Katika siku kadhaa zilizopita, wanasayansi watano waliopewa tuzo ya Nobel ya sayansi ya uhai yaani Bw. Louis J. Ignarro na Bw. Ferid Murad kutoka Marekani, Bw. Robert Huber na Bw. Hartmut Michel kutoka Ujerumani na Bw. Aaron kutoka Israel walitembelea China. Katika mkutano wa baraza moja uliofanyika mjini Beijing, wanasayansi hao watano walibadilishana maoni na kujadiliana na wanasayansi wa China kuhusu sayansi ya uhai na afya ya binadamu.
Utafiti wa wanasayansi waliopewa tuzo ya Nobel ni wenye utaalamu wa kiwango cha juu, na si rahisi kwa watu wa kawaida kuelewa kazi zao. Hivyo wanasayansi hao watano walipokuwa mjini Beijing, walitoa mihadhara kuhusu kinga na matibabu ya magonjwa sugu ya binadamu ambayo watu wa kawaida waliyafahamu na kuelewa kwa urahisi zaidi. Dr. Louis J. Ignarro alitoa hotuba kuhusu kula chakula bora na mazoezi ya viungo kunaweza kukinga magonjwa ya mishipa ya damu moyoni. Mwaka 1998 Dr. Louis J. Ignarro na Dr. Ferid Murad walipewa tuzo ya Nobel ya matibabu kutokana na ugunduzi wa athari maalum ya kemikali ya nitrous oxide kwenye mfumo wa mishipa ya damu iliyoko moyoni. Hivi sasa, wanasayansi hao wawili wanazingatia namna ya kutumia ugunduzi huo katika kutibu magonjwa ya mishipa ya damu kwenye moyo ambayo yanasababisha vifo vingi kabisa duniani.
Kwenye mkutano wa baraza hilo, Bw. Ignarro alieleza kuwa, kemikali ya nitrous oxide ni kama mlinzi wa mwilini dhidi ya magonjwa ya mishipa ya damu ya kwenye moyo, upungufu wa nitrous oxide unaweza kusababisha magonjwa ya mishipa ya damu ya moyoni na ugonjwa wa kisukari, kuhakikisha kiwango mwafaka cha kemikali hiyo kunaweza kukinga na hata kutibu magonjwa hayo. Dr. Ignarro alisema:
"ukila mboga za majani na matunda mengi zaidi yenye kemikali za antioxidant, uwezekano wa kuharibika kwa kemikali ya nitrous oxide iliyoko mwilini utapungua. Aidha, samaki, chokoleti nyeusi, mvinyo na juisi za matunda mbalimbali vyote ni vyakula bora, na vyote vina kemikali nyingi za antioxidant."
Hotuba ya Dr. Ignarro ilimpa fununu mtafiti wa taasisi ya sayansi ya China Bw. Shi Xianglin. Alisema, ugunduzi wa athari maalum ya kemikali ya nitrous oxide kwa mfumo wa mishipa ya damu ya kwenye moyo umeweka msingi wa kinadharia kwa utafiti wa elimu ya lishe.
Utafiti wa Bw. Robert Huber na Bw. Hartmut Michel umejibu swali na kwa nini majani ya miti ni ya rangi ya kijani, na kufichua siri ya athari ya photosynthesis. Wanasayansi hao wawili walipewa tuzo ya Nobel ya kemia mwaka 1988 kutokana na ugunduzi wao wa miundo ya 3D ya protein kwenye athari ya photosynthesis. Walisema, ugunduzi huo una umuhimu katika maeneo ya utafiti wa dawa na hifadhi ya mimea. Kwa mfano, baadhi ya dawa za ugonjwa wa kisukari zinatengenezwa kwa kutegemea ugunduzi huo.
Baada ya kusikiliza hotuba za wanasayansi hao, wanasayansi wa China walisema, katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, ongezekzo kubwa la urefu wa muda wa maisha ya binadamu linahusiana barabara na michango muhimu ya wanasayansi hao waliopewa tuzo ya Nobel katika eneo la sayansi ya uhai, na utafiti wao ni wa kiwango cha juu kabisa duniani. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hivi sasa bado hakuna mwanasayansi yeyote wa China aliyekwishapata tuzo hiyo.
