Sehemu ya magharibi mwa China ina mikoa na miji 12 kwa jumla, eneo lake ni kilomita za mraba milioni 6.85 likichukua asilimia 71.4 ya ardhi yote ya China, na ina idadi ya watu milioni 367. Sehemu ya magharibi ya China ina rasilimali nyingi na soko kubwa katika siku za baadaye. Kutokana na vyanzo vya kimaumbile, kihistoria na kijamii, maendeleo ya uchumi ya sehemu ya magharibi yamekuwa nyuma ikilinganishwa na ya sehemu nyingine za China, hivyo sehemu hiyo inataka sana kuharakisha hatua za mageuzi, ufunguaji mlango na ujenzi wa kisasa. Mwezi Januari mwaka 2000, serikali ya China iliamua kuanzisha harakati kubwa za kustawisha sehemu ya magharibi.
Guangxi ni moja ya mikoa 12 inayoshiriki kwenye harakati hizo za ustawishaji. Ili kuharakisha ujenzi wa kisasa na kuhimiza maendeleo ya uchumi, mwezi Julai mwaka huu serikali ya mkoa unaojiendesha wa Guangxi ilitoa wazo la kuanzisha "eneo kubwa la ushirikiano wa uchumi la ghuba ya kaskazini". Naibu mkurugenzi wa ofisi ya kamati ya usimamizi wa mpango wa ujenzi wa eneo la uchumi Bw. Wang Naixue alisema,
"Eneo la uchumi la ghuba ya kaskazini ni wazo jipya, ambalo linaundwa na miji ya Beihai, Qinzhou, Fangchenggang na Nanning iliyoko kwenye sehemu ya pwani ya mkoa wa Guangxi. Eneo hilo la uchumi lina kilomita za mraba elfu 42.5 na idadi ya watu milioni 12.2." Kuhusu sababu ya kuweka mpango mmoja wa maendeleo kwa miji hiyo 4, na kuanzisha eneo la uchumi la Guangxi la ghuba ya kaskazini, mkurugenzi Wang alisema,
"Eneo hilo lina rasilimali nyingi na uwezo mkubwa wa masoko katika siku za baadaye. Eneo hilo linapakana na nchi za Asia ya kusini mashariki kwenye ardhi na baharini, na ni njia pekee ya kwenda kwenye nchi hizo kutoka China. Licha ya hayo, mkoa wa Guangxi una pwani yenye urefu wa kilomita 1,600, katika maendeleo ya uchumi wa kisasa, bahari ni rasilimali kubwa, ambayo inanufaisha upangaji mwafaka na uendelezaji wa rasilimali.
Kwa hiyo serikali ya mkoa wa Guangxi imeunganisha miji hiyo minne kuwa eneo moja la kiuchumi na kuendelezwa kwa mpango mmoja, kusawazisha maendeleo yake, kupanga kwa njia mwafaka ujenzi wa miradi na matumizi ya mitaji ili kuwa na nguvu kubwa ya maendeleo."
Mkurugenzi Wang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, wafanyabiashara wengi wa nchini na wa nchi za nje waliposikia habari kuhusu mkoa wa Guangxi kujenga eneo jipya la ustawishaji uchumi, walivutiwa sana na habari hiyo, baadhi ya makampuni ya kimataifa yalikwenda huko kufanya uchunguzi. Mkuu wa mkoa wa utawala maalumu wa Hong Kong Bw. Zeng Yingquan aliongoza kundi la watu kwenda kufanya uchunguzi kwenye ghuba ya kaskazini, tena aliongoza wanaviwanda zaidi ya 80 kutembelea mji wa Fangchenggang.
Katika mazingira ya maendeleo ya kasi ya utandawazi wa uchumi duniani, umoja wa uchumi wa kikanda unaimarishwa kwa mfululizo. Pamoja na kuanzishwa na kuwepo kwa maendeleo ya kasi ya uhusiano wa kiwenzi kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, ghuba ya kaskazini ikiwa ni sehemu inayounganisha China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, imezingatiwa na pande mbalimbali. Sasa China inatoa wazo la kuanzisha ushirikiano wa uchumi wa kimataifa unaounganisha "eneo la kiuchumi la ghuba ya kaskazini", kanda ya mto Mekong na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Naning na Singapore, na kuungwa mkono sana na Vietnam, Thailand na Singapore, hususan kuanzisha miradi ya uwekezaji na biashara kutaleta faida na mali kwa kundi la nchi 10 + 1. Kwa mfano, viwanda vilivyoko kwenye eneo la delta ya Lulu nchini China vinataka sana kuhamia nchi za nje, wakati Vietnam, Thailand, Cambodia, Mynanmar na Laos zinataka kuvutia uwekezaji. Licha ya hayo baada ya kukamilika kwa mawasiliano kati ya Nanning na Singapore, nchi za peninsula ya Indo-China zitaweza kutumia rasilimali na masoko mengi ya nchi za nje, kuongeza shughuli za biashara na usambazaji bidhaa, na kuhimiza ongezeko la miradi ya uwekezaji, ambapo shughuli nyingi za biashara zilizofanyika kwenye sehemu nyingine, sasa zinaweza kufanyika katika eneo hilo.
Mbali na hayo, eneo la uchumi la ghuba ya kaskazini la mkoa wa Guangxi linaweza kutumia ipasavyo ubora wa kijografia wa sehemu yake na kuhimiza ujenzi wa sehemu muhimu na kuchagua miradi bora halisi.
Kwa mfano, mji wa Fangchenggang uko kando ya ghuba ya kaskazini, mji huo wa viwanda ni mpya na mzuri.
Mji wa Fangchenggang ulianza kujengwa mwaka 1968, na unajulikana kwa kuwa na moja kati ya bandari kubwa yenye magati yanayoweza kutia nanga kwa meli zenye uwezo wa kubeba tani laki 2 za mizigo. Mkurugenzi wa ofisi ya kampuni ya Fangchenggang Bw. Ren Weibin alisema,
"Bandari hiyo sasa imejengwa ina magati 35, na 21 kati yake yanaweza kutia nanga kwa meli za tani zaidi ya elfu kumi, hivi sasa bandari hiyo ina uwezo wa kushughulikia tani zaidi ya milioni 25 za mizigo, na imekuwa na uhusiano wa usafirishaji na bandari zaidi ya 220 za nchi zaidi ya 70 duniani, hususan kutumika kwa magati ambayo meli zenye uzito wa tani laki mbili zinaweza kutia kumeongeza nguvu za ushindani."
Pamoja na kuharakishwa kwa hatua za ujenzi wa eneo la biashara la umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, ubora wa kijografia na wa bandari ya mji huo umekuwa muhimu mwaka hadi mwaka. Hivi sasa mji huo una fursa nzuri ya kujenga eneo la ustawishaji uchumi la ghuba ya kaskazini, umekuwa na wazo la kujenga bandari kubwa ya kimataifa na kujenga viwanda vingi kwenye sehemu ya pwani.
Ili kuendeleza ushirikiano na ustawishaji wa ghuba ya kaskazini, mkoa wa Guangxi umezindua mradi wa ujenzi wa eneo la ustawishaji uchumi, na unanuia kujenga mkoa huo kuwa kituo cha usambazaji bidhaa cha kikanda kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-17
|