"Hujambo", "Natoka Zambia"?? Tarehe 21 asubuhi mwezi Agosti, maneno ya Kichina yenye lafudhi ya kigeni yalisikika katika ukumbi wa mkutano wa ubalozi wa China nchini Zambia. Wanafunzi zaidi ya 10 wa Zambia waliokuwa wanatakiwa kuja kusoma nchini China waliwafuata wafanyakazi wa ubalozi wa China kujifunza Kichina.
Maria Punabantu, msichana wa Zambia mwenye umri wa miaka 20, alimwambia mwandishi wa habari, "Nataka kwenda China kusomea udaktari. Unajua nchini Zambia kuna maradhi mengi, kama vile ukimwi na malaria, lakini nchi yetu ina upungufu wa madaktari, hivyo baada ya kuhitimu nitarudi nchini kuanzisha zahanati ili kuwatibu watu."
Maria ni mmoja kati ya wanafunzi 25 wa Zambia waliokuja kusoma nchini China mwaka huu, ambao watadhaminiwa na serikali ya China, alijifunza udaktari katika chuo kikuu cha Zambia kwa miaka miwili, na amefaulu mtihani wa kuingia kwenye kitivo cha udaktari cha chuo kikuu cha Dongnan cha China. Kwa kuwa amekuja China kwa mara ya kwanza, hivyo anapaswa kujifunza Kichina kwa mwaka mmoja, baadaye ataanza kozi yake. Maria alisema, anapenda sana matibabu ya kichina kwa kuwa Zambia ni nchi maskini, watu wengi hawana pesa za kwenda hospitali na kununua dawa, lakini matibabu ya kichina yanahusu dawa nyingi za mitishamba, hivyo baada ya kuhimitu masomo nchini China na kurudi nchini Zambia, ataweza kuwafundisha watu wa nchi yake kutumia dawa za mitishamba ili kutibu magonjwa, kama vile kutumia maji ya tangawizi yaliyochemshwa kutibu mafua.
Maria alisema bila kujali atakabiliwa na matatizo gani, atakabiliana nayo kwa ushujaa, kwani kwenda kusomea udaktari nchini China ni ndoto yake ya siku zote, na udhamini wa masomo unaotolewa na serikali ya China utamsaidia kutimiza "ndoto ya China".
Ikilinganishwa na Maria, Kibaki Banda anayesoma nchini China kwa miaka mitano anaonekana kuwa amepevuka zaidi na kujiamini. Banda alimwambia mwandishi wa habari kuwa, kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2003, aliwahi kusomea kozi ya uhandisi wa umeme katika chuo kikuu cha mawasiliano cha Xi'an cha China, na safari hii atasoma shahada ya pili nchini China kuhusu mambo ya Kompyuta katika chuo kikuu kilichoko mjini Guangzhou, China. "Nitarudi nchini Zambia kwa kuwa nataka kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi yetu."
Banda aliporudi nchini Zambia baada ya masomo ya mwaka 2003 alifanya kazi katika kampuni ya Zhongxing ya China iliyoko nchini Zambia kwa mwaka mmoja, baadaye alifanya kazi katika kampuni ya mawasiliano ya simu ya Zambia. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kutokana na kusoma nchini China, alipewa kipaumbele alipotafuta kazi katika kampuni ya Zhongxing, na alijifunza mambo mengi kuhusu mawasiliano ya simu wakati alipofanya kazi katika kampuni hiyo, ambayo ilimsaidia sana alipofanya kazi katika kampuni ya mawasiliano ya simu ya Zambia. Alikuwa mhandisi mwandamizi mara tu alipoanza kufanya kazi katika kampuni ya mawasiliano ya simu ya Zambia. Hii inatokana na uzoefu wake katika kampuni ya Zhongxing.
Kama ilivyo kwa Banda, Linda Miyoba pia amekuja nchini China kusoma kwa mara ya pili, ambapo atasomea shahada ya pili ya Kompyuta. Linda alisema alipokuwa nchini China kwa mara ya kwanza, alikuwa hajui lugha ya Kichina hata kidogo, na alipaswa kushughulikia mambo yote mwenyewe, hivyo mwanzoni aliona ni vigumu, lakini wenzake na walimu wake wa China walimtendea kwa urafiki, alipokabiliwa na matatizo yoyote walimsaidia, hivyo alizoea maisha ya China kwa haraka.
Hivi sasa Linda ameacha kazi yake na kuendelea kusoma nchini China, kwa kuwa anatumai kujifunza elimu kuhusu usalama wa tovuti, ili aweze kufanya kazi katika benki baada ya kurudi nchini. Miaka nenda miaka rudi, ubalozi wa China nchini Zambia uliwaaga wanafunzi wengi waliokuja kusoma nchini China. Konsela wa ubalozi wa China nchini Zambia Bw. Zhao Zhanbin alijulisha kuwa, serikali ya China ilitoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa Zambia kuanzia miaka ya 60 ya karne iliyopita, muda mfupi baada ya Zambia kupata uhuru, sasa idadi ya wanafunzi wanaosaidiwa na serikali ya China imeongezeka hadi 25 kutoka 10 kila mwaka. Alisema mpaka sasa, wanafunzi wa Zambia waliokuja kusoma nchini China wamefikia 555, miongoni mwao zaidi ya 500 wamehitimu na kurudi nchini Zambia, na kufanya kazi katika sekta mbalimbali za Zambia, wakati wanapotoa mchango kwa nchi yao pia wamekuwa kama mabalozi wa urafiki kati ya Zambia na China.
Mkuu wa kamati ya udhamini wa masomo ya Zambia anayeshughulikia kuchagua wanafunzi wanaosoma nje ya nchi Bw. Siluyeli alimwambia mwandishi wa habari kuwa, udhamini wa masomo unaotolewa na China unakaribishwa sana nchini Zambia, na kila mwaka idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha ikupata udhamini huo ni kubwa. Alisema anatumai kuwa serikali ya China itatoa nafasi nyingi zaidi kwa Zambia kila mwaka, ili kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kutimiza ndoto zao.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-22
|