Mwaka huu ni mwaka wa 50 tangu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya watu wa China na nchi za Afrika uanzishwe. Tokea nusu karne iliyopita, ingawa mabadiliko mengi yalitokea katika hali ya dunia, lakini uhusiano wa kirafiki umedumishwa kati ya pande hizo mbili, ambapo ushirikiano kati ya pande hizo mbili kwenye sekta za siasa, uchumi, utamaduni na sekta nyingine unaendelea katika hali ya utulivu, ushirikiano huo umekuwa mfano wa kuigwa wa uhusiano kati ya nchi zinazoendelea. Gazeti la Renminribao la China tarehe 11 limechapisha makala aliyoandika balozi wa Ethiopia nchini China Bwana Hailekiros Geseesee, ambayo imeeleza vilivyo uhusiano kati ya Afrika na China.
Makala hiyo inasema katika miongo kadhaa iliyopita, China na Afrika ziliungana mkono na kushirikiana barabara katika mambo makubwa ya kimataifa na kikanda yaliyojadiliwa kwenye Umoja wa Mataifa na majukwaa mengine ya kimataifa, ambapo zililinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea. Serikali ya China inatilia maanani ushirikiano wa kiuchumi na nchi za Afrika. Katika miaka mingi iliyopita, China ilitoa misaada mingi ya kimali na kifedha, kuzihamasisha kampuni za China kuwekeza na kuanzisha viwanda barani Afrika, kuharakisha ushirikiano wa kikanda kwenye sekta za elimu na matibabu na maingiliano ya kiutamaduni, na kuzidisha urafiki kati ya China na nchi mbalimbali za Afrika. Sera ya kidiplomasia ya China kwa Afrika siku zote inashikilia kuheshimiana, na kutendeana kwa usawa, China haiweki masharti yoyote ya vizuizi katika ushirikiano kati yake na nchi za Afrika kwenye sekta za uchumi na siasa, hasa serikali ya China itatoa misaada kwa nchi za Afrika bila masharti yoyote.
Makala hiyo inasema baada ya kuingia kwenye karne ya 21, China na Afrika zinakabiliwa na hali mpya ya kimataifa, hivyo zinatakiwa kuthibitisha sera mpya ili kuongeza mshikamano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili, na kuendeleza uhusiano wa kirafiki kwenye kiwango kipya. Katika hali hiyo mkutano wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mwezi Oktoba mwaka 2000, mkutano huo ulifungua ukurasa mpya muhimu kwenye historia ya uhusiano kati ya China na Afrika. Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika limeweka msingi mpya kwa maendeleo ya uhusiano kati ya pande hizo mbili, nyaraka mbili muhimu za "Taarifa ya Beijing ya Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika" na "Mwongozo wa ushirikiano kati ya China na Afrika kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii" zilizopitishwa kwenye mkutano wa kwanza wa baraza hilo zimekuwa dira za vitendo vya kuongeza ushirikiano kati ya China na Afrika.
Makala hiyo inasema kutokana na utaratibu wa mpango wa utekelezaji baada ya mkutano wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, mkutano wa mawaziri na maofisa waandamizi ufanyike kwa zamu nchini China au katika nchi za Afrika. Ethiopia ilipata fahari ya kuchaguliwa kuwa nchi mwendeshaji wa mkutano wa 2 wa mawaziri, mkutano huo muhimu ulifanyika mwezi Desemba mwaka 2003 huko Addis Ababa, "Mpango wa utekelezaji wa Addis Ababa" uliopitishwa kwenye mkutano huo uliongeza zaidi ushirikiano kati ya China na Afrika. Tokea mkutano huo, maendeleo makubwa yamepatikana katika ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta mbalimbali. Kutungwa kwa "Mpango wa utekelezaji wa Addis Ababa" kumeleta maendeleo makubwa katika historia ya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika, mpango huo unasaidia kutekeleza kanuni na malengo yaliyowekwa kwenye "Taarifa ya Beijing ya Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika" na "Mwongozo wa ushrikiano kati ya China na Afrika kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii.
Makala hiyo pia inasema, mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika pamoja na mkutano wa 3 wa mawaziri wa baraza hilo itafanyika hivi karibuni, ambapo wakuu wa China na nchi za Afrika watakutana mjini Beijing, kuzungumzia urafiki na ushirikiano, kupanga mipango ya maendeleo na kujenga siku za mbele. Watu wanatarajia mikutano hiyo itaweza kutunga nyaraka kadhaa zenye umuhimu mkubwa zaidi wa kimkakati ili kuzidisha ushirikiano kati ya China na Afrika.
Balozi Geseesee alisisitiza kuwa China ni kama mnara wa taa wenye ishara ya matumaini kwa Afrika. Wananchi wa Afrika wanaweza kujifunza kutoka kwa uzoefu wenye mafanikio wa China kutokana na hali yao halisi. Nchi za Afrika zinahitaji kujenga uhusiano wa kirafiki ulio wa usawa, kunufaishana na ushirikiano wa dhati na China, ili kusukuma mbele maendeleo endelevu ya uchumi wa Afrika.
Idhaa ya Kiswahili 2006-10-06
|