Katika miaka ya karibuni Beijing imehamisha viwanda vingi vya kazi nzito ambavyo ni pamoja na kampuni ya chuma na chuma cha pua ya mji mkuu, kiwanda cha makaa ya mawe na kiwanda cha mitambo ya vyombo (machine tool). Kuhamishwa kwa viwanda vya kizamani, siyo tu kwamba kunahimiza uboreshaji wa muundo wa sekta ya uzalishaji mali na kubadilisha mtindo wa ongezeko la uchumi mjini Beijing, bali pia kunapunguza matumizi ya nishati ya sekta ya uzalishaji mali, kuboresha mazingira ya hewa na kuweka msingi bora kwa michezo ya Olimpiki ya rangi ya kijani. Baada ya kuhamishwa sehemu nyingine, viwanda hivyo vitakuwa na teknolojia, zana na usimamizi wa kiwango cha juu.
Mwezi Julai mwaka jana, kampuni ya chuma na chuma cha pua ya mji mkuu, iliyoko kwenye sehemu ya magharibi mwa Beijing ilizima moto wa tanuri No. 5 la kuyeyusha chuma, ambalo limetumika kwa miaka 47. Mwaka mmoja baadaye, tanuri la kuzalisha makaa ya mawe la kiwanda cha makaa ya mawe kilichoko sehemu ya kusini mashariki mwa Beijing, pia lilisimamisha kazi. Viwanda hivyo viwili vikubwa vya serikali, ambavyo vilitoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Beijing katika karne karibu nusu iliyopita, vimetoweka machoni mwa watu.
Mwandishi wetu wa habari alipofika kwenye kiwanda cha makaa ya mawe hakuona hata mtu mmoja kwenye matanuri mawili ya kuzalisha makaa ya mawe. Mfanyakazi wa miaka mingi wa kiwanda hicho aliyemtembeza Bw. yang Xiaolin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, alifanya kazi kwenye matanuri hayo mawili kwa miaka 26, lakini sasa anasikitika sana kuacha kufanya kazi kwenye matanuri hayo.
"Kiwanda cha makaa ya mawe cha Beijing kimesimamishwa kazi kwa ajili ya kuboresha hewa kutokana na kuwa michezo ya Olimpiki itafanyika mjini Beijing. Matanuri hayo mawili bado yako katika kipindi cha ujana. Kwa kawaida matanuri ya namna hiyo hutumika kwa kiasi cha miaka 35, lakini matanuri hayo mawili yametumika kwa miaka 12 hivi. Hivyo kusimamishwa kazi zake, kunatusikitisha kidogo."
Kiwanda cha makaa ya mawe cha Beijing kilianza kuzalisha makaa mwezi Novemba mwaka 1985, na kuanzisha historia ya uzalishaji makaa nchini China. Mkuu wa sasa wa kiwanda hicho aliyefanya kazi kwa miaka zaidi ya 30 kwenye kiwanda hicho Bw. Zhang Xiwen alisema, wakati ule nishati iliyotumika zaidi ilikuwa ni makaa ya mawe, na moshi ulitandaa kwenye anga ya Beijing, hususan uchafuzi kwa hewa ulikuwa mbaya zaidi katika majira ya baridi, ili kupunguza uchafuzi, serikali ya Beijing ilifikiri kubadilisha muundo wa matumizi ya nishati ya Beijing, na iliamua kujenga kiwanda cha makaa ya mawe.
"Kiwanda hicho kilijengwa mwaka 1958 na kupanuliwa katika miaka ya 60. Gesi iliyozalishwa na kiwanda hicho licha ya kutumiwa na Jumba la mikutano ya wananchi, hoteli kubwa, balozi za nchi mbalimbali zilioko mjini Beijing na majengo ya serikali kuu ya Zhongnanhai, pia ilitumiwa na baadhi ya wakazi wa Beijing."
Kiwanda cha makaa ya mawe cha Beijing kiliongezwa matanuri mawili makubwa katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, na gesi iliyozalishwa na kiwanda hicho ilitumiwa na wakazi wengi zaidi. Bw. Zhang Xiyou alisema wakati ule gesi iliyotolewa na kiwanda hicho ilichukua kiasi cha 80% ya gesi yote iliyotumika mjini Beijing,
Mwanzoni baada ya kuasisiwa China mpya, Beijing iliweka mpango wa kujenga viwanda kadhaa vikubwa vya kazi nzito. Maendeleo ya kazi za viwanda yaliweka msingi kwa uchumi wa Beijing. Wakati ule, kiwanda cha makaa ya mawe cha Beijing kilikuwa moja ya viwanda muhimu kabisa vya Beijing, na thamani uzalishaji mali wake iliwahi kufikia 1% hivi ya jumla ya thamani ya uzalishaji mali ya Beijing.
Ingawa kiwanda hicho kilikuwa na historia ndefu, lakini pamoja na kupanuliwa kwa eneo la mji na kuongezeka kwa idadi ya watu, matatizo yanayosababishwa na viwanda vinavyotoa uchafuzi mwingi yanakuwa makubwa mwaka hadi mwaka. Kila mwaka serikali ya Beijing haina budi kutumia fedha na nguvu kazi nyingi kushughulikia uchafuzi unaotolewa na kiwanda cha makaa na kiwanda cha chuma na chuma cha pua. Kwa hiyo kufungwa kwa viwanda hivyo viwili vikubwa vya serikali ni chaguo la busara katika marekebisho ya muundo wa sekta ya uzalishaji mali na kuhamisha viwanda visivyoendana na hadhi ya mji mkuu wa Beijing. Naibu mkurugenzi wa idara ya uendelezaji wa viwanda ya serikali ya Beijing, Bibi Chang Qing alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, shughuli za marekebisho na uhamishaji wa viwanda vya Beijing zilianza mwanzoni mwa miaka ya 90, mwanzoni ilitokana na vitu vyenye uchafuzi na usumbufu vilivyotolewa kwa wakazi, na zilifanyika kwa kulazimika. Baada ya Beijing kuwa na wazo la kujenga mji huo wenye mazingira bora kwa wakazi na kufanya michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 kuwa michezo ya kijani, Beijing ilijituma kuchukua hatua za kuhamisha baadhi ya viwanda visivyofaa kwa mazingira ya mji mkuu. Alidokeza kuwa katika miaka 5 iliyoipita, viwanda 144 vilihamishwa kutoka kwenye eneo la mji la Beijing. Bibi Chang Qing alisema,
"Baada ya kuhamishwa kwa baadhi ya viwanda vikubwa vikiwemo kiwanda cha chuma na chuma cha pua na kiwanda cha makaa, muundo wa sekta ya uzalishaji mali wa viwanda na mazingira ya Beijing kimsingi yatakuwa yamebadilika. Licha ya kuweza kutatua kimsingi tatizo la uchafuzi wa viwanda, italeta nafasi mpya ya maendeleo kwa viwanda hivyo vinavyohamishwa, fedha vitakazopata kutokana na viwanja vya ardhi vya viwanda, zitatumika kuendeleza ujenzi wa viwanda na kuinua kiwago cha teknolojia ya viwanda."
Kitu kinachostahili kuelezwa ni kuwa kuhamisha viwanda hivyo hakuna maana ya kuhamisha uchafuzi, bali kujenga viwanda vya kisasa kwenye sehemu nyingine.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-24
|