Katika siku za joto mwaka huu, jiji la Chongqing lililopo kusini magharibi mwa China lilikumbwa na maafa makubwa ya ukame ambayo hayakutokea katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, ambapo wakazi na mifugo walikosa maji safi ya kunywa, mimea ya kilimo iliharibika sana na moto ulitokea misituni mara kwa mara. Lakini wakazi wa Chongqing walinusurika katika maafa hayo kwa kutumia mbinu mbalimbali na kufanya bidii kubwa.
Kijiji cha Shiqiao ni moja kati ya vijiji vilivyoathiriwa vibaya na ukame, kiasi kwamba vyanzo vya maji ya kunywa vilikauka. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alikitembelea kijiji hicho. Aliona kuwa wakazi wa huko sasa wana maji safi ya kunywa yanayopatikana kwenye visima. Mkazi wa kijiji hicho Bw. Wan Liding alielezea furaha akisema, "Hivi sasa tuna visima vinavyotoa maji ya kutosha ya kukidhi mahitaji yetu, hata kama ukame utatokea tena katika siku za baadaye hatutakuwa na wasiwasi. Tulichonga maneno kando ya visima yasemayo, ukinywa maji usisahau wachimba visima wala chama cha kikomunisti. Tunaishukuru serikali, bila misaada ya chama na serikali tusingeweza kukamilisha uchimbaji wa visima kwa kutegemea nguvu zetu pekee."
Bwana huyo alimwambia mwandishi wa habari kuwa, tangu tarehe 18 Julai mwaka huu mto Liujia uliopo huko karibu ulikauka, mto huo ulikuwa ni chanzo cha maji wanachotegemea wakazi wa huko, wanakijiji wapatao 3,700 na mifugo zaidi ya 1,600 ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji. Alisema "Katika kipindi kibaya kabisa, watu wa familia moja walikuwa wakichangia maji kunawa nyuso, mimi sikuoga kwa wiki moja mfululizo. Kulikuwa hakuna maji ya kumwagilia mboga, kwa hiyo mimea mingi ilikufa kutokana na ukame."
Meya wa jiji la Chongqing Bw. Wang Hongju alifafanua akisema "Wakati huo hali joto kali ilifikia centigrade 44.5, theluthi mbili ya mito ilikauka, mashamba yenye hekta zaidi ya milioni 1.3 na watu milioni 21 waliathiriwa na ukame, na hasara za moja kwa moja zilifikia Yuan bilioni 9.07."
Katika kukabiliana na ukame, serikali ya mji wa Chongqing iliamua jambo muhimu la kwanza ni kuhakikisha wakazi wanapata maji safi ya kunywa, kwa hiyo ilitumia malori mengi kupeleka maji kwenye sehemu zilizoathiriwa na upungufu wa maji. Wananchi pia walijitolea kuunda makundi mbalimbali ya kutafuta vyanzo vipya vya maji.
Katika kijiji cha Shiqiao, wakazi walifanikiwa kupata chanzo cha maji baada ya jitihada za siku 5 mfululizo. Baada ya serikali ya huko kupata habari hiyo, ilituma mafundi na mashine kusaidia kazi ya uchimbaji wa kisima. Naibu mkuu wa kata Bi. Li Shilan alisema "Tuliwatuma mafundi kuwafundisha njia sahihi ya kuchimba kisima, pia tuliwapa misaada ya vitu na zana mbalimbali zinazotumika katika uchimbaji kama vile saruji, mitambo ya kuvuta maji, ili kuhakikisha njia sahihi ya kuvuta maji na wakazi wanaweza kunywa maji safi."
Ujoto mkali na ukame mkubwa ulikuwa ni kama mtihani kwa wakazi wote wa Chongqing. Wilaya ya Bishan ipo kwenye sehemu ya magharibi ya Chongqing, mkuu wa kijiji cha Longan hapa wilayani Bw. Mao Deli alikuwa akitembelea kati ya vituo zaidi ya 20 vya kusambaza maji kila siku, alikuwa anarudi mwenye maskani yake kwa mara chache sana. Mke wake alikuwa alimlalamikia, lakini bwana huyo alisema "Mimi ni mwanachama wa chama cha kikomunisti cha China, pia ni kada mmoja wa kijiji, kwa hiyo ni wajibu na kazi yangu ya kuwasaidia wananchi kuondoa taabu zinazowasumbua."
Ujoto mkali ulikuwa unasababisha kuzuka kwa moto misituni mara kwa mara. Polisi wa misitu, askari polisi na askari wa zima moto walikuwa wakishika zamu kwenye mstari wa kwanza. Bw. Ren Shihong ni kiongozi wa ofisi ya uongozi ya kinga ya moto misituni ya eneo la Yubei la Chongqing. Aliwahi kufanya kazi kwenye mstari wa kwanza wa kuzima moto kwa siku 3 mfululizo. Wakati akikabiliana na moto, alikiri kuwa aliona hofu kama ilivyo kwa watu wa kawaida. Alisema "Hofu? Ndiyo, niliona hofu, mimi ni mtu kama watu wengine. Lakini kama tungeshindwa kuzima moto, basi maisha ya wenzangu na mali zao zingeweza kuunguzwa na moto. Nikiwa mkuu wa kikosi cha zima moto, kama nisingetoa mfano wa kuchapa kazi, wengine wasingefuatana nami katika kuzima moto."
Katika kukabiliana na ujoto na ukame uliokuwa unaendelea, wafanyakazi wengine wa sekta ya kutoa huduma za umeme, gesi, mawasiliano na tiba pia walikuwa wanashika zamu zao. Mbali na hayo watu wa China wa sehemu nyingine pia walitoa misaada kwa wakazi wa Chongqing. Hadi kufikia tarehe 11 Oktoba mwaka huu, walikuwa wamechangisha fedha za Renminbi Yuan milioni 130 kwa ajili ya kuisaidia Chongqing katika mapambano dhidi ya ukame. Zaidi ya hayo wakazi wa Chongqing walipata maji safi ya kunywa yaliyosafirishwa kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Kutokana na juhudi hizo, wakazi wa Chongqing wamepata ushindi katika mapambano dhidi ya ukame, ambapo kulikuwa hakuna mtu hata mmoja aliyekufa kutokana na kukosa maji au chakula. Hivi sasa ukame umepita na msimu wa masika umekuja. Mvua zinanyesha mara kwa mara, na maji ya mvua yanaingia mitoni, mashambani na pembezoni mwa jiji la Chongqing.
Idhaa ya kiswahili 2006-11-09
|