Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-09-25 15:41:36    
Maduka maarufu mjini Beijing

cri

Mji wa Beijing ni mji mkuu wa China wenye historia ndefu, mbali na vivutio kadha wa kadha vya utalii, pia kuna maduka mengi maarufu yaliyoanzishwa tangu zamani sana, ambayo yameonesha historia na hadithi za kuvutia kuhusu Mji wa Beijing.

Duka la dawa la Tong Ren Tang ni lenye historia ndefu zaidi miongoni mwa maduka maarufu mjini Beijing. Duka hilo la dawa lililoanzishwa mwaka 1669 hata limekuwa alama ya maduka maarufu ya Beijing.

Mwanzilishi wa Duka la dawa la Tong Ren Tang anaitwa Le Xianyang, ambaye alikuwa ofisa mwandamizi wa matibabu aliyemhudumia mfalme. Kutokana na uhusiano wake wa karibu na jamaa wa wafalme, tena alikuwa na uwezo mzuri wa kuchagua na kutengeneza dawa za mitishamba, Duka la dawa la Tong Ren Tang aliloanzisha Le Xianyang lilichukuliwa kuwa duka la kufanya biashara ya dawa za mitishamba la kumhudumia mfalme na jamaa zake tu. Mfanyakazi mzee Bwana Jin Yongnian aliyefanya kazi kwa miaka mingi katika duka hilo alisema, hata vyeti vingi vya dawa vilivyoandikwa na Duka la dawa la Tong Ren Tang vilipatikana kutoka kwenye kasri la kifalme. Bwana Jin alisema:

Kwa mfano pombe ya Guogong iliyotengenezwa na Tong Ren Tang ilitokana na cheti cha dawa alichopata ofisa Guogong wa Enzi ya Ming ya karne ya 14 baada ya kutafutatafuta miongoni mwa raia, zamani ofisa huyo alitengeneza pombe hiyo ya dawa nyumbani kwake. Pombe hiyo ya dawa kweli inasaidia kupitisha damu bila matatizo kwenye mishipa na bila kuona maumivu mwilini. Baadaye cheti hicho kilitumiwa katika hospitali ya kifalme. Na Duka la dawa la Tong Ren Tang lililowahudumia mfalme na jamaa zake lilirekebisha mara kwa mara cheti hicho cha dawa, na kuifanya pombe hiyo ya dawa ipate ufanisi mzuri wa matibabu. Hata malkia Cixi wa mwishoni mwa Enzi ya Qing alitumia pombe hiyo ya dawa, mpaka sasa pombe hiyo ya dawa bado ni pombe ya dawa maarufu inayotengenezwa na Duka letu Tong Ren Tang.

Bwana Jin alisema Duka la dawa la Tong Ren Tang linafuata kwa makini kanuni moja ya kutengeneza dawa yaani, ingawa mchakato wa kutengeneza dawa hauwezi kufahamishwa kwa watu, lakini watengenezaji wa dawa wanapaswa kufuata maadili ya kazi bila uzembe hata kidogo. Bwana Jin alisema katika zaidi ya miaka 300 iliyopita, Duka la dawa la Tong Ren Tang siku zote linafuata kanuni hiyo kwa makini sana katika kutengeneza kila dawa. Alisema:

Kwa mfano dawa ya Zixue ambayo ni dawa moja maarufu ya kutibu homa ya watoto, katika cheti cha dawa cha zama za kale, watengenezaji walitakiwa kutumia sufuria ya dhahabu na mwiko wa fedha. Kwa kawaida watengenezaji wa maduka mengine hawawezi kufuata matakwa haya, lakini Duka la dawa la Tong Ren Tang linaona kuwa, kanuni hiyo iliyowekwa kwenye cheti cha dawa cha zama za kale, hakika ina umuhimu wake na kuonesha kuwa dhahabu na fedha zinaweza kuonesha umuhimu wake katika mchakato wa utengenezaji wa dawa, hivyo ingawa Duka la dawa la Tong Ren Tang halina sufuria kubwa ya dhahabu, lakini lilikusanya vidani vya dhahabu kilo 5, kila likitengeneza dawa ya Zixue vidani hivyo vya dhahabu huchemshwa pamoja na dawa nyingine za mitishamba kwenye sufuria, kazi hiyo iliendelea vivyo hivyo katika miaka mia kadhaa iliyopita.

