Chama cha Msalaba Mwekundu kikiwa chama cha kutoa msaada kwa jamii, siku zote kinashughulikia kazi za kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa na kufanya uokoaji wa kibinadamu. Chama cha Msalaba Mwekundu kilianzishwa nchini China mwaka 1904, hivi sasa kina matawi 31 katika ngazi ya mikoa na matawi mengine mawili katika mikoa ya utawala maalum ya Hong Kong na Macao. Aidha Chama cha Msalaba Mwekundu cha China kina vitengo zaidi ya elfu 70.
Katika mji mdogo wa Jinshang uliko mjini Shishi mkoani Fujian, kuna kitengo cha Chama cha Msalaba Mwekundu kilichoanzishwa na raia wa kawaida ambao wana hamu kubwa ya kushiriki kwenye shughuli za hisani. Kitengo hicho kinafanya shughuli za hisani kwa kukusanya fedha na vitu vya raia, na kimepata uaminifu na uungaji mkono wa raia.
Mji wa Jinshang ni mji mdogo ulioko karibu na bahari wenye wakazi wasiozidi elfu 10, lakini jamaa zao wanaoishi katika nchi za nje ni zaidi ya elfu 10. Wastani wa mapato ya kila mtu mjini humo kwa mwaka ni Yuan elfu 8. Lakini katika mji huo tajiri, bado kuna watu kadhaa wanakumbwa na matatizo na kuhitaji msaada kutokana na kuwa wagonjwa au kukumbwa na maafa.
Siku moja mnamo mwaka 1999 meneja wa duka la uchapishaji Bw. Wu Qichang alisikitishwa na jambo moja. Mwanakijiji mmoja maskini alimwomba kumwandikia barua jamaa yake anayeishi nchini Philippines na kuomba msaada ili mama yake apate matibabu. Baadaye Bw. Wu alijua kuwa mwanakijiji huyu ni maskini sana hata hana pesa ya kununulia taa ya mafuta. Hivyo Bw. Wu aliamua kuanzisha mfuko wa kutoa msaada.
"Nimewahi kukutana na wazee wengi, waliniomba niwaandikie barua jamaa zao wanaoishi nchini Philippines na mkoani Hong Kong, ili kuomba pesa chache na kutatua matatizo ya kiuchumi. Baadhi yao walipata magonjwa au kukumbwa na maafa. Wakati huo niligundua kuwa katika sehemu zilizoendelea kiuchumi, bado kuna watu maskini wanaohitaji msaada kutoka kwa watu wengine."
Mawazo ya Bw. Wu Qichang ni sawa na ya askari mstaafu Bw. Qiu Yushang. Kutokana na juhudi zao za pamoja tarehe 17 mwezi Januari mwaka 2001, kitengo cha Chama cha Msalaba Mwekundu mjini Jinshang kilianzishwa rasmi, na baada ya muda fulani kitengo hicho kilifanya mambo kadhaa yanayowastaajabisha wanavijiji wa huko.
Mjini humo kuna mtoto mmoja anayeitwa Qiu Yuyu. Kwenye ukaguzi wa afya shuleni alipokuwa na umri wa miaka 7, aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa moyo. Lakini kutokana na umaskini, mtoto huyo hakutibiwi kwa muda mrefu.
Baada ya kujua jambo hilo, Bw. Qiu Yushang, Bw. Wu Qichang na watu wengine walitembelea nyumba ya Qiu Yuyu. Mtoto huyo dhaifu alikuwa amelala kitandani, na wazazi wake walilia kando ya kitanda. Baada ya kuondoka nyumba kwake, watu wote walisema ni lazima wafikiri njia ya kumsaidia mtoto huyo ili atibiwe. Siku hiyo jioni kitengo cha Chama cha Msalaba Mwekundu cha mji wa Jinshang kilifanya mkutano wa dharura wa makatibu. Baada ya kujua hali ya Qiu Yuyu, makatibu zaidi ya 30 wanaotoka kwenye vijiji mbalimbali walitoa pesa zao. Baadaye walitoa mwito wakitaka wajumbe wa Chama cha Msalaba Mwekundu na wanavijiji kutoa mchango wao. Kutokana na juhudi zao walikusanya Yuan laki 1.3.
