Jana (tarehe 24) ni siku ya viziwi duniani. Tangu siku ya kwanza ya viziwi duniani ithibitishwe na Shirikisho la Viziwi Duniani mnamo mwaka 1958, miaka 48 imeshapita. Baada ya hapo jumapili ya 4 ya mwezi Septemba ya kila mwaka imekuwa siku maalum kwa viziwi kote duniani.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya viziwi duniani ni "Tumia lugha ya ishara, Ondoa shida katika mawasiliano" Kabla siku hiyo maalum haijafika, mwandishi wetu alienda kisiwani Zanzibar na kumhoji mkalimani mmoja maalum, ambaye anatumia lugha ya ishara kuwasaidia viziwi kuwasiliana na watu wengine.
Q: Hujambo?
A: sijambo.
Q: waeleze wasikilizaji jina lako kamili
A: Mimi kwa jina naitwa Heri Muhamed Simai, ni mzaliwa wa Zanzibar katika kijiji kimoja kiitwacho Makunduchi.
Q: nimeona leo kuna shughuli mbalimbali katika sherehe hiyo, unashghulikia mambo ya kutafsiri lugha kwa kutumia ishara, kwanza naomba utuelezee hiyo lugha ambayo umekuwa ukiitumia inaitwaje?
A: Hii lugha inaitwa lugha ya ishara, ni lugha maalum kwa watu ambao wanaitwa viziwi. Kwa kweli watu wengine huwaita mabubu, lakini wenyewe hawataki kuitwa mabubu ni kosa kubwa sana, wanataka waitwe viziwi. Na kuna walemavu wengine ambao hawawezi kuona hawataki waitwe vipofu, wanatakwa waitwe wasiona, kuwaita vipofu ni kosa kubwa sana.
Q: Ni nini kilichokufanya uamue kuwasaidia viziwi?
A: Kwa kweli nilianza toka shule za msingi, tumeona matokeo yao hayaridhishi kutokana na walimu wanapofundisha wanatoa sauti, watu wasiosikia wanakuwa hawajui anachofundisha, na wakifanya mitihani utaona wanakosea sana na matokeo ya mtihani hayaridhishi. Naona kitu hiki si kizuri, na si haki katika haki za binadamu, nawashawishi na kushirikiana nao kwa hali na mali. Hasa katika mambo ya dini, nataka tuingie katika mambo ya dini kuwasaidia.
Q: wakalimani kama wewe wanawasaidia viziwi kwa lugha ya ishara, mnawasaidia katika makongamano au sherehe gani?
A: Tunawasaidia katika sehemu mbalimbali mfano kama misikitini, kila Ijumaa kuna hotuba. Isitoshe kuna semina, kwa sababu huwa wanaenda kwenye chama chao, chama cha viziwi Zanzibar, vilevile kuna semina ya umoja wa Zanzibar tunaenda kuwasaidia huko.
Q: Watu hawa wasiosikia wanauchukuliaje msaada wenu?
A: Kwa kweli wameupokea vizuri sana tunafurahi sana, wameshukuru sana na kupenda kukaa pamoja nasi kila wakati.
Q: Mtu akitaka kuwasaidia viziwi kwa lugha ya ishara, anakwenda kusomea wapi?
A: unaweza kupata masomo katika sehemu nyingi. Hata unaweza kufika kwenye nchi jirani zetu unaweza kujifunza lugha ya ishara, kwa kweli ukifika kwenye sehemu nzuri tu unaweza kupata mafunzo.
Q: Wewe uliifahamu vipi lugha hiyo ya ishara?
A: Nimeifahamu lugha hii kutokana na kufundishwa na mlemavu mmoja aliyetoka Tanzania bara, alikuja kutufundisha na tumepata mafunzo na sehemu ambapo tunawasaidia watu huku vizuri zaidi.
Q: Jamii kwa ujumla inawapokeaje, au inauonaje mchango wenu wa kuwasaidia viziwi kwa lugha ya ishara?
A: jamii inafurahi sana na kushukuru sana. Kwa sababu kwa viziwi, vyombo vya habari hasa televisheni na radio, vimekuwa haviwasaidii kwa hali ya juu, jamii inaitaka serikali iweke sehemu ya mkalimani katika taarifa ya habari ya televisheni, ili viziwi waweze kuelewa kitu kinachozungumzwa, kwa sababu hivi sasa viziwi wanapata habari kutoka kwenye magazeti tu, hawapati habari kutoka kwenye vyombo vya habari vya aina nyingine.
Q: Leo katika sherehe hiyo umesimama mchana kutwa huchoki au mnapokezana vipi katika shughuli zenu?
A: kama wakiwepo watu wawili tunaweza kuendelea na kazi bila kuchoka, tunaweza kukaa masaa yote, kwa sababu mmoja anafanya kazi akichoka anatoa ishara kwa ishara kwa mwenzake, na kumwambia sasa njoo unisaidie. Na mwenzake anakuja kuchukua nafasi yake, na wa kwanza anaweza kupumzika, hivyo ndivyo tunavyopokezana.
Q: Kwa kufanya kazi hiyo kama mkalimani wa lugha ya ishara, binafsi yako unapata faida gani?
A: nimepata faida kubwa kutokana na kazi hiyo. Katika mambo yangu mengi lugha ya ishara inanisaidia. Kwa mfano naweza kununua vitabu kutokana na kazi hiyo, katika semina inayofanyika kwa siku 5 katika siku hizi, naweza kupata kitu ambacho kinaweza kukanisaidia katika kujielimisha, kwa mfano kulipiwa ada ya shule.
Q: Lugha ya ishara ina umuhimu gani kwa jamii?
A: baadhi ya watu wanadharau kitu hiki, na kuwadharau viziwi na kutuchukulia sisi wakalimani kama watu tusio na kazi yoyote. Lakini kuna wengine tunawashukuru wanapokea vizuri na kufahamu vizuri hii lugha na kuona kuwa hao viziwi ni sawasawa na watu wengine, na wengine wana hamu kubwa ya kuingia kujifunza lugha ishara.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-27
|