Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-16 17:18:34    
Mwanaharakati wa sanaa, Dong Mengyang

cri

Tamasha la kwanza la kimataifa la nyumba za sanaa lililofanyika miaka miwili iliyopita na "Tamasha la Sanaa la Beijing" litakalofanyika mwezi Oktoba, yote ni matamasha yaliyoandaliwa na mwanaharakati kijana wa sanaa nchini China Dong Mengyang. Kutokana na juhudi zake ameunganisha soko la sanaa la China na soko la nchi za nje.

Dong Mengyang ni kijana anayeonekana mwenye adabu na aibu, ingawa ana umri wa karibu miaka 40 lakini anaonekana bado ni kijana, wafanyakazi wenzake wamezoea kumwita "kaka mzuri". Dong Mengyang alisema, aliwahi kuwa na tumaini la kuwa msanii.

Dong Mengyang alizaliwa na kukulia mkoani Shanxi, toka alipokuwa mtoto alipenda kuchora picha. Alimaliza kozi yake ya uchoraji wa picha za mbao katika Chuo Kikuu cha Sanaa cha Beijing mwaka 1993, akapewa kazi katika kampuni moja ya sanaa na utamaduni mjini Beijing. Mwaka huo kampuni yake ilitaka kufanya tamasha la kwanza la sanaa nchini China, Dong Mengyang alishiriki kwenye maandalizi ya tamasha hilo. Mwaka 1993 tamasha hilo lilifanyika mjini Guangzhou, mji ambao ulikuwa mbele katika mageuzi ya uchumi nchini China. Dong Mengyang alisema, "Tamasha la mwaka 1993 lilikuwa ni la kwanza kabisa kufanyika nchini China, tamasha hilo ni tofauti na maonesho ya kawaida, bali ni maonesho ya picha yaliyowashirikisha wachoraji, washiriki wote walikuwa ni wasanii, hawakuwa na madalali. Wakati huo soko la sanaa nchini China lilihitaji aina hiyo ya tamasha na wasanii pia walikuwa na haja ya kuonesha na kuuza picha zao wao wenyewe."

Dong Mengyang alieleza kuwa kwa kawaida maonesho ya picha katika nchi za nje hufanywa kwa kuzishirikisha nyumba za sanaa na wasanii hawashiriki kwenye maonesho. Lakini mwaka 1993 nyumba za sanaa zilianza tu kutokea nchini China, ingawa nyumba za sanaa hazikuwepo kwa hata miaka mia moja iliyopita, lakini shughuli zake hazikuwa maonesho ya sanaa bali zilikuwa ni duka tu la kuuzia picha. Nyumba ya sanaa ni dalali wa wasanii maalum kwa mkataba wa kuwaunganisha wauzaji, wasanii na wahifadhi na kuwapa nafasi za maingiliano.

Kutokana na kuendelea kwa uchumi wa China, wahifadhi wa vitu vya sanaa wanaongezeka, na nyumba halisi za sanaa pia zinaongezeka, soko la sanaa limeanza kustawi nchini China, Kutokana na hali hiyo, mwaka 2003 baada ya kufanya tamasha la sanaa kwa mara ya kwanza Dong Mengyang alijiuzulu kutoka kwenye kampuni yake na kuanza kushughulika na tamasha la kimataifa la sanaa, ili awapatie wasanii wa nchini China na wa nchi za nje jukwaa la mawasiliano. Alisema, "Habari kutoka nchi za nje zinanifahamisha kwamba katika nchi za nje tamasha la sanaa linafanyika kwa msingi wa nyumba za sanaa na nyumba hizo za sanaa zinataka kuingia nchini China, hivyo soko la China litakuwa la kimataifa. Kutokana na hali hiyo nimemua kuwahudumia wasanii wa China na wa nchi za nje."

Mwaka 2004 Dong Mengyang kwa mara ya kwanza alifanya tamasha la kimataifa la sanaa lililowashirikisha madalali. Nyumba za sanaa kutoka Korea ya Kusini, Japan, Italia, Marekani na Uholanzi karibu mia moja zilishiriki kwenye tamasha hilo. Washiriki walifurahia sana tamasha hilo, waliona kwamba kutokea kwa tamasha hilo kulitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kuimarisha msingi wa soko la sanaa nchini China.

Ufanisi wa tamasha lake la kwanza nchini China haukumfanya Dong Mengyang avimbe kichwa, aliona kwamba soko la sanaa nchini China bado liko mwanzo tu wa safari yake ya maendeleo, na elimu ya sanaa kwa umma, kiwango cha kupima sanaa na ufahamu wa maana ya kuhifadhi vitu vya sanaa bado ni wa chini. Alisema soko la sanaa haliwezi kustawi sana mpaka wakati ambapo uchumi utakuwa umeimarika sana. Kwa hiyo, mwezi Oktoba mwaka huu atafanya tamasha la "Sanaa ya Beijing". Alisema, "Nafikiri kuwa hivi sasa soko la sanaa nchini China limestawi kiasi, lakini soko hilo limekuwa la kibiashara kupita kiasi, tamasha la sanaa linaonekana kama halihusiani na sanaa bali ni soko la biashara tu, naona wakati huo ni lazima niwe mtulivu, ni lazima niimarishe taaluma na kuwaambia wanunuzi nini maana ya vitu vya sanaa, na kuwaambia mwelekeo wa hifadhi ya vitu vya sanaa kinadharia. Naona kwamba thamani ya vitu vya sanaa sio ya kibiashara tu, bali ni thamani ya uzuri wake, thamani ya kibiashara ipo lakini sio thamani yake yote."

Tamasha la "Sanaa ya Beijing" limechagua nyumba za sanaa 85 kutoka nyumba zaidi ya 200 kutoka nchini na nchi za nje. Dong Mengyang alisema, "Tumechagua nyumba za sanaa kwa asilimia 50 kutoka nchini China, asilimia 30 kutoka nchi nyingine za Asia na asilimia 20 kutoka Ulaya na Marekani, yaani nyumba za sanaa za China zinachukua kiasi kikubwa katika tamasha hilo, tumechagua nyumba za sanaa kutoka Ulaya na Marekani lakini haifai kuchagua nyumba nyingi za sanaa, bali tumechagua zile tu ambazo zinataka kuanzisha nyumba zao nchini China."

Dong Mengyang mara nyingi alitaja "Tamasha la Sanaa la Basel" katika mazungumzo yake. Kwani "Tamasha la Sanaa la Basel" ni tamasha maarufu sana duniani. Bw. Dong Mengyang anatumai "Sanaa ya Beijing" litakuwa kama "Tamasha la Basel" baada ya miaka 20, kwamba watu wanapotaja "Tamasha la Sanaa la Beijing" itakuwa ni kama wanavyolifahamu "Tamasha la Sanaa la Basel". Kuhusu lengo hilo Dong Mengyang ana uhakika. Alisema,

"Hivi leo China ipo katika kipindi muhimu cha maendeleo ya historia, hatua kwa hatua hakika itatangulia mbele kati ya nchi za Asia katika sekta ya tamasha la sanaa na soko la sanaa. Natumai "Tamasha la Sanaa la Beijing" litakuwa kituo cha kukusanya na kusambaza vitu vya sanaa vya bara la Asia, watu wanaotaka kuona vitu vya sanaa vya Asia kwa uzuri na aina nyingi kwanza watakumbuka "Tamasha la Sanaa la Beijing."

Idhaa ya kiswahili 2006-10-16