Wiki hii naibu waziri wa habari na mawasiliano wa Kenya Bwana Koigi Wamwere anafanya ziara hapa Beijing, ambapo alikuja Radio China Kimataifa kwa matembezi, zifuatazo ni mahojiano kati ya Radio China Kimataifa na Bw. Wamwere.
CRI: Mheshimiwa kwanza ningekukaribisha kwenye studio zetu hapa Radio China Kimataifa. Je picha yako uliyoipata kuhusu China ni vipi?
Waziri: Tumepata matayarisho ya hali ya juu, umekutana na ukarimu mwingi, na kusema kweli imekuwa ni picha tofauti sana na picha ambayo tulihubiliwa wakati wa vita vya baridi ya kwamba, wachina ni watu tofauti sana na watu wengine duniani. Nimefurahiwa sana kuona maendeleo ya hali ya juu ambayo sikudhani kukutana nayo hapa China. Na zaidi nimefurahia sana kuja hapa kwenye studio zenu, kwa kweli nimeshangaa kidogo kuona namna mlivyoendelea: jumba kubwa, wafanyakazi wengi na utaalamu kubwa wa Lugha, sikutarajia kukutana nayo nchini China.
CRI: Mheshimiwa tuzungumzie kidogo kuhusu jinsi matangazo ya lugha ya Kiswahili ya CRI yanavyopokelewa nchini Kenya?
Waziri: Nadhani yanapokelewa vizuri hasa kwa sababu ya ufasaha wenu wa lugha. Unajua ufasaha ni jambo muhimu, kwa sababu inaweka utamu katika lugha ambayo inawavutia wasikilizaji, na katika hilo mmefaulu sana. Wakenya na wakazi wa eneo la Afrika mashariki kwa jumla wana hamu kubwa ya kujua hali ilivyo katika mataifa mengine. Matangazo yenu yamewapasha watu ujuzi mpya wa hali ilivyo katika mataifa ya nje. Na ufasaha wenu wa lugha ya Kiswahili umewapa wakenya imani kubwa kwamba, kama wachina au vituo vya nje vinaweza vikaielewa lugha hivi na vikaitumia kwa namna nzuri kiasi kile, na sisi tunapata imani ya kuwa hatuna sababu ya kujivunia ya kuweza kutumia lugha yetu namna inavyotakikana kutumiwa. Kwa hivyo siyo tu tunafurahia kusikia, bali pia tumepata funzo kubwa.
CRI: Wachina wamekuwa labda ni waathirika wa propaganda ya vyombo vya habari vya magharibi kwa sababu sasa hivi watu wengi wa nchi za magharibi ukiwaambia kuhusu nchi za Afrika wanajua tu ni vita, magonjwa, njaa kama unavyosema kuhusu China wakati wa vita vya baridi. Serikali ya Kenya itachukua hatua gani kuondoa kasumba ya vyombo vya habari vya magharibi kutoa picha mbaya ya nchi kama ya China na nchi zetu za Afrika.
Waziri: Nadhani namna ya pakee ya kupambana na tatizo hili ni kupatia kwa mfano wachina nafasi ya kujieleza kwa watu wetu, wawe na kituo chao cha radio pale, wawe na program zao za luninga pale, ili wajieleze wenyewe kwa watu wa Kenya, kwa sababu ikitegemewa mwingine akueleze kwa jamii aidha yake au kwa dunia, uwezekano wa kupotosha ni mkubwa sana, lakini wachina hawawezi wakajieleza kimakosa kwa watu wa dunia hii. Wakipewa nafasi hii watasema mema yao .
Watu wa magharibi wakiongea mambo ya watu sio wazungu mara nyingi wametupa taswira ambayo si yetu. Wametuonesha tofauti na vile tulivyo, wametuweka nyuma, wamejaribu kutuonesha sisi ni watu ambao hatukustaarabika, watu ambao hatuwezi kuyamudu maendeleo, tuko chini kifikra. Lakini sasa wachina na warusi ambao walijazwa na propaganda bovu kuwahusu, namna ya wao kupata sifa wanaostahili ni wao kuweza kujieleza katika vituo vya radio. Na wakati huo huo sisi tunaomba kupata nafasi hiyo hiyo katika nchi kama ya China, na nchi za Ulaya, Marekani ambako tumechorwa vibaya. Ingawa tunataka kuamini wachina wanaweza kupeana taswira sawa yetu, lakini zaidi tungetaka na sisi tupate nafasi ya kujieleza kwa wachina sisi wenyewe moja kwa moja. Yaani tungetaka tuwe na vipindi katika luninga ya China pahali ambapo tukaweza tukieleza juu ya maendeleo tuliyoyapata, yale ambayo tunataka kuyafanya kesho na kesho kutwa. Kama vile kituo cha mafasa ya FM hapa China, tuweze kujielezea, kutangazia biashara, bidhaa tunazotoa, kuelezea utamaduni wetu, ndiyo wachina wanaweza kutuelewa vile tulivyo kuliko propaganda ambazo zimesambaziwa duniani ambazo siyo sahihi. Kwa hivyo namna ya pekee ya watu kujuana vizuri zaidi ni kuweza kupeana nafasi ya kila mtu kueleza yake pasipo ya kumtegemea mwingine. Na tukielewana hivyo nadhani tutafika pahali ambapo tunaweza kutegemeana kuelezana bila ya kupotosha chochote mmoja juu ya mwingine.
CRI: Bila shaka una imani kubwa juu ya kufanya ushirikiano kati ya China na Kenya katika sekta mbalimbali?
Waziri: Nasema kweli siyo imani tu, wengi katika serikali tumeona kuna haja ya uhusiano huo, kwa sababu biashara kati yetu na nchi za magharibi kuna kasoro yake, wale walikuwa ni watawala wetu, na wale bado wana hamu ya kuendelea kututawala kiuchumi ikiwezekana. Huo ni muda wetu wa kutafuta marafiki wapya tunawatafuta katika China na nchi nyingine za Asia, pia tunatafuta marafiki wapya katika nchi za magharibi, lakini siyo wale wale wenye kasumba ya kikoloni, wale wale ambao wanaamini watu wa dunia nyingine ni watu wa kunyanyaswa, ni watu wa kudunishwa. Na kwa sababu hiyo tuna imani kubwa, haja kubwa na nia kubwa ya kuhakikisha kwamba, tumefanya watu wa China na watu wengine wa dunia hii kuwa marafiki zetu wa dhati.
Idhaa ya Kiswahili 2006-09-29
|