Wakati inapokaribia kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, nchi nyingi za Afrika zinatilia maanani kupata uzoefu kutoka kwa China zikiwa na nia ya kupanua ushirikiano na China katika shughuli za uwekezaji na teknolojia.
Balozi wa Gabon nchini China Bw. Emmanuel Mba Allo hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China, alisema "Tunakaribisha viwanda na kampuni za China kuwekeza barani Afrika, kujenga viwanda vya ubia na kutusaidia kuongeza thamani ya bidhaa zetu. Pia tunataka China iongeze nguvu katika kuiuzia Afrika teknolojia husika, kwa kufanya hivyo ndipo China itakapoweza kuziasaidia nchi za Afrika kuondokana na hali ya kuwa nyuma ya kimaendeleo."
Balozi wa Jamhuri ya Kongo Bw. Pierre Passi alisema anatumai kuwa kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika hapa Beijing, kutasaidia kuwahamasisha wanaviwanda wa China kuwekeza vitega uchumi moja kwa moja barani Afrika, kuhimiza ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta mbalimbali muhimu, zikiwemo ujenzi wa miundo mbinu, nishati, mawasiliano na posta, pamoja na kilimo. Na Balozi wa Senegal nchini China Bw Papa Khalilou Fall alieleza kuwa, ni jambo lenye umuhimu sana kwa Afrika kupata teknolojia kutoka kwa China.
Katika miaka ya hivi karibuni kwa ujumla hali ya Afrika imekuwa ikielekea kutulia, uchumi wake unaendelezwa kwa hatua madhubuti, na vitega uchumi vinavyowekezwa barani Afrika pia vinaongezeka kwa asilimia 4 hadi 6 kwa mwaka. Nchi nyingi za Afrika zinataka kujikwamua kutoka kwenye hali ya uchumi kutegemea bidhaa kadhaa tu, bali zina nia kubwa ya kupata maendeleo katika sekta zote.
Neno la "kunufaishana" ni neno linalotajwa mara kwa mara na mabalozi wa nchi za Afrika nchini China wakizungumzia masuala yanayohusu ushirikiano kati ya China na Afrika. Balozi wa Senegal nchini China Bw Fall alisema, "Tunataka China ifungue sekta mpya kwa nchi za Afrika ili tufanye ushirikiano, na kwa upande wa nchi za Afrika, pia zinatakiwa kufungua soko la ndani kwa China."
Na balozi wa Gabon nchini China Bw Mba Allo alisema hivi sasa viwanda vingi vya China vimeanzisha shughuli zao nchini Gabon. Alisema nchi yake inapenda kuvutia viwanda na kampuni nyingi zenye nguvu na uaminifu za China kuwekeza kwenye shughuli zote za kiuchumi.
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya biashara ya China zinaonesha kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005 Afrika ilikuwa imevutia vitega uchumi vya China vyenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 6, ambapo kampuni za China zilianzisha viwanda zaidi ya 800 barani Afrika. Serikali ya China ilisaini mikataba ya kulinda uwekezaji na nchi 28 za Afrika, aidha China na nchi 8 za Afrika zilisaini mikataba ya kuepusha kutoza ushuru wa forodha kwa mara mbili kwa bidhaa. Kwa mujibu wa makadirio ya wizara ya biashara ya China, thamani ya biashara kati ya China na Afrika itazidi dola za kimarekani bilioni 50 mwaka huu, hivyo kuleta ongezeko la kasi kwa miaka mitano mfululizo.
Mabalozi wa nchi za Afrika nchini China wameeleza kuwa, uchumi wa China na Afrika una sifa za kusaidiana, kuna fursa nyingi ambazo bado hazijatumika katika ushirikiano wa pande hizo mbili. Wamekadiria kuwa katika kipindi cha miaka mitano hadi minane ijayo viwanda vya China vitakwenda barani Afrika kuwekeza zaidi vitega uchumi.
Idhaa ya Kiswahili 2006-11-01
|