Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-19 15:53:37    
Mji wa Jingdezhen wafuata njia mpya ya maendeleo

cri

Katika lugha ya Kiingereza jina la nchi ya China ni sawasawa na jina la vyombo vya kauri, zamani nchi nyingine duniani ziliifahamu China kutokana na vyombo vya kauri, katika China, vyombo vya kauri vilivyozalishwa kwenye mji wa Jingdezhen vina sifa nzuri na kupendwa na watu wengi kuliko vyombo vya kauri vilivyozalishwa kwenye sehemu nyingine nchini China. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alitembelea mji huo mdogo wenye historia ya miaka zaidi ya 1,000 ya uzalishaji wa vyombo vya kauri. Katika kipindi hiki cha leo, tunawafahamisha namna mji wa Jingdezhen unavyofuata njia mpya ya maendeleo.  

Uliposikia kipande hiki cha muziki, huenda ulidhani ni muziki wa kawaida wa kichina, lakini pengine utashangaa baada ya kuambiwa kuwa muziki huo ulipigwa kwa vyombo vya kauri. Katika mji wa Jingdezhen niliona, utamaduni wa kauri umeingia katika mambo mbalimbali ya mji huo. Wakazi wa huko wanajivunia kuwa wakazi wa Jingdezhen, na uchumi wa mji huo wa kale pia unakuzwa kwa kuambatana na sifa za kauri za Jingdezhen.

Jingdezhen iko kaskazini mashariki mwa mkoa wa Jiangxi, ambao uko sehemu ya kati ya China, udongo wa huko unafaa sana kwa utengenezaji wa vyombo vya kauri. Licha ya hayo huko kuna milima mingi yenye miti ya misonobari, ambayo ina mafuta mengi, mbao za misonobari zikitumiwa kuchoma moto vyombo vya kauri, moto unaweza kufikia nyuzi 1,300, moto mkali huo unaweza kuzalisha vyombo vya kauri nyeupe vya hali ya juu, hususan kauri yenye michoro ya rangi nzito ya kibluu. Mazingira bora ya kipekee yalikuwa msingi madhubuti wa uzalishaji wa vyombo vya kauri vya huko. Kabla ya miaka zaidi ya 1,000 iliyopita, mfalme mmoja wa enzi ya Song nchini China aliona kauri laini ya hali ya juu na michoro ya rangi ya kupendeza, aliipenda sana na kuishika mkononi bila kuiacha, hivyo akaipa jina tarafa hiyo ndogo iliyotengeneza kauri za aina hiyo, kwa jina la enzi yake ya "Jingde", hii ndiyo chanzo cha jina la tarafa hiyo.

Tokea hapo jina la vyombo vya kauri vya tarafa ya Jingde lilivuma sana, siyo tu kwamba vyombo vya kauri hivyo vilikuwa vitu vya anasa vya mabwanyenye wa enzi mbalimbali, bali pia vilikuwa ni vitu vilivyopendwa sana na watu wa nchi za nje, ambavyo vilisafirishwa kwa nchi za nje kwa kupitia njia ya hariri kwenye bahari. Hadi hivi sasa vyombo vizuri vya aina mbalimbali vya Jingdezhen vinaoneshwa kwenye majumba makubwa ya makumbusho katika nchi mbalimbali duniani.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kama ilivyo kwa bidhaa nyingi za kawaida, sekta ya uzalishaji vyombo vya kauri ya Jingdezhen pia ilikabiliwa na changamoto kubwa, na kuonekana baadhi ya kasoro zikiwa ni pamoja na kutoongezeka kwa sifa za kauri, kuwepo kwa aina chache za vyombo vya kauri, kutowekwa katika paketi nzuri, na hususan kuwepo kwa bidhaa hafifu za magendo.

Mkurugenzi wa idara ya vyombo vya kauri ya mji wa Jingdezhen Bw. Huang Kangming alipoeleza hali hiyo alisema kwa masikitiko makubwa,

"Katika miaka ya karibuni tuliponzwa na vurugu ya utaratibu wa soko na bidhaa za magendo. Tokea mwaka 2001, maonesho mengi ya vyombo vya kauri visivyo rasmi vya Jingdezhen yalifanyika katika nchi za nje, ambayo hatimaye yalikuwa yanauza bidhaa zake zenyewe na wala siyo vyombo vya kauri vya Jingdezhen, lakini yalikuwa yanatumia jina la Jingdezhen tu, hata ilifikia hatua hadi kuuzwa kando za barabara, ambayo ni biashara ya mtindo wa kizamani na ya kiwango cha chini."

Alisema licha ya bidhaa za magendo zinazofanana na za Jingdezhen, kulikuwa na baadhi ya watu waliowadanganya wanunuzi wakijiita mabingwa wa vyombo vya kauri. Vitendo hivyo vilipaka matope jina la vyombo vya kauri vya Jingdezhen.

Kutokana na vitendo hivyo vya kuhujumu haki, mji wa Jingdezhen ukawa makini zaidi, katika miaka ya hivi karibuni kwa ushirikiano na idara ya usimamizi wa viwanda na biashara ya huko, mji wa uligundua mara nyingi vyombo vya kauri vya magendo. Mahakama za huko zimeanzisha "mahakama ya kulinda haki-miliki ya kiujuzi", katika miaka mitano iliyopita ilishughulikia kesi zaidi ya 200 za kuhujumu haki-miliki ya kiujuzi na kusawazisha utaratibu wa masoko.

Mbali na kuathiriwa na bidhaa za magendo, sekta ya uzalishaji wa vyombo vya kauri vya Jingdezhen inatatizwa na shida nyingine zikiwemo kutoshirikiana kwa viwanda vya uzalishaji wa vyombo vya kauri pamoja na kutojulikana sana kwa bidhaa hizo. Maendeleo ya sekta ya uzalishaji wa vyombo vya kauri vya Jingdezhen yalikwama kabisa katika miaka ya 90 ya karne iliyopita. Wakati ule viwanda vingi vya Jindezhen vilizalisha vyombo vya kauri, ambavyo vilibandikwa nembo za kampuni maarufu za nchi za nje. Nyongeza ya thamani ya bidhaa ilikuwa ndogo sana na faida ya viwanda pia ilikuwa ndogo mno. Ili kurekebisha hali ya namna hiyo, katika miaka michache iliyopita, viwanda vikubwa vitano vya mji wa Jingdezhen viliunganishwa na kuanzisha kampuni moja kubwa ya vyombo vya kauri, ambayo inazalisha vyombo vya kauri vya hali ya juu vinavyotumika katika maisha ya watu, na kuanza kufanya utafiti na usanifu kuzalisha vyombo vya kauri za rangi mbalimbali vyenye umaalumu wa kipekee. Tokea hapo mji wa kauri wenye historia ya miaka zaidi ya elfu 1, uliacha kazi ya kutengeneza vyombo vya kauri kwa ajili ya kampuni maarufu za nchi za nje, bali unajiendeleza kwa bidhaa zake bora.

Alipoeleza kuhusu kuanza kwa utengenezaji wa bidhaa bora maarufu, meya wa mji wa Jingdezhen Bw. Yu Guoqing alisema,

"Uzoefu unathibitisha kuwa, wazo la kuwa na bidhaa bora maarufu kunanufaisha kampuni kukuza uwezo wake wa ushindani kwenye masoko, vilevile kunasaidia kampuni kuboresha sura ya kampuni na kuinua ubora wa bidhaa, na zaidi ya hayo kunawahimiza wanunuzi kulinda maslahi yao kwa mujibu wa sheria."

Kuwa na bidhaa maarufu bado hakutoshi, tukitaka kupata mafanikio katika masoko yenye ushindani mkali, jambo lililo muhimu zaidi ni kuinua ubora wa bidhaa. Hapo zamani kitu kilichoongeza sifa za vyombo vya kauri vya Jingdezhen duniani ni ufundi wa uzalishaji wa vyombo vya kauri, hususan kuweka michoro ya rangi kwenye vyombo vya kauri vilivyokwisha chomwa moto. Ubora wa ufundi huo ni kufanya rangi kuwa mbichi na kupendeza zaidi, lakini kasoro yake ni kwamba vyombo vya vikichomwa moto tena, madini yaliyoko ndani yake na kwenye sehemu ya nje, yanaweza kuwa na madhara kwa afya ya binadamu. Ili kuzalisha bidhaa zinazolingana na vigezo vya hivi sasa duniani, kampuni ya vyombo vya kauri ya Jingdezhen imekuwa na ufundi mpya wa uzalishaji, ambao licha ya kudumisha rangi mbili za kupendeza, pia unafanya madini yaliyoko ndani ya vyombo vya kauri yasijitokeze nje wakati vyombo vya kauri vinapochomwa moto mara ya pili.

Meneja mkuu wa kampuni ya vyombo vya kauri ya Jingdezhen Bw. Wang Yao alipoeleza uvumbuzi huo alisema,

"Hivi sasa Umoja wa Ulaya umeweka kigezo kuhusu wingi wa madini ya risasi inayojitokeza nje kwa vyombo vya kauri vinavyoagizwa kutoka nchi za nje, ambacho ni milligram 0.2 katika lita 1 ya maji, lakini vyombo vya kauri tunavyozalisha vyenye nembo ya "Jani Jekundu", risasi iliyojitokeza kwenye maji ya lita 1 ni milligram 0.01 tu, kiasi hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na kigezo cha Umoja wa Ulaya.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-19