Utafiti wa awali uliofanywa na wanasayansi katika nchi za Uganda na Kenya, na kuwasilishwa kwenye kongamano la 16 la kimataifa la Ukimwi lililofanyika nchini Canada mapema mwezi Agosti, umeunga mkono ripoti iliyokuwa imetolewa hapo kabla na kundi jingine la utafiti uliofanywa nchini Afrika Kusini, na kubaini kuwa tohara kwa wanaume inaweza kusaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa zaidi ya asilimia 60.
Kwenye makala maalum ya afya iliyochapishwa katika gazeti la kila wiki la The East African ni kuwa, utafiti wa Afrika Kusini ulifanywa na kundi la wanasayansi kutoka nchini Ufaransa mwaka 2003, na kuwahusisha wanaume 3,274 katika shamba lililoko huko Orange, karibu na mji wa Soweto.
Matokeo ya uchunguzi huo yamepewa nguvu na utafiti mwingine uliofanywa nchini Kenya katika mji wa Kericho na kundi la Walter. Uchunguzi wa wanasayansi wa kundi la Walter uliowahusisha wanaume 324 umebaini kuwa, kufanyiwa tohara kwa wanaume kunapunguza hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi hadi kiwango cha asilimia 69.
Matokeo ya tafiti hizo yanatarajiwa kutoa shinikizo kwa Shirika la Afya Duniani, WHO, hata kuidhinisha rasmi sera ya tohara kwa wanaume kama njia mojawapo ya kupunguza hatari ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Nako nchini Uganda familia 300 za wanaume na wanawake zilifanyiwa uchunguzi, na kuthibitisha kuwa ikiwa wanaume watafanyiwa tohara, basi hatua hiyo inaweza kupunguza kwa asilimia 30 uwezekano wa wake zao kuambukizwa virusi vya Ukimwi. Mwezi jana makala moja ilitolewa na Dr. Auvert katika jarida la Plos Medicine, ambapo daktari huyo alidokeza kuwa kufanyika kwa tohara ya wanaume barani Afrika, kunaweza kuokoa maisha ya watu wapatao milioni tatu katika muda wa zaidi ya miaka 20 ijayo.
Jamii ambazo zinatekeleza tohara zimekuwa zikifanya hivyo kama njia mojawapo ya kuonesha kuwa kijana amevuka ujana na kuwa mwanaume. Lakini hivi sasa kutokana na matokeo ya utafiti huo, tohara inaweza kutiliwa mkazo zaidi kutokana na uvumbuzi huo. Hata hivyo tohara kwa vijana wa kiume vilevile inaweza kukabiliwa na upinzani kutoka na baadhi ya mila.
Idhaa ya Kiswahili 2006-10-04
|