Bw. Wang Shuzeng ni mwandishi wa vitabu, na vitabu alivyoandika vinasomwa na watu wengi. Wakati Wachina wanapoadhimisha miaka 70 ya "Safari Ndefu ya Jeshi Jekundu" kitabu kiitwacho "Safari Ndefu" kilichoandikwa na Bw. Wang Shuzeng kwa miaka sita sasa kimechapishwa.
Bw. Wang Shuzeng ana umri wa miaka 54, ni mrefu na amekuwa mwanajeshi kwa zaidi ya miaka 30. Alianza kuandika vitabu alipokuwa na umri wa miaka 20, aliwahi kuchapisha riwaya nyingi, na moja ya tamthilia zake ilipata tuzo ya hayati Cao Yu, ambaye alikuwa mwandishi mashuhuri wa tamthilia nchini China. Katika miaka ya karibuni amejikita katika fasihi na ameandika kitabu kinachoitwa "Vita katika Korea ya Kaskazini" na kitabu kinachoitwa "Mwaka 1901" kinachoeleza uvamizi wa jeshi la muungano wa nchi nane za kibeberu za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Urusi, Japan, Italia na Austria ulioilazimisha serikali ya Enzi ya Qing kusaini "Mkataba wa Mwaka 1901" usio wa haki. Vitabu hivyo vinavyovutia vinasifiwa na wasomaji kuwa ni fasihi ya historia halisi.
Maisha ya kuwa mwanajeshi kwa miongo kadhaa yalimfanya Bw. Wang Shuzeng awe mtu wa wazi kabisa na kupuuza maslahi binafsi. Ili aweze kuandika kitabu cha "Safari Ndefu" kwa moyo wote alijiuzulu kazi yake ya uongozi na alijifungia ndani ya chumba cha kusomea kwa miaka sita kushughulika na uandishi wake. Alisema yeye hafai kuwa kiongozi, atakuwa askari tu na kuandika vitabu maishani mwake. Kutokana na sababu hiyo alijiunga tena na jeshi baada ya kuondoka jeshini kwa kuwa mkurugenzi wa uongozi wa Chuo Kikuu cha Fasihi ya Lu Xun kwa miaka mine. Alipozungumzia uhusiano kati ya mwanajeshi na mwandishi wa vitabu alisema,
"Maisha ya kuwa mwanajeshi yaliniwezesha kufika kila mahali nchini China na kuifahamu jamii, na maisha ya kuwa mwanajeshi yalinipatia uwezo wa kuvumilia hali ngumu bila kurudi nyuma."
Bw. Wang Shuzeng alisema ana mpango wa kuandika vitabu vya aina mbili, moja ni historia ya mapinduzi ya China ikiwa ni pamoja na "Vita vya Korea ya Kaskazini", "Safari Ndefu" na "Vita vya Ukombozi"; na aina nyingine ni vitabu vya historia ya zama za karibuni ikiwa ni pamoja na kitabu cha "Mwaka 1901" ambapo Vuguvugu la Wakulima la Yi He Tuan lilizuka na uvamizi ulifanywa na jeshi la muungano wa nchi nane za kibeberu dhidi ya China, kitabu kiitwacho "Mapinduzi ya Mwaka 1911" yaliyoongozwa na Sun Yatsea na kumaliza mfumo wa kimwinyi uliotawala China kwa zaidi ya miaka elfu mbili na kitabu cha "Mwaka 1921" ambapo Chama cha Kikomunisti cha China kilinzishwa. Alisema, vitabu hivyo vyote vinaandikwa kwa ajili ya vijana wa siku hizi, ili waifahamu historia ya China. Alisema,
"Vijana wetu hawafahamu sana historia ya taifa letu. Mambo ya zamani ya taifa yaliyokuwa ya furaha na ya huzuni lazima yawe kama mnara wa taa wa kuongoza safari ya taifa hilo. Vijana wetu wakiwa wanaishi katika mazingira yenye maisha ya starehe kwa vyovyote vile hawatakiwi kupoteza imani yao, China ni taifa lenye imani imara na nguvu kubwa ya uhai."
