Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-12 16:09:00    
Lengo la sera mpya za udhibiti wa matumizi ya ardhi

cri

Hivi karibuni baraza la serikali ya China lilitoa "Ilani kuhusu udhibiti wa matumizi ya ardhi". Je, lengo la sera mpya za udhibiti wa matumizi ya ardhi ni nini, na athari gani kwa uchumi wa taifa? Mwandishi wetu wa habari alikwenda kumwuliza maswali hayo mtaalamu husika.

"wimbi la kutumia ovyo ardhi litapungua baada ya ilani ya baraza la serikali kutolewa. Lakini tamaa ya watu kutumia ardhi kama wapendavyo haiwezi kudhibitiwa kimsingi, kabla ya kuboresha mfumo na utaratibu husika." Hayo yalisemwa na mjumbe wa halmashauri kuu ya baraza la mashauriano ya kisiasa ambaye pia ni naibu mkurugenzi wa kituo cha utafiti cha wizara ya ardhi Bw. Liu Wenjia.

Tangu kamati kuu ya chama cha kikomunisti cha China na baraza la serikali zitoe kwa pamoja "Ilani kuhusu uimarishaji wa matumizi ya ardhi ya mashamba", kudhibiti ipasavyo matumizi ya ardhi na kupiga marufuku matumizi ya ovyo ya ardhi ya mashamba ya kilimo, zilikuwa ni kazi muhimu katika shughuli za usimamizi wa ardhi nchini China. Lakini katika miaka 20 iliyopita, ingawa serikali kuu ilitoa amri na maagizo mara kwa mara, lakini wimbi la kutumia ovyo ardhi halikuweza kuzuiliwa ipasavyo, hata ilifikia hadi baadhi ya serikali za mitaa, ambazo zinabeba jukumu la usimamizi, zilitumia ovyo ardhi kinyume cha sheria.

Alipoeleza hayo Bw. Liu Wenjia alisema, "Chanzo cha kutumia ovyo ardhi kwa serikali za mitaa katika ngazi mbalimbali ni 'fedha'. Baadhi ya serikali za mitaa zinachukulia ardhi kuwa chombo muhimu cha kuleta fedha, baadhi yake zilitoa kibali kwa kukiuka madaraka, kukubali bila kusema maneno na kuunga mkono matumizi ya ovyo ya ardhi; au zilianzisha zenyewe masoko ya ardhi kwa ajili ya kujipatia fedha."

Kutokana na makadirio aliyofanya Bw. Liu Wenjia, faida ya biashara ya ardhi ya hivi sasa ni karibu 250%. Hiki ni chanzo muhimu kwa baadhi ya serikali za mitaa nchini China kupenda sana kuendesha biashara ya ardhi, na kutotekeleza majukumu yake ya usimamizi, na kuwa sababu muhimu ya kushindwa kuzuia matumizi ya ovyo ya ardhi.

Sera mpya zilizotolewa safari hii kuhusu matumizi ya ardhi, zimeagiza wazi jukumu la serikali za mitaa katika usimamizi wa ardhi na hifadhi ya mashamba ya kilimo, endapo makosa hayo yatarudia katika siku za baadaye, basi viongozi husika watachukuliwa hatua; Kwa upande mwingine, gharama za ardhi ya taifa inayotumiwa zitakatwa kutoka kwenye bajeti ya matumizi ya fedha ya serikali za mitaa ili kupunguza tamaa ya serikali serikali za mitaa ya kutumia ovyo ardhi.

Hata hivyo Bw. Liu Wenjia bado ana wasiwasi, alisema "faida zitakazopatikana kutokana na matumizi ya ardhi itakayochukuliwa, kwa mfano ardhi ya mashamba yaliyochukuliwa na ardhi yake kutumika kwa ujenzi, faida hiyo itakuwa ya nani, itagawanywa namna gani, hivi sasa bado hakuna sera husika zinazoagiza wazi, hivi sasa faida hiyo inachukuliwa bure na serikali za mitaa. Kama suala hilo halitatatuliwa vizuri, serikali za mitaa zitaendelea kuwa na faida kutokana na vitendo vya kutumia ovyo ardhi ya taifa, na tamaa yake ya kutumia ovyo ardhi ya taifa haitaweza kudhibitiwa kimsingi."

Aidha kutokana na uzoefu wa siku za nyuma, katika kipindi cha kupokezana kwa sera mpya na za zamani, itatokea hali ya kuidhinisha kwa wingi maombi ya matumizi ya ardhi, au kuchukua kwanza ardhi inayohitajiwa, jambo ambalo litapunguza ufanisi wa sera mpya za udhibiti. Mtaalamu husika alisema idara husika zinatakiwa kuwa macho kuhusu suala hilo, na zichukue hatua kwa haraka ili kuepusha hali ya namna hiyo kutokea.

Toka zamani serikali kuu inaona, tatizo kubwa lililoko katika shughuli za uchumi za hivi sasa ni ongezeko kubwa la uwekezaji kwa mali zisizohamishika. Endapo tatizo hilo halitatatuliwa vizuri, basi litaongeza hatari ya kutokea kwa mgogoro wa mambo ya fedha na kuathiri maendeleo ya uchumi wa taifa. Hivyo baadhi ya watu wanasema kutolewa kwa sera mpya za udhibiti wa matumizi ya ardhi ni hatua muhimu inayochukuliwa na serikali kuu ya kudhibiti uwekezaji wa mali zisizohamishika na kudumisha maendeleo mwafaka wa uchumi wa taifa.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-12