Hivi sasa Duka la dawa la Tong Ren Tang siyo duka la kuuza dawa tu, bali limekuwa mwakilishi wa utamaduni wa matibabu ya jadi ya kichina na dawa za mitishamba za kichina. Siku chache zilizopita, vyeti vya dawa Tong Ren Tang na ufundi wake wa kutengeneza dawa umeorodheshwa kuwa mali ya urithi wa utamaduni usioonekana nchini China. Dawa za mitishamba za aina mbalimbali zilizotengenezwa na Duka la dawa la Tong Ren Tang zinaweza kutibu magonjwa mbalimbali ama kuleta misaada ya kwa afya za watu. Ndani ya duka hilo, pia kuna waganga wazee wa matibabu ya kichina wanaokaa kwenye viti ambao wanaweza kugusa mishipa ya watu halafu kutoa ushauri kuhusu afya za watu.

Duka lingine maarufu lililojengwa zamani sana mjini Beijing ni Duka la chai la Zhang Yi Yuan lenye historia ya zaidi ya miaka 100. Chai maarufu zaidi ya duka hilo ni chai ya jasmini, ofisa wa duka hilo Bwana Liu Jiabo alisema:

Tunachagua kwa makini majani ya chai na maua ya jasmini, majani ya chai hiyo lazima ni yale yaliyostawi katika siku za mchipuko, na maua ya jasmini yanatakiwa ni yale ya siku za joto, tena ni yale yaliyotunga kabla ya kuchanua, kwani maua hayo ya jasmini yana harufu nzuri zaidi, yakichanganywa pamoja na majani ya chai yatawawezesha watu wajisikie hali ya starehe wakati wa kunywa chai.

Mbali na chai ya jasmini, wateja pia wanaweza kununua chai nyingine maarufu za China na vyombo vya chai vinavyopendeza, ama wanaweza kupumzika kwa muda kwenye duka hilo kunywa chai ya jasmini, ambapo watasimuliwa hadithi kuhusu chai na wahudumu, ama wanaweza kutazama maonesho ya ustadi wa jadi wa China wa kunywa chai.

Na Duka la Rui Fu Xiang la kuuza vitambaa vya hariri pia ni duka moja lenye historia ndefu. Duka hilo lilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 na mfanyabiashara Meng. Jengo la duka hilo ni lenye mtindo maalum wa Ulaya lakini mapambo yake ni michongo ya jadi ya mawe meupe ya marmar ya China, jengo hilo linahifadhiwa mjini Beijing likiwa ni moja kati ya mabaki ya utamaduni. Inasemekana kuwa mwaka 1900, wakati mtaa wa biashara wa Da Shanlan mjini Beijing ulipoungua, maduka mengi yaliteketezwa, lakini jengo imara la Duka la Rui Fu Xiang halikuathirika hata kidogo.

Duka la Rui Fu Xiang la kuuza vitambaa vya hariri linawavutia sana wateja wengi, hata wake wa marais wa nchi mbalimbali walipotembelea nchini China pia walikwenda kwenye duka hilo kununua vitambaa vya hariri. Bibi Madeleine Albright aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani alipofanya ziara nchini China, kwa mahsusi alikwenda kwenye duka hilo kununua vitambaa vya hariri vyenye thamani ya Yuan elfu kadhaa. Bibi Setsuko Chambers kutoka Marekani alisema, alipokuwa Marekani aliambiwa habari kuhusu duka hilo, alisema:

Nilisoma kitabu na kupata habari kuhusu duka la Rui Fu Xiang, habari ilisema vitambaa vilivyouzwa kwenye duka hilo vina mtindo maalum, hivyo nimekuja kwenye duka hili kununua vitambaa vya hariri, vitambaa hivyo ni vitu maalum sana kwa watu wa Marekani, nafurahia kweli.

Idhaa ya kiswahili 2006-09-25