakuwa mkubwa sana.
Reli ya TAZARA ina urefu wa kilomita 1860, kampuni ya biashara ya China na Tanzania ya Qingdao kwa miaka mingi inatengeneza vipuri kwa ajili ya reli hiyo. Mara hii meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Guan Hongzhong alianza kushiriki kwenye majadiliano na wanakampuni wengine maarufu wa China kuhusu mpango wa kuwashirikisha wanakampuni wengi binafsi wa China katika usimamizi wa reli ya TAZARA, ili kuifanya reli hiyo iwe na ufanisi mkubwa zaidi kiuchumi na kijamii.
Ili kueleza fikra zake mpya kuhusu maendeleo na uwekezaji, mkuu wa shirikisho la wafanyabiashara binafsi wa China, mkuu wa ujumbe wa ukaguzi Bwana Hu Deping aliitaka ofisi ya shirika la maendeleo na mipango ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kuitisha kongamano kati ya wajumbe wa China na waandishi wa habari wa Tanzania. Kwenye kongamano hilo, waandishi wengi wa habari wa Tanzania waliwakaribisha wafanyabiashara wa China kuwekeza nchini humo, lakini waandishi kadhaa wa habari walieleza wasiwasi wao kuwa, uwekezaji mwingi kutoka makampuni binafsi ya China nchini humo huenda utaleta shinikizo kubwa kwa makampuni ya Tanzania. Bwana Hu Deping alisema kuwa, mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita China ilipoanza kufungua mlango kwa nje, wanakampuni wengi wa China pia walikuwa na wasiwasi wa aina hiyo, lakini muda mfupi tu waligundua kuwa, uwekezaji kutoka nje si kama tu umeleta mitaji, teknoljia, usimamizi, kutatua tatizo la mahitaji kuzidi utoaji bidhaa na kuinua sifa ya bidhaa za China, bali pia umeleta kodi na nafasi za ajira, yaani umehimiza maendeleo makubwa nchini China. Na hiyo ndiyo sababu ya China kupata ongezeko kubwa la kiuchumi katika miaka 30 iliyopita. Mawazo ya Bw. Hu Deping si kama tu yamewafurahisha waandishi wa habari wa Tanzania, bali pia yamewatia moyo wanakampuni wa China na wafanyabiashara wa China walioko nchini humo.
Idhaa ya kiswahili 2006-09-08
|