Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-04 18:25:59    
China yahifadhi sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin kwa teknolojia za kisasa

cri

Sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin ambazo ni vitu vilivyozikwa pamoja na mfalme wa enzi ya Qin zinajulikana duniani na kusifiwa kuwa ni "ajabu la nane duniani". Katika miaka ya hivi karibuni, maonesho ya sanamu hizo yalifanyika mara nyingi katika nchi mbalimbali duniani. Sanamu hizo za mfinyanzi zilizozikwa chini ya ardhi kwa milenia kadhaa zikitoka hewani, rangi zake zilizopakwa kwa nje zitaharibika haraka. Ili kuhifadhi vizuri rangi zilizopakwa kwenye sanamu hizo, watafiti wa China wanaoshughulikia hifadhi ya vitu vya kale wamefanya utafiti mwingi. Lakini je walitumia mbinu gani kuhifadhi uzuri wa sanamu hizo wa hapo awali?

Katika majira ya mchipuko ya mwaka 1974, wakulima wa wilaya ya Lintong iliyoko kilomita 37 kutoka mji wa Xi'an mkoani Shanxi, walipochimba kisima cha maji, walifukua vipande vidogo vya sanamu za ufinyanzi kutoka mita mbili chini ya ardhi, ugunduzi huo umefuatiliwa sana na idara za kuchunguza vitu vya kale za China, na kazi za kufukua vitu hivyo zilifichua kaburi la mfalme wa enzi ya Qin ambayo ni hazina ya utamaduni iliyozikwa chini ya ardhi kwa miaka zaidi ya 2200.

Kwenye kasri hilo kubwa lililoko chini ya ardhi, kuna sanamu elfu kadhaa za askari zinazofanana na binadamu halisi na zimepangwa kwa utaritibu mzuri, jambo la kushangaza zaidi ni kwamba kila sanamu ina nguo na sura tofauti. Mbali na hayo, pia kuna farasi wa ufinyanzi wanaofanana na farasa halisi, na farasi hao ambao wamepangwa kwa vikundi nne, wanavuta mikokoteni ya kivita. Sanamu hizo nyingi zina rangi ya kijivu, lakini pia kuna sanamu chache zenye rangi za kupendeza.

Mtafiti wa jumba la makumbusho la sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin Bw. Zhou Tie alieleza, wakati sanamu hizo zilipofukuliwa, nyingi kati yake bado zilikuwa na rangi zinazong'ara. Lakini baada ya sanamu hizo kutoka hewani kwa muda mfupi tu, rangi zake zilitoweka haraka.

"Hali hiyo inatokana na sababu mbili, ya kwanza ni kwa kuwa sanamu hizo zilifukiwa chini ya shinikizo kubwa la ardhi kwa miaka zaidi ya elfu mbili, ya pili ni kwamba vitu muhimu vinavyoitwa kitaaluma Pectin vipo kwenye rangi zilizopakwa kwenye sanamu hizo vilitoweka au kuharibika haraka baada ya kufukuliwa."

Ili kukabilina na tatizo hilo, jumba la makumbusho la sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin lilitumia raslimia nyingi za vitu na nguvukazi na kuanzisha kikundi cha kuhifadhi rangi za sanamu hizo. Kikundi hicho kilifanya majaribio mengi na kufahamu kwa hatua ya mwanzo namna ya kuhifadhi rangi hizo. Mbali na hayo, kikundi hicho pia kinashirikiana na idara za utafiti na wataalamu wa nchi za nje, ili kupata teknolojia bora ya kuhifadhi rangi za sanamu hizo.

Mtafiti wa jumba hilo la makumbusho Bw. Zhou Tie alieleza kuwa, pamoja na utafiti wa kujitegemea, wataalamu wa China pia walianzisha ushirikiano na wataalamu wa Ujerumani. Pande mbili zilifanya majaribio mengi ya kemikali na njia mbalimbali zaidi ya kumi, na hatimaye zilipata maendeleo makubwa ya teknolojia. Bw. Zhou Tie alisema:

"katika ushirikiano huo uliodumu kwa miaka zaidi ya kumi, China na Ujerumani zilitumiana wataalamu, wataalamu wa China wanaongoza kazi za usanifu wa majaribio na Ujerumani inatoa misaada ya nguvu kazi, fedha na teknolojia kwa China. Kutokana na juhudi za pamoja za nchi hizo mbili, mradi wa hifadhi ya rangi za sanamu hizo ulikamilika kwa mafanikio."

Wataalamu walisema, teknolojia hii si kama tu yamehifadhi rangi za sanamu hizo zilizotengenezwa katika miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, bali pia ilitoa nyaraka muhimu kwa utafiti wa historia kuhusu uchoraji wa rangi na rangi za nguo za wakati huo. Lakini kwa watafiti wa jumba hilo la makumbusho, haimaanishi kukamilika kwa kazi za utafiti wa hifadhi ya rangi za sanamu hizo, naibu mkuu wa jumba hilo la makumbusho Bw. Lei Yuping alisema:

"hifadhi ya rangi za sanamu hizo si lengo letu la mwisho, bali ni mbinu moja tu. jambo muhimu zaidi ni kuonesha sanamu hizo kwa watalii wa nchini China na wa nchi za nje kwa kutumia teknolojia za kisasa, ili kufahamisha zaidi utamaduni wa China kote duniani."

Wakati wa kukamilisha zaidi teknolojia za hivi sasa za hifadhi ya rangi za sanamu, jumba la makumbosho la sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin pia limeanzisha utafiti kuhusu matatizo mengine ya rangi kwenye sanamu hizo.

Aidha, hivi sasa China pia inafanya uchunguzi wa mfululizo kuhusu uchafuzi wa hewa ndani ya jumba la makumbusho la sanamu za askari na farasi, na kutathmini kikamilifu hali ya kuharibika kwa sanamu hizo iliyosababishwa na vitu vichafu; kujenga ghala la data za jumla kuhusu hali ye hewa ya ndani ya jumba, gesi za kuunguza na vumbi; kutafiti umaalum wa jumla na utaratibu wa mabadiliko ya uchafuzi wa hewa ndani ya jumba hilo la makumbusho."

Kwa mujibu wa takwimu husika, tangu jumba la makumbusho la sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin lifunguliwe, limepokea watalii zaidi ya milioni 55 wa China na wa nchi za nje, miongoni mwao watalii wapatao milioni 5.5 wanatoka nchi za nje, na viongozi zaidi ya 140 wa nchi za nje waliwahi kutembelea jumba hilo la makumbusho. Wengi wao walisifu sana juhudi zilizofanywa na China katika kuhifadhi sanamu hizo. Mtalii mmoja kutoka Ufaransa Bw. Jean Andraux alisema:

"sanamu za askari na farasi wa enzi ya Qin huenda ni kaburi kubwa kabisa la mfalme lililohifadhiwa vizuri kabisa duniani, na limeonesha juhudi kubwa zilizofanywa na China katika kuhifadhi mabaki ya kihistoria na ya kiutamaduni."

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu jinsi China ina inavyohifadhi sanamu wa askari na farasi wa enzi ya Qin kwa teknolojia za kisasa. Asanteni kwa kutusikiliza. Kwa herini!

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-04