Mwishowe Qiu Yuyu alilazwa katika hospitali kuu ya jeshi ya Fuzhou. Baada ya miezi minne Qiu Yuyu alipoa na kurudi shuleni.
Mwandishi wa habari alipokwenda kwenye shule ya msingi ya Qiongshan, alimwona Qiu Yuyu na wenzake wakicheza pamoja kwa furaha. Qiu Yuyu alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wakati alipokuwa darasa la tatu aliumwa na hata hakuweza kutembea. Daktari alimwambia ni lazima akatibiwe kwenye hospitali kubwa. Kutibiwa kwenye hospitali kubwa kulihitaji Yuan laki 1.1, lakini familia yake haikuwa na pesa za kutosha. Sasa baada ya kurudi shuleni anaona furaha kubwa. Na alisema baada ya kuwa mtu mzima, atatoa hisani kama watu waliomsaidia, na kuwasaidia watu wengine wanaohitaji msaada.
Mtoto wa kike wenye umri wa miaka 6 Qiu Yunying alikuwa na vivumbe wa aina zaidi ya kumi mwilini mwake, aliumwa hata hakuweza kulala kwa siku nzima. Bw. Qiu Yushang na wenzake walikusanya pesa hapa na pale ili kumsaidia Qiu Yunying kupata matibabu hospitalini. Bw. Qiu alisema,
"familia ya Mtoto Yunying haikuwa na pesa za kutosha kumpeleka hospitali kufanyiwa operesheni. Mkuu wa kijiji aliomba Chama cha Msalaba Mwekundu kumsaidia. Tulifanya mkutano wa makatibu, makatibu walitoa Yuan elfu 3 hadi elfu 4, lakini pesa hizo hazikutosha, hivyo tulitoa mwito kwa jamii ili itoe msaada. Kwa ujumla tulikusanya Yuan laki 1 elfu 10 na mia 5.
Qiu Yunying alilazwa hospitalini na kufanyiwa operesheni, vivimbe viliomsumbua kwa miaka minne viliondolewa. Mama yake alisema baada ya operesheni mtoto wake anaweza kulala na kwenda shuleni. Anakishukuru sana Chama cha Msalaba Mwekundu kwa ufuatiliaji na msaada wao. Tangu mwaka 2001, kitengo cha Chama cha Msalaba Mwekundu cha mji wa Jinshang kimechangisha Yuan laki 4, kutoa msaada kwa zaidi ya mara 30, na kuwanufaisha watu zaidi ya 3000.
Kutokana na maendeleo ya kazi, wanachama wa kitengo cha Chama cha Msalaba Mwekundu cha mji wa Jishang wameongezeka kuwa watu 212 kutoka 37 wakati kilipoanzishwa. Wanachama wameenea katika vijiji 10 mjini humo, pia kuna wanachama katika vijiji na miji iliyo karibu na mji huo. Baadhi yao ni wakulima, mameneja wa makampuni ya watu binafsi, vibarua, matajiri na watu wasio na pesa nyingi. Lakini wote wanajiunga na Chama cha Msalaba Mwekundu ili kutoa mchango wao. Mwanachama mmoja ambaye ni meneja wa kampuni binafsi Bw. Cai Shengli alisema,
"Uwezo wa mtu mmoja ni mdogo, ni lazima tukusanye nguvu za watu wote, ndipo tutaweza kutoa mchango kwa jamii, na tutaweza kutatua matatizo kwa kutegemea Chama cha Msalaba Mwekundu."
Hivi sasa kitengo hicho cha Chama cha Msalaba Mwekundu kinafanya mkutano wa wanachama kila baada ya muda kadhaa na kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za Chama cha Msalaba Mwekundu. Wanachama wote wanatoa mchango bila kusita.
|