Wakati mkutano wa viongozi wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ulipokaribia kufanyika, tarehe 25 wasanii kutoka nchi tano za Afrika walifanya maonesho ya michezo ya sanaa mjini Beijing. Katika miaka 50 iliyopita tokea uhusiano wa kibalozi kati ya China na Afrika uanzishwe, maingiliano ya kiutamaduni kati ya pande mbili hizo yanazidi kupamba moto na hasa katika miaka ya karibuni.
Mliyosikia ni sauti iliyosikika wakati michezo ya sanaa ilipooneshwa na wasanii wa Kundi la Umkhonto kutoka Afrika Kusini, watazamaji walifurahia jinsi wasanii hao walivyocheza kwa nguvu. Baada ya mchezo kumalizika mtazamaji mmoja alimwambia mwandishi wa habari akisema,
"Mchezo wao umegusa hisia zangu kwa nguvu, nashangaa uhodari wao wa kucheza, kwangu ni mara ya kwanza kabisa kuona ngoma kama hiyo. Safi sana!" Mtazamaji mwingine alisema,
"Maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika yametuwezesha kufahamu utamaduni wa Afrika ulivyo. Michezo yao inaonesha maisha yao moja kwa moja, ni mchezo unaotokana na maisha halisi, na wala sio ya kubuniwa."
Licha ya michezo ya kutoka Misri, Afrika Kusini, Mauritius, Gabon na Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, pia yalikuwepo maonesho ya vitu vya sanaa za mikono katika Jumba la Makumbusho la Taifa ambayo yanaonesha vitu adimu kutoka zaidi ya nchi 20 za Afrika, vikiwemo vinyago, picha za Tingatinga, vitu vya kusukwa na vyombo vya kauri zaidi 300. Watazamaji wamepata fursa ya kufurahia sanaa halisi za Kiafrika nyumbani kwao.
Ingawa China na Afrika kijiografia ziko mbali, lakini katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kutokana na juhudi za pande mbili maingiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika yanaimarika mwaka hadi mwaka. Hadi sasa mikataba ya utamaduni kati ya China na Afrika imefikia 156, vikundi vya utamaduni 230 vimetumwa na serikali ya China barani Afrika kufanya maonesho na makundi ya wasanii yamekuwa karibu 300. Licha ya hayo, pande mbili zinafanyiana maonesho ya utamaduni na sanaa, na kuwa na ushirikiano katika sekta za vitabu, ushapishaji wa habari, uandