Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-20 17:12:40    
Misaada ya China kwa Afrika ni ya dhati

cri

China ilianza kutoa misaada kwa nchi za Afrika mnamo miaka ya 50 karne iliyopita. Ikiwa nchi inayoendelea, China imewaunga mkono na kuwasaidia watu wa Afrika kwa hali na mali. Katika miaka 50 iliyopita, China imezipatia misaada ya aina mbalimbali nchi za Afrika yenye thamani zaidi ya Reminbi Yuani bilioni 44.4 sawa na dola za kimarekani bilioni 5.6, kukamilisha miradi karibu 900 ya miundo mbinu, na kupeleka madaktari elfu 16 kwa nchi 47 za Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, China ilipunguza madeni 156 yenye thamani ya renminbi Yuan bilioni 10.5 kwa nchi 31 za Afrika, na kutimiza ahadi yake ya kutoa mafunzo mbalimbali ya kitaalamu kwa watu elfu 10 wa nchi za Afrika. Mbali na hayo, jumla ya wanajeshi zaidi ya 3000 wa China wamepelekwa kwenye nchi za Afrika kufanya kazi ya kulinda amani katika majeshi ya Umoja wa Mataifa.

Juhudi za China kusaidia nchi za Afrika zinasifiwa sana na watu wa Afrika. Viongozi wa mashirikisho makubwa ya wafanyakazi wa nchi za Afrika waliohudhuria kongamano lililofanyika hivi karibuni hapa Beijing China walieleza kuwa, misaada inayotolewa na China kwa Afrika ni ya dhati na ya moyo safi. Walisema misaada hiyo imewasaidia sana watu wa Afrika, na ni tofauti na ile iliyotolewa na nchi za magharibi. China inazisaidia nchi za Afrika katika miradi ya miundo mbinu kwa hali na mali bila ya kuweka masharti yoyote.

Mnamo mwishoni mwa mwaka 1963 hadi mwanzoni mwa mwaka 1964, wakati hayati waziri mkuu wa zamani wa China Bw. Zhou Enlai alipofanya ziara katika nchi 10 za Afrika, alifafanua kanuni ya China kutoa misaada kwa nchi za nje, akisema serikali ya China inaheshimu mamlaka ya nchi zinazosaidiwa, na kutoa misaada bila ya masharti yoyote. Hata sasa kanuni hiyo ni maelekezo ya China inapotoa misaada kwa nchi za Afrika.

Naibu mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Mambo ya Afrika na Nchi za Asia magharibi ya Taasisi ya Taifa ya Sayansi ya jamii ya China Bw. Zhang Hongming alifafanua kwamba, ikilinganishwa na nchi za magharibi, sera ya China kuhusu kutoa misaada kwa Afrika ina umaalum wake, yaani kwanza, wakati inapotoa misaada kwa nchi za Afrika, China haiweki masharti yoyote, na wala haiingilii mambo ya ndani ya nchi zinazopewa misaada na kudai haki maalum. Pili, madhumuni ya China kutoa misaada kwa nchi za Afrika ni kuzisaidia kuongeza uwezo wa kujitegemea, hivyo China inatilia maanani kuwafundisha wataalam na meneja kwa nchi hizo. Tatu, China inapotoa misaada inachagua miradi ambayo inahitajika zaidi kwa nchi zinazosaidiwa. Nne, serikali ya China siku zote inatoa misaada kwa kuambatana ns kanuni ya usawa na kunufaishana.

Huu ni mwaka wa 50 tangu China mpya ianzishe uhusiano wa kibalozi na nchi za Afrika. Katika miaka 50 iliyopita, misaada iliyotolewa na China imetoa michango muhimu katika kuhimiza maendeleo ya kiuchumi, kuboresha maisha ya watu, kuinua kiwango cha elimu, matibabu na huduma za afya na nyinginezo barani Afrika. Miradi mingi ya misaada iliyotolewa na China ikiwemo Reli ya TAZARA, Bandari ya urafiki ya Mauritania zimekuwa nguzo za kiuchumi katika nchi hizo. Sio tu misaada hiyo iliimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika tu, bali pia imeongeza uaminifu, na kuhimiza mawasiliano na uratibu wa misimamo ya kisiasa kati ya pande hizi mbili. Katika masuala mengi ya kimataifa, China imeungwa mkono na nchi za Afrika.

Kwa kuwa Afrika ni bara lenye nchi ambazo ziko nyuma kiuchumi duniani, kutoa misaada kwa nchi za Afrika ni sera ya kimkakati na ya muda mrefu ya serikali ya China. Tangu mwishoni mwa karne iliyopita, hali ya jumla ya uchumi wa Afrika imebadilika na kuanza kuwa nzuri. Lakini nchi nyingi katika bara hilo bado zinakabiliwa na matatizo mbalimbali katika juhudi zao za kujiendeleza, na zinahitaji misaada kutoka nchi za nje katika maendeleo ya kiuchumi.

Mwenyekiti wa shirikisho kuu la wafanyakazi wa Namibia Bw. Alphaus Vehonga Muheua alisema, China ni nchi ya kwanza iliyotoa misaada kwa Namibia, na kuwasaidia sana watu wa nchi hiyo katika kujipatia uhuru. Sasa China inaisaidia Namibia kujenga jumba la serikali huko Windhoek mji mkuu wa nchi hiyo. Aliongeza kuwa watu wa Namibia wanawashukuru sana watu wa China, na kuwachukulia kama ni ndugu wa damu.

Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika unaendelea kwa kasi. Baadhi ya watu wa Afrika wana wasiwasi kwamba mauzo ya bidhaa za China zenye bei nafuu katika nchi za Afrika yataharibu maendeleo ya viwanda vya nchi hizo. Bw. Muheua alisema watu wa Afrika wanafurahia bidhaa zinazotengenezwa nchini China kuwa ni zenye bei nafuu, hali ambayo imeleta shinikizo kwa viwanda na wafanyabiashara wenyeji barani Afrika. Lakini kwa upande mwingine, ushindani huo unaleta mabadiliko, wanaviwanda na wafanyabiashara wa Afrika wanapaswa kuiga mfano wa watu wa China, na kuimarisha uwezo wao.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-20