Kutokana na hali hiyo, katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imeongeza fedha katika utafiti wa sayansi ya uhai na teknolojia za viumbe, na maendeleo kadhaa yamepatikana. Mwanachama wa taasisi ya sayansi ya China Bw. Zhang Yaping alisema:
"katika miaka ya hivi karibuni, uwezo wa uvumbuzi wa China katika maeneo ya sayansi ya uhai na teknolojia za viumbe umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Kutokana na idadi ya hataza za teknolojia za viumbe, mwaka 2002 idadi ya hataza za kimatiafa za China ilichukua nafasi ya pili miongoni mwa nchi zinazoendelea."
Aidha, mawasiliano na ushirikiano kati ya wanasayansi wa China na wa nchi za nje pia yanaendelea kuimarishwa, hivi sasa China inaongoza mpango mmoja wa utafiti kuhusu protein ya ini ya binadamu. Mbali na hiyo, wanasayansi wa China wamefanikiwa kufichua mchakato wa mabadiliko ya virusi vya SARS, na kuweka msingi wa kisayansi kwa shughuli za kinga na tiba ya ugonjwa wa SARS duniani.
kinachofurahisha zaidi ni kuwa, China ilishiriki kwenye mpango wa kimataifa wa utafiti wa makundi ya jeni ya binadamu, na kumaliza kazi ya kuthabitisha orodha ya asilimia 1 ya jini ya binadamu. Hiyo ni alama kuwa utafiti wa jeni ya binadamu wa China unaenda sambamba na ule wa dunia. Mtafiti wa jeni ya binadamu wa China Bw. Yu Jun alisema, magonjwa mengi, yakiwemo tatizo la shinikizo kubwa la damu, ugonjwa wa kisukari na saratani ya matiti, yote yanahusiana na jeni. Kama kila mtu angeweza kuthibitishwa jeni zake, basi angeweza kujua hatari zake za kupatwa na ugonjwa fulani, hivyo atachukua tahadhari ili kuukinga na ugonjwa huo. Kuwawezesha watu wa kawaida wa China wathibitishe jeni zake ili kukinga na magonjwa ndilo ni lengo linalofuatwa na Bw. Yu Jun na wenzake. Bw. Yu Jun alisema:
"mwaka 1984 kuthibitisha utaratibu wa jeni ya mtu mmoja kulihitaji dola za kimarekani bilioni 30, mwaka 2004 kulihitaji dola za kimarekani milioni 30, mwaka 2006 ni dola za kimarekani bilioni 1.5, lengo letu ni kwamba kupunguza gharama yake hadi kufikia dola za kimarekani elfu moja katika miaka kadhaa ijayo."
Profesa E rnest Beutler wa Marekani aliyehudhuria mkutano huo alieleza, hivi sasa katika nchi za Marekani na za Ulaya tayari kuna maabara zinazotoa huduma za kuthibitisha utaratibu wa jeni kwa watu wa kawaida, na anaamini kuwa huduma kama hiyo itatolewa nchini China katika miaka 5 hadi 10 ijayo.
Dr. Robert Huber alisema, aliona na kusifu maendeleo yaliyopatikana China katika eneo la sayansi ya uhai katika miaka ya karibuni. Alisema:
Katika muda mrefu uliopita, China ilikuwa nyuma katika eneo la sayansi ya uhai na ilikuwa hainabudi kujifunza teknolojia kutoka kwa nchi za nje. Lakini hali hiyo sasa inabadilika, katika miaka mitano iliyopita, China imepata maendeleo makubwa katika eneo hilo. Hivi sasa watafiti wa China wameanza kufanya utafiti wa kiwango cha juu kabisa."
Wanasayansi wa China na wa nchi za nje pia wanakadiria kuwa, katika miaka 15 hadi 20 ijayo, China itakuwa moja ya nchi zinazoongoza katika tenolojia za viumbe duniani.
Baraza hilo linalohudhiriwa na wanasayansi wa China na nchi za nje limedhihirisha kuwa, watafiti duniani wanajitahidi kutafuta mbinu za matibabu ya magonjwa sugu, yakiwemo magonjwa ya mishipa ya damu moyoni, kisukari na SARS. Pamoja ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, binadamu watakuwa afya zaidi.
|