Shughuli za utalii kwenye sehemu za vijijini nchini China zilipiga hatua kubwa katika kipindi cha likizo ya siku ya taifa, tarehe 1 Oktoba. Mtaalam wa utafiti wa utalii wa sehemu ya vijijini maybe ambaye pia ni Profesa wa chuo cha elimu cha Guizhou Bw. Zhang Xiaosong alisema, maendeleo ya soko la utalii kwenye sehemu ya vijijini nchini China bado yako katika kipindi cha mwanzo, lakini soko hilo lina nafasi kubwa za uendelezaji na biashara katika siku za baadaye.
Mkurugenzi mkuu wa idara ya utalii ya taifa Bw. Shao Qiwei hivi karibuni alipofanya ukaguzi kuhusu utalii wa sehemu za vijijini mkoani Guizhou alidokeza kuwa, katika miaka ya karibuni, utalii wa sehemu za vijijini nchini China ulivutia watu wengi katika likizo tatu za "tarehe 1 Mei", "tarehe 1 Oktoba" na "siku kuu ya Spring", ambapo 70% ya wakazi wa mijini nchini China walichagua kufanya utalii kwenye sehemu za vijijini, na idadi ya watalii waliotembelea sehemu za vijijini katika kila likizo ilikuwa kiasi cha milioni 60.
Inakadiriwa kuwa hivi sasa zaidi ya watalii milioni 300 wanatembelea sehemu za vijijini nchini China kwa mwaka, na pato linalotokana na shughuli za utalii linazidi Yuan bilioni 40.
Bw. Zhang Xiaosong alisema kufanya utalii kwenye sehemu ya vijiji nchini China kulichelewa kuanza, ambako kulianza katikati na mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne ya 20 kwenye mikoa iliyoendelea ya pwani ya mashariki na miji ya sehemu za kati na magharibi za China, ambapo watalii walikwenda kuangalia mandhari ya sehemu ya vijiji na kujiburidisha kwa maisha ya wakulima katika nyakati za mapumziko. Katika miaka ya hivi karibuni, utalii wa sehemu za vijijini umeendelezwa kwenye sehemu mbalimbali nchini na kuongezwa matembezi kwenye majengo na tarafa maarufu za zamani.
Katika miaka ya karibuni utalii kwenye sehemu ya vijiji umechukuliwa kuwa moja ya mbinu muhimu ya kuongeza pato la wakulima. Hivi sasa sehemu ya vijiji nchini China imekuwa na hoteli za wageni zaidi ya 320 zenye vitanda laki 1.3, ambazo zinaweza kuwapokea watalii zaidi ya elfu kumi kwa wakati mmoja.
Sehemu za majaribio ya utalii wa kilimo zilizoanzishwa nchini China kutokana na mapendekezo ya idara ya utalii ya taifa zimefikia 359, ambazo ziko katika mikoa 31 kuhusu shughuli za kilimo, misitu, uchungaji wa mifugo malishoni, kazi za kiuchumi, uvuvi na kazi za usindikaji wa mazao ya kilimo.
Mratibu wa shirika la utalii wa kimataifa la Umoja wa Mataifa Bw. Francisco pia anavutiwa na soko la utalii wa sehemu za vijijini la China, alisema "bila kujali sekta ya utalii ya China itakuwa imepata maendeleo kwa kiwango gani ifikapo mwaka 2020, watalii wa nchini China na wa kutoka nchi za nje, watakuwa hawafikirii tu kuchagua miji ya Beijing, Shanghai, Guangzhou, Xian na Guilin
Mkurugenzi wa idara ya utalii ya serikali ya China Bw. Shao Qiwei alisema, 70% ya rasilimali za utalii za China ziko kwenye sehemu ya vijiji, soko hilo lina uwezo mkubwa wa kuendelezwa katika siku za baadaye, lakini hivi sasa kiwango cha maendeleo ya utalii kwenye sehemu ya vijiji kiko katika kipindi cha mwanzo tu kutokana na hali hafifu ya mawasiliano na miundo-mbinu.
Mkurugenzi wa idara ya utalii ya mkoa wa Guizhou Bw. Yang Shengming alisema, hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, mkoa wa Guizhou umekamilisha mpango wa kwanza wa utalii wa sehemu za vijijini, hivi sasa wanafanya uchunguzi na utafiti kuhusu sera za sekta ya utalii za kuvutia uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka sehemu za nje.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-30
|