Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-15 15:58:54    
Maelezo kuhusu kusoma nchini China yafanyika nchini Kenya

cri

Kutokana na jinsi uhusiano kati ya China na Afrika unavyoendelea, mawasiliano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta mbalimbali hasa nyanja ya elimu yanaimarika siku hadi siku. Ifuatayo ni ripoti aliyotuletea mwandishi wetu wa habari kutoka Nairobi.

Tarehe 5 Septemba mwaka huu, ujumbe wa elimu wa China ulioundwa na wajumbe wa kamati ya usimamizi wa udhamini wa masomo ya China na vyuo vikuu 14 vya China ulifanya shughuli za kutoa "maelezo kuhusu kusoma nchini China" katika chuo kikuu cha Nairobi .

Kwenye shughuli hizo wajumbe kutoka chuo kikuu cha ualimu cha Tianjin, chuo kikuu cha mawasiliano cha Shanghai, chuo kikuu cha Zhejiang na vyuo vikuu vingine maarufu waliwaeleza wanafunzi wa Kenya kwa njia mbalimbali hali ya vyuo hivyo na sera husika za kuwapokea wanafunzi wa nchi za Afrika. Wanafunzi mia kadhaa wa vyuo vikuu vya Kenya walisongamana mbele ya meza za maonesho wakiomba wafahamishwe zaidi, na kuchukua karatasi za maelezo kuhusu vyuo vikuu mbalimbali na kuonesha hamu kubwa ya kujifunza nchini China. Mwanafunzi mmoja alisema:

"Nashukuru vyuo vikuu vya China kufanya shughuli hizo, nafurahi kweli, natumai kama inawezekana, shughuli kama hizi zifanyike mara mbili kwa mwaka nchini Kenya."

Kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara ya elimu ya China, mwaka 2005 kulikuwa na wanafunzi 2757 kutoka Afrika nchini China hili ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyotangulia. Kufanya shughuli za maonesho ya elimu ya juu ya China barani Afrika ni njia nzuri ya kuwafahamisha wanafunzi wa Afrika wanaotaka kusoma nchini China. Mkuu wa ujumbe huo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa kamati ya usimamizi wa udhamini wa masomo ya China Bwana Li Jianmin alisema, Kenya ni kituo cha pili cha safari ya ujumbe huo barani Afrika, kabla ya kufika Kenya walishiriki katika maonesho ya pili ya elimu na sayansi na teknolojia ya Tanzania yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Alisema:

"Ujumbe wa China ulikuwa ujumbe mkubwa kabisa kutoka nchi za nje uliohudhuria kwenye maonesho hayo. Tanzania ilitilia maanani sana maonesho hayo. Kwa mujibu wa hesabu isiyokamilika, wajumbe wa China waliwapokea wanafunzi mia sita au saba hivi wa Tanzania, kati yao asilimia 15 waliacha majina na anuani zao, wana hamu kubwa ya kusoma nchini China."

Bw. Li Jianmin alisema licha ya Kenya, China pia inafanya shughuli za kueleza vyuo vikuu vya China nchini Misri na Afrika kusini kila baada ya miaka miwili. Mwezi Novemba mwaka huu kamati ya usimamizi wa msaada wa masomo ya China itaunda ujumbe wa pili wa kufanya shughuli za "maelezo ya kusoma nchini China" nchini Misri na Afrika Kusini, ambao utashirikisha vyuo vikuu 50 vya China .

Mbali na kufanya maelezo ya kusoma nchini China, serikali ya China pia imeongeza idadi ya wanafunzi wa Afrika wanaopata udhamini wa masomo wa kusoma nchini China. Mjumbe kutoka kamati ya usimamizi ya msaada wa masomo ya China Bi. Li Bing alisema, mwaka huu idadi ya wanafunzi wa nchi za nje wanaopata udhamini wa kusoma nchini China imeongezeka hadi kufikia elfu kumi, na aina za misaada ya masomo kwa wanafunzi wa nchi za nje pia zimeongezeka, wala siyo aina moja tu ya msaada wa serikali, alisema:

"Mwaka jana serikali ya mji wa Beijing na Shanghai zilianzisha udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa nchi za nje. Hivi sasa vyuo vikuu mbalimbali vya China pia vinaweza kuomba udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa nchi za nje kutoka kwa serikali za huko."

Meza ya chuo kikuu cha Tianjin iliwavutia wanafunzi wengi zaidi. Naibu mkuu wa chuo cha elimu ya kimataifa cha chuo kikuu cha Tianjin Bwana Chen Jinhe alijibu maswali yote yaliyoulizwa na wanafunzi wa Kenya. Alisema licha ya kuwapatia wanafunzi wa nchi za nje udhamini wa masomo, serikali ya China pia inawapatia wanafunzi hao udhamini mwingine. Kwa mfano, kutokana na kuwa wanafunzi wa nchi za nje wanaosoma nchini China hukabiliwa na matatizo ya lugha na uwezo mdogo kwenye hisabati, fizikia na kemia, chuo kikuu cha Tianjin kimechukua hatua mwafaka kuwasaidia, alisema:

"Tokea mwaka jana, wizara ya elimu ya China ilianza kutekeleza utaratibu wa darasa la maandalizi, yaani kuwasaidia wanafunzi kujifunza lugha kwanza na kuinua kiwango chao cha hisabati, fizikia na kemia, chuo kikuu cha Tianjin, chuo kikuu cha ualimu cha Nanjing na chuo kikuu cha Shangdong ni vituo vya kwanza vya majaribio, na vimepata matokeo mazuri."

Siku chache zilizopita wanafunzi 29 wa Kenya ambao wamepata udhamini wa masomo kutoka serikali ya China waliwasili nchini China. Mmoja kati yao anayeitwa Bitange Hipa Tochi alipoulizwa kwa nini amechagua kuja kusoma nchini China, alisema:

"Ikilinganishwa na hali ya zamani, hivi sasa watu wa China na Kenya wamekaribiana zaidi, serikali ya Kenya imetunga sera ya kuelekea mashariki, badala ya kutupia macho magharibi tu kama hapo zamani, hii ni sababu ya kuchagua kusoma nchini China."

Idhaa ya kiswahili 2006-09-15