Katika miaka ya karibuni bidhaa zilizotengenezwa nchini China zimekuwa zikiuzwa kwa wingi katika nchi za nje na kupendwa na watu wa huko. Katika shughuli za biashara katika muda mrefu uliopita, wanaviwanda wa kisasa nchini China wametambua kuwa bidhaa maarufu ni muhimu sana kwa uhai na maendeleo ya viwanda. Hivi sasa kuna bidhaa nyingi za jadi na za teknolojia ya kisasa zenye hataza ya China zinazopata sifa nzuri siku hadi siku. Katika kipindi hiki cha leo tutawafahamisha namna viwanda vya China vinavyojitahidi kutengeneza bidhaa bora zenye hataza ya China. Pamoja na kuongezeka kwa mfululizo kwa bidhaa zinazosafirishwa katika nchi za nje, watu wanaona ni aina chache tu ya bidhaa maarufu kati ya bidhaa za China zinazosafirishwa kwa nchi za nje, tena bidhaa hizo nyingi zinasafirishwa kwa nje kwa kubandikwa chapa maarufu za nchi za nje, na viwanda vya China havipati faida kubwa katika shughuli hizo. Ili kubadilisha hali hiyo, viwanda vya China ambavyo vimeimarika na kuwa na uzoefu wa uzalishaji, vinaanza kuzingatia kuwa na bidhaa zake maarufu. Tokea muda mrefu uliopita, nafasi ya soko la magari ya kiwango cha juu nchini China inachukuliwa na magari maarufu ya nchi za nje yakiwemo Audi, Benz na BMW, ambapo nafasi ya soko la magari ya kiwango cha kati inachukuliwa na magari ya kampuni za Volkswagen, Hyundai na Ford. Lakini katika miaka ya karibuni viwanda vya magari vya China vyenye haki-miliki ya uzalishaji kama vile vya Chery na Geely vilijichomoza. Sasa tunachukua mfano wa kampuni ya Chery, siyo tu kwamba magari yanayotengenezwa na Kampuni hiyo aina ya Chery yanasifiwa kwenye soko la magari ya kiwango cha kati nchini China, bali magari mengi yanasafirishwa kwenye masoko ya magari ya nchi za nje. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, magari aina ya Chery yaliyosafirishwa nchi za nje yalichukua 70% ya jumla ya magari madogo ya China yaliyosafirishwa kwa nchi za nje, na nchi na sehemu zaidi ya 40 ziliagiza magari ya Chery. Licha ya hayo injini za Chery zimeanza kusafirishwa kwenye masoko ya nchi za Amerika ya kaskazini kuanzia mwaka huu, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, zaidi ya injini 7,000 zilisafirishwa kwenda Marekani. Naibu meneja mkuu wa kampuni ya magari ya Chery Bw. Li Feng alisema, kushikilia kutengeneza magari yenye hataza ya China ni dhamana ya maendeleo kwa kampuni ya Chery. "Tulianza kutengeneza magari kwa kuanza na magari madogo na ya kubana matumizi ya mafuta, kisha tulianza kutengeneza magari ya kiwango cha juu, ambapo jina la kampuni pia limeanza kujulikana sana." Maendeleo ya kampuni ya Chery yanaleta mali kwa mji wa Wuhu, toka kampuni ya Chery ianzishwe miaka 9 iliyopita hadi hivi sasa, kumekuwa na viwanda zaidi ya 230 vya kutengeneza vipuri vya magari vilivyojengwa kwenye mji huo ulioko sehemu ya kati ya China. Kampuni ya Chery na viwanda vinavyotengeneza vipuri vinavyotumika katika magari ya Chery katika nusu ya kwanza ya mwaka huu vilikuwa na pato la Yuan bilioni 9.3, ikichukua karibu 40% ya pato la viwanda vya mji wa Wuhu. Bidhaa maarufu zinapotengenezwa katika sekta za jadi nchini China, pia zinaota mizizi katika sekta ya teknolojia ya kisasa. Kampuni ya teknolojia ya tarakimu ya Huaqi, Beijing ilianzishwa mwaka 1993, hivi sasa inaongoza katika sekta ya utengenezaji wa bidhaa za teknolojia ya tarakimu nchini China, bidhaa zake za display, memory stick na kamera za teknolojia ya tarakimu zinachukua nafasi kubwa kwenye soko la nchini China, pato la kampuni ya Huaqi kutokana na mauzo limeongezeka kwa zaidi ya 60% kwa mwaka katika miaka 10 iliyopita, na pato lake kutokana na mauzo mwaka jana lilikuwa Yuan karibu bilioni 2. