Mtengeneza sanamu wa China Wu Weishan ingawa bado ni kijana, lakini sanamu 300 za wanautamaduni mashuhuri wa China ya kale alizotengeneza zinathaminiwa sana na kuhifadhiwa nchini China na katika nchi za nje, mtengeneza sanamu huyo ni msanii pekee wa Asia katika Shirikisho la Wachonga Samanu la Kifalme nchini Uingereza yaani the Royal Society of British Sculptors.
Hivi karibuni, Wu Weishan ambaye hivi sasa ni mkuu wa taasisi ya Chuo Kikuu cha Nanjing alifanya maonesho yake binafsi katika Jumba la Sanaa la China mjini Beijing, kwenye maonesho hayo sanamu alizotengeneza za wanautamaduni mashuhuri katika historia ya China zinaoneshwa, kati ya sanamu hizo kuna sanamu za wanafalsafa wakubwa wa China ya kale Confucius, Laozi, na pia kuna sanamu za watu mashuhuri wa zama hizi za mchekeshaji mkubwa wa ngonjera Ma Sanli na mwanasayansi mkubwa Yang Zhenning, sanamu hizo zinashabihiana moja kwa moja na watu hao wawili. Mfalme wa kwanza aliyeunganisha China nzima, Qin Shihuang, mwili wake ulifinyangwa kwa mlima na kilele cha "mlima" huo kilichongwa taji la kifalme likimaanisha mamlaka ya mwisho katika jamii ya kimwinyi nchini China. Ingawa sura ya sanamu ya Qin Shihuang haikutengenezwa, lakini watazamaji wanapoona sanamu hiyo mara wanatishika na madaraka yake makubwa. Sanamu ya mwanafalsafa mkubwa katika China ya kale, Lao Zi, ina urefu wa mita 16, joho lake kubwa lenye mikono mipana inawakumbusha watazamaji utamaduni mzito wa zama za kale, na sanamu ya mchekeshaji wa ngonjera, Ma Sanli, inawachekesha watazamaji kwa kuwa na mwili mwembamba, kichwa cha kuinuka, mkono wa kulia ukionesha vidole vitatu, anaonekana kama akiwasimulia watazamaji hadithi ya kuchekesha jukwaani.
Watazamaji wanapoangalia sanamu hizo wanakuwa kama wanasoma historia ndefu ya utamaduni mkubwa wa China. Mwananadharia mkubwa wa sanaa Prof. Yin Shuangxi alisema,
"Sanamu hizo zinaonekana kama zimelowa utamaduni wenye historia ndefu nchini China, kwani watu hao ni wawakilishi wakubwa wa utamaduni wa taifa la China."
Miaka kadhaa iliyopita, malkia wa Uholanzi Beatrix alipoangalia sanamu hizo alisema, "Ni wazi kwamba sanamu za watu hao zilizotengenezwa na Bw. Wu zinatokana na utamaduni wa China wenye historia ya miaka elfu tano." Lakini Bw. Wu aliwezaje kutengeneza sanamu hizo kwa kutumia utamaduni huo wa miaka elfu tano?
Bw. Wu Weishana ni kijana anayevaa shati la Kichina, mwenye nywele ndefu na anaonekana muungwana, alisema toka alipokuwa mtoto alipenda sana mashairi ya kale ya China na bila kujua alikuwa anajifunza utamaduni wa kale wa China.
Wu Weishana alizaliwa katika ukoo wa wasomi mkoani Jiangsu, mashariki mwa China, aliwahi kushiriki kwenye mtihani wa kujiunga na chuo kikuu kwa mara mbili, lakini alishindwa mara mbili, baadaye alijiunga na shule ya sanaa mjini Wuxi. Wuxi ni mji wenye watu wengi wanaotengeneza sanamu. Wu Weishan alifundishwa ufinyanzi wa sanamu katika shule hiyo na alifahamiana na wasanii wengi, kati yao, alikuweko mzee mmoja mwenye umri wa miaka themanini hivi, Wu Weishan alimheshimu sana kutokana na ujuzi wake mkubwa wa sanaa.
Wu Weishan akiwa katika mazingira hayo yenye watengeneza sanamu wengi, kidogo kidogo alishikwa na hamu ya kuifahamu sanaa hiyo. Baadaye alifanya kazi katika kiwanda kimoja, katika miaka alipokuwa akifanya kazi kiwandani hapo pia alishiriki mara kadhaa kwenye mtihani wa kujiunga na chuo kikuu, mwishowe alifanikiwa kujiunga na idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Ualimu mjini Nanjing, huko alipata msingi imara wa sanaa. Baada ya kuhitimu chuo kikuu alikuwa mwalimu katika chuo alichosomea, na katika miaka alipokuwa mwalimu alikwenda Ulaya kuendeleza zaidi elimu ya kutengeneza sanamu, baada ya kurudi nchini China alipata ufahamu mpya kuhusu utamaduni wa China. Alisema,
"Kutokana na kulinganisha mara kadhaa kati ya utamaduni wa China na wa Kimagharibi, nimepata ufahamu mpya kuhusu utamaduni wa China. Sanaa yangu inatokana na ufahamu huo kwamba asili yake ni mashairi, na moyo wa mashairi ya China ndio moyo wa watu wa China, China ni nchi ya mashairi, kwenye mashairi kuna busara za watu wa China na ufahamu wao kuhusu uzuri na hasa uwezo wao wa kufikiri, na hayo ndio mahitaji ya utungaji wa sanaa."
Katika miaka ya tisini ya karne iliyopita, Wu Weishan alianza kutengeneza sanamu za wanautamaduni mashuhuri wa China ya kale. Ili kuonesha vilivyo jinsi watu hao walivyokuwa alifanya utafiti wa saikolojia na alichapisha kitabu chake chenye maneno laki sita na elfu sita. Sanamu zake huzitengeneza kwa haraka kutokana na msukumo alionao moyoni. Watu wengi walisema, yeye ni "mtu mwenye kipawa". Lakini yeye mwenyewe alisema,
"Ninapotengeneza sanamu huwa nafanya haraka, kwani nafahamu moyoni jinsi sanamu itakavyokuwa, kipaji changu kinatokana na viturubisho vya ardhi yenye rutuba, na ardhi hiyo ni wasanii wa kienyeji na sanaa ya jadi ya China."
Sanamu zilizowahi kutengenezwa na Wu Weishan ziliwahi kuoneshwa katika nchi mbalimbali duniani, na sanamu ya "Mtoto Aliyelala" ilipata Tuzo ya Pangolin. Bw. Wu alisema, mafanikio yake yanatokana kutoka utamaduni wa jadi wa China na upendo mkubwa wa sanaa ya jadi. Alisema,
"Napenda sana utamaduni wa jadi wa China, ingawa sijawahi kuwaona wanautamaduni mashuhuri wa kale lakini kwenye ndoto yangu mara kwa mara nazungumza nao, mvuto wa watu hao umeimarisha nia yangu ya kuwaonesha watu hao waliokulia katika ardhi ya nchi yetu."
Bw. Wu Weishan alipotengeneza sanamu ya mwanasayansi mkubwa Yang Zhenning alijikumbusha ndoto yake alipokuwa mtoto, alipozungumza na mwanasayansi huyo nyumbani kwake alisema "nakuheshimu sana na mimi nilitaka kuwa mwanafizikia nilipokuwa mtoto", mke wa Yang Zhenning aliyekuwepo pembeni alisema, "Ni bahati hukuwa mwanafizikia, la sivyo tungekosa mtu mwenye kipawa cha sanaa."
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-11
|