Bwana Raphael Hokororo kutoka Tanzania pamoja na waandishi habari wengine wa za Afrika hivi sasa wako nchini China kushiriki kwenye semina ya waandishi wa habari wa Afrika. Yafuatayo ni mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Bw. Hokroro?
CRI: Kwanza Bwana Hokororo tungependa utuambie kwa ufupi nia ya wewe pamoja na watu umekuja nao, mmekuja kwa lengo gani safari hii?
Hokororo: Tumekuja Beijing kwa ajili ya semina ya waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika. Tuko waandishi 29 wa habari kutoka Tanzania, Kenya Botswana, Namibia, Sierra Leone, Ghana, Liberia, Djibouti na Ethiopia.
CRI: Ni mpango gani ambao umewahusisha waandishi wa habari wengi namna hii kutoka Afrika, kuna uhusiano wowote wa mambo ya habari kati ya Afrika na China?
Hokororo: Ziara hii imeandaliwa na wizara ya biashara ya China, ili sisi waandishi wa habari wa Afrika tuje tuone nini wanachofanya Wachina na tuweze kupeleka habari nyumbani.
CRI: Inaonekana hii si mara yako ya kwanza kufika China, kuna mabadiliko yoyote umeyaona?
Hokororo: Yapo mabadiliko makubwa katika miaka hii mitatu tangu safari yangu iliyopita nchini China. Ujenzi wa miundo mbinu umeendelea, barabara zimejengwa, majumba yanajengwa, na mji wa Beijing unapanuka sana.
CRI: Mwezi ujao kuna tukio kubwa kwenye baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, unafahamu kitu chochote kuhusu hilo baraza?
Hokororo: Nafahamu baraza hilo, lengo lake ni kujenga ushirikiano kati ya Afrika na China, na hasa hasa lengo ni kusaidiana, kubadilishana utaalamu. China ni nchi ambayo inaendelea sasa, na sisi Afrika bado ni nchi changa. China ni nchi changa na Afrika ni nchi changa, lakini wenzetu wako mbele kidogo, kwa hivyo nafikiri China wanataka wazivute nchi changa za Afrika zijiunge kwenye barabara ya maendeleo haraka.
CRI: Kutokana na uzoefu ulinaonao wa uhusiano kati ya Afrika na China, wewe unaona sasa hivi ni kweli China inafanya kazi za kuzivuta nchi za Afrika ziendelee au unaona bado kuna matatizo?
Hokororo: Wachina wanajitahidi, wanakuja sana kwenye nchi za Afrika, sisi nafikiri bado tuko nyuma kidogo, hatutaki kujifunza haraka kutoka wachina, au tunajifunza kidogo, lakini tungejifunza wao wanapigaje hatua za maendeleo, wao wanajengaje uchumi kuliko kukaa tu nyumbani. Tuseme kwamba wameendelea sana. Lakini tukiiga mfano wao, njia yao ya maendeleo, nafikiri sisi Afrika tutapiga hatua. Tukiiga uchapaji kazi wao, tulete watu wasome, warudi nyumbani, watusaidie kujenga uchumi wetu na mambo mengine.
CRI: Katika miaka ya karibuni wachina wametambua kwamba vyombo vya habari vya magharibi vinatoa picha isiyo sahihi ya China yenyewe na nchi za Afrika, kwa hiyo kuna juhudi za kujaribu kufanya ushirikiano kwenye mambo ya habari kati ya wachina na waafrika. Unaona kuna mafanikio yoyote ambayo inaweza kuonekana kwenye ushirikiano huu?
Hokororo: Mafanikio yanaonekana kidogo katika sekta hiyo kwa sababu kubwa ni kwamba, sisi nchi za Afrika bado tunawang'ang'ania wale wanaoitwa wakoloni waliotutawala, kwa hiyo utakuta tuna imani kubwa kwa mashirika yao ya magharibi yakitoa habari, ingawa wanatoa habari potofu kuhusu Afrika. Lakini wachina sasa wanajaribu kutusaidia, kutoa habari sahihi za kwao na za Afrika kwa sababu wenzetu wa nchi za Ulaya wanatafuta mabaya ya China na ya Afrika, wanayatangaza zaidi mabaya badala ya mema, na mazuri ambayo ni mengi yapo huku Afrika na pia hapa China hayatangazwi.
CRI?Sasa hivi vyombo vya habari vya Afrika vinaitangazaje China?
Hokororo: Inategemea, nchi nyingine kwa mfano Tanzania na Kenya zina uhusiano karibu na China, kwa hiyo watanzania na wakenya wengi wanaijua China kwa sababu tumekuwa tunashirikiana na China katika nyanja mbalimbali. Kwa mfano mradi wa reli ya TAZARA walitujengea wachina, tunakumbuka kuwa, walipoijenga TAZARA, nchi za magharibi ziliiita kuwa ni reli ya mianzi, haitadumu, au itadumu kwa miaka mitano tu, na italeta maafa vitu kama hivi. Lakini kwa mshangao wao, reli hiyo bado inafanya kazi mpaka sasa.
Mwandishi wa Habari: Unaonaje haki ya biashara kati ya China na Afrika, sasa hivi inaonekana kama China inauza sana bidhaa kwa Afrika, hali hii unaionaje?
Hokororo: Biashara ni ya pande mbili, isiwe ya upande mmoja. Sasa sisi Waafrika tunadhani kuwa, malighafi za Afrika zinakubalika kununuliwa na wachina, kama pamba, korosho na chai. China ina viwanda vingi vya kutengeneza bidhaa kamili, inaweza kutusaidia katika sekta hiyo, kwa mfano Tanzania ina matunda mengi ya machungwa na mananasi, lakini matunda mengi yanaoza, wakulima wanashindwa kujua wafanye nini, hatuna viwanda vya kutengeneza matunda hayo.
|