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Huaqi Bw. Feng Jun alisema, bidhaa maarufu zenye hataza ya China licha ya kuwa chanzo cha utulivu na faida ya kudumu kwa kampuni, pia zinaonesha nguvu na sura ya nchi. "Tunafahamu kuwa bidhaa maarufu, hususan bidhaa maarufu za taifa zinaaminiwa na watu, zinaonesha moyo wa uvumbuzi na heshima ya kuinuka kwa taifa. Viwanda vyote vyenye uwezo wa kuwa viwanda maarufu duniani, vinapaswa kwanza kuwa viwanda maarufu vya nchini China, kujenga msingi madhubuti nchini, kutoa huduma bora kwanza, halafu viingie kwenye soko la kimataifa kwa hatua madhubuti. Ninaamini kuwa kutokana na juhudi za pamoja, bidhaa nyingi maarufu zitazalishwa nchini China" Katika uchumi wa soko huria wenye ushindani mkali, kufahamu umuhimu wa kuzalisha bidhaa maarufu hakutoshi, namna ya kuwafahamisha watu bidhaa zako bora na kufanya wanunuzi wachague bidhaa zako kati ya bidhaa mbalimbali za aina hiyo limekuwa ni suala linalovikabili viwanda vingi vya China. Baadhi ya viwanda vya China vinajaribu kutumia mbinu zilizotumiwa sana na viwanda vya kimataifa za kulinda na kuendeleza bidhaa zake. Kampuni ya Baidu ambayo ni ya kutafuta habari ni mfano mmoja halisi. Kampuni ya teknolojia ya tovuti ya Baidu ilianzishwa mwaka 2000, kazi zake za kipindi cha mwanzoni ilikuwa ni ya kutoa teknolojia ya utafutaji habari kwenye mtandao wa internet. Baada ya mwaka mmoja, mwanzilishi wa kampuni hiyo Bw. Li Yanhong aliamua kuanzisha tovuti maalumu ya utafutaji habari kwenye mtandao inayojulikana kwa jina la kampuni yao la Baidu. Mwaka 2005, hisa za kampuni ya Baidu zilianza kuuzwa kwenye soko la hisa la NASDAQ nchini Marekani, katika siku ya kwanza bei ya hisa ya kampuni ya Baidu ilipanda kwa 350%, na kampuni ya Baidu ilikusanya mitaji dola za kimarekani milioni 109, na kuweka rekodi ya kukusanya mitaji katika nchi za nje kwa kampuni ya Internet za China. Bw. Li Yanhong alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kuuza hisa sokoni ni njia ya kupata mitaji zaidi ya kuendesha shughuli za kampuni, pia ni nafasi nzuri ya kutangaza jina la kampuni. "Wawekezaji wanapokuamini, jina la kampuni yako linakuwa nembo maarufu. Hali ya kampuni yetu inafuatiliwa na watu wengi kwenye soko la hisa. Jambo hilo linasaidia sana kutangaza jina la Baidu. Tunatarajia kutumia muda mrefu katika siku za baadaye kuwafahamisha hatua kwa hatua wawekezaji, kuwa inawezakana kuanzisha nembo kubwa maarufu ya huduma nchini China." Ni kutokana na kufahamu umuhimu wa bidhaa maarufu kwa maendeleo ya viwanda, viwanda vingi zaidi na zaidi nchini China vinawekeza mitaji kwa mfululizo kujenga sifa za nembo maarufu kama kampuni za Chery, Huaqi na Baidu. Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai alisema, serikali ya China itajitahidi kusaidia viwanda kuboresha uzalishaji na uendeshaji shughuli za viwanda na kampuni kuzalisha bidhaa maarufu zenye hataza ya China, kubadilisha "kutengenezwa China" kuwa "kuvumbuliwa "Hivi sasa maneno ya 'imetengenezwa na China' yanajulikana sana katika sehemu mbalimbali duniani, lakini tunatakiwa kutimiza 'imevumbuliwa na China' kubadili maneno 'imetengenezwa China' kuwa 'imevumbuliwa na China', tunatakiwa kuzalisha bidhaa zetu bora maarufu.
Idhaa ya kiswahili 2006-09-12
|