Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-13 15:14:34    
Mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika kuharakisha ujenzi wa uhusiano mpya wa kimkakati kati ya pande hizo mbili

cri

Mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika mkutano wa 3 wa mawaziri wa baraza hilo unatazamiwa kufanyika hapa Beijing kuanzia tarehe 3 hadi 5 Novemba mwaka huu. Wataalamu husika wanachukulia kuwa, kufanyika kwa mikutano hiyo kutasukuma mbele ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika, na kufanya kazi muhimu katika kukuza uhusiano kati ya China na Afrika na kuharakisha ujenzi wa uhusiano wa kimkakati na kiwenzi kati ya China na Afrika.

Mtafiti wa idara ya utafiti wa mambo ya Afrika ya Taasisi ya Sayansi ya Jamii ya China Bi. He Wenping alisema, mkutano huo wa wakuu utafanyika wakati wa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na nchi za Afrika, ni tukio muhimu katika historia ya uhusiano kati ya China na Afrika, pia ni tukio muhimu katika historia ya kidiplomasia ya Jamhuri ya watu wa China. Kutokana na takwimu za awali, wakuu 40 hivi wa nchi za Afrika wanatazamiwa kuhudhuria mkutano huo, jambo hili bila shaka litasukuma mbele uhusiano kati ya China na Afrika. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Qin Gang alifahamisha kuwa, kauli mbiu ya mkutano huo itakuwa "urafiki, amani, ushirikiano na maendeleo".

Wakati wa mkutano huo, viongozi wa China na nchi za Afrika watajumuisha mchakato wa urafiki na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika miaka 50 iliyopita, na mafanikio yaliyopatikana tangu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lianzishwe, kuweka ushirikiano wa kufuata ufanisi katika siku zijazo, na kubadilishana maoni kuhusu mambo makubwa ya kimataifa.

Habari zinasema nyaraka zitakazotolewa baada ya mkutano huo zitabainisha sekta mbalimbali za ushirikiano. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China kwa mara ya kwanza ilitoa waraka wa sera ya China kwa Afrika, ukitoa pendekezo la kuanzisha uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi kati yake na nchi za Afrika wenye usawa na kuaminiana kisiasa, kufanya ushirikiano wa kunufaishana kiuchumi na kufundishana katika sekta ya utamaduni. Rais Hu Jintao wa China na waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao walitembelea nchi 10 za Afrika mwezi Aprili na mwezi Juni mwaka huu. Mkuu wa Idara ya Utafiti wa Mambo ya Afrika ya China Bwana An Yongyu alisema, ni nadra kwa rais na waziri mkuu wa China kutembelea nchi za Afrika katika mwaka mmoja, jambo hilo limedhihirisha kuwa China inatilia maanani sana uhusiano kati yake na Afrika.

Bwana An Yongyu alisema Afrika ni bara lenye nchi nyingi kabisa zinazoendelea, na China ni nchi kubwa kabisa inayoendelea duniani, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya China na Afrika ni chaguo la muda mrefu la kimkakati la China. Mkurugenzi wa idara ya utafiti wa mambo ya Afrika ya Taasisi ya Utafiti wa Uhusiano wa Kimataifa wa China wa zama zetu Bwana Xu Weizhong alisema, uhusiano kati ya nchi za magharibi na Afrika hauna usawa, nchi za magharibi zinapenda kuhusisha misaada na masharti fulani, na kuzilazimisha nchi za Afrika kufuata sera zao. China inahimiza kuanzisha ushirikiano kati ya kusini na kusini wenye usawa na kushauriana na kunufaishana. Kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni "urafiki, amani, ushirikiano na maendeleo" imeonesha msimamo huo wa serikali ya China.

Licha ya kufanya mkutano wa wakuu, pia yatafanyika mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya viongozi wa China na Afrika na wajumbe wa wanaviwanda na wafanyabiashara, na mkutano wa pili wa wanakampuni wa China na Afrika. Wahusika wameona kuwa suala la biashara na uchumi hasa uwekezaji litakuwa ni mada muhimu itakayojadiliwa kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika unaendelea vizuri, thamani ya biashara ya pande hizo mbili iliongezeka kwa haraka na kufikia dola za kimarekani bilioni 40 katika mwaka 2005 kutoka ile ya dola bilioni 4 ya mwaka 1995, na thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja ya China katika nchi za Afrika imefikia dola za kimarekani bilioni1.18, na kuanzisha makampuni zaidi ya 800 barani Afrika.

Bi. He Wenping alisema ikilinganishwa na ongezeko la kasi la thamani ya biashara ya pande mbili, uwekezaji wapande mbili unaonekana ni dhaifu kidogo. Hivyo katika mkutano huo wa wakuu, viongozi wa China na Afrika watajadili hatua zitakazochukuliwa katika kuhimiza wanakampuni wa pande hizo mbili kuwekeza kwenye upande mwingine.

Kutokana na ongezeko la kasi la China kuagiza bidhaa kutoka nchi za Afrika mwaka hadi mwaka, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika umeingia katika kipindi kipya, ambao una mustakabali mzuri, tena utapata maendeleo makubwa katika siku zijazo. Watafiti wanaona kuwa, katika mkutano wa wakuu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, viongozi wa China na nchi za Afrika pia watafanya majadiliano kuhusu kuimarisha ushirikiano katika sekta za usalama kama vile kupambana na uhalifu na ugaidi na kulinda amani, na mawasiliano ya kiutamaduni.

Bwana An Yongyu alisema, historia na ukweli wa mambo umeonesha kuwa, ushirikiano kati ya China na Afrika una msingi mzuri. Kufanyika kwa mkutano wa wakuu kutaleta athari kubwa kwa uhusiano wa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-13