Bw. Wang Shuzeng alikuwa na tumaini hilo alipoandika kitabu chake cha "Safari Ndefu". Mwishoni mwa mwaka 2000 alipata kitabu kilichochapishwa na Shirika la "Times" la Marekani. Kitabu hicho kiliorodhesha matukio makubwa 100 yaliyoathiri historia ya binadamu tokea mwaka 1000 hadi mwaka 2000, na moja kati ya matukio hayo ni Safari Ndefu iliyofanywa na Jeshi Jekundu la China mwaka 1934. Anaona kwamba vijana hawalielewi sana tukio hilo lililotokea miaka 70 iliyopita. Aliwahi kujiuliza "Kuna tofauti gani kati ya watu wa China na watu wa magharibi katika kuielewa Safari Ndefu ya Jeshi Jekundu? Na katika miaka ya karibuni vijana wengi wa nchi za nje wanasafiri kwa kufuatia njia ya Safari Ndefu, je, vijana hao wenye hali nzuri ya kimaisha wanatafuta nini katika Safari Ndefu? Bw. Wang Shuzeng alisema,
"Naona vijana hao wanatafuta moyo fulani katika njia ya Safari Ndefu. Sababu ya watu wa nchi za magharibi kuorodhesha Safari Ndefu kwenye matukio makubwa 100 ni kuwa safari hiyo imeonesha moyo na nia thabiti isiyowahi kutokea katika historia ya binadamu, moyo usiolegalega, ambapo mmoja anaanguka mwingine anaendelea nao kwa ajili ya kutimiza imani yao, Safari Ndefu ni safari ya idadi kubwa ya watu ambayo haikuwahi kutokea katika historia ya binadamu na ni moyo wa binadamu wanaotaka kujiendeleza bila kusita, na ni moyo usiokubali kushindwa kamwe na kusonga mbele daima."
Bw. Wang Shuzeng alisema kwamba ili kukamilisha kitabu cha "Safari Ndefu" alisoma nyaraka nyingi zenye maneno milioni kumi kadhaa na aliandika habari zenye maneno milioni mbili kwenye daftari lake, na ramani ya Safari Ndefu karibu ilichanika kutokana na kutumiwa sana. Kwa kuwa mwandishi makini, kuandika kitabu hicho pia ni kama safari yake ndefu na ngumu.
Kitabu cha "Safari Ndefu" kimerekodi mambo mengi ambayo hayakujulikana hapo kabla, na kimeieleza historia kwa undani zaidi. Alisema wakati alipoandika kitabu hicho, pia ilikuwa ni miaka yake ya kuongeza ufahamu wake wa kina zaidi kuhusu Safari Ndefu. Hapo mwanzo aliifahamu Safari Ndefu kuwa ni nia na uvumilivu wa hali ngumu, lakini baadaye amefahamu kuwa safari hiyo ilifanywa kwa tumaini lililoshikiliwa na jeshi jekundu la China. Alisema, jeshi hilo liliundwa kwa sehemu mbili, moja ni sehemu ya watu hodari walioelimika kisiasa, na wengine ni watu maskini kutoka tabaka la chini la jamii ambao hawakujua kusoma wala kuandika, moyo wa kupambana na matatizo ya kila aina kwa ajili ya kukamilisha tumaini lao kutokana na muungano wa sehemu hizo mbili ni mkubwa na unawavutia watu. Alisema,
"Wakulima wa China walikuwa ni watu maskini kabisa duniani, walinyonywa na kukandamizwa na matabaka kadhaa, dhuluma waliyopata ilikuwa ni kubwa. Kwa hiyo jeshi jekundu lilipopita walikokuwa wanaishi watu hao, na waenezi siasa wa jeshi hilo waliwaambia 'Hamkuzaliwa kama ng'ombe na punda, bali ni binadamu sawa na wengine, na msitegemee mtu mwingine kuja kuwaokoa bali mfuate bendera ya jeshi jekundu na kufyeka dhuluma zote duniani', walikuwa na furaha na wakalifuata jeshi jekundu. Askari wengi walipokufa kwa ajili ya tumaini lao walikuwa hata hawakufahamu nini tofauti kati ya Marx mwenye sharafa ndefu na Lenin mwenye masharubu kwa sababu hawakujua kusoma. Lakini nina hakika ya kwamba wakati walipoanguka hawakujuta kutokana na tumaini lao."
Bw. Wang Shuzeng alisema, Safari Ndefu ni tukio kubwa la kihistoria linalowavutia watu, na mvuto huo unawafanya Wachina watafakari kuhusu mustakbali wa taifa lao.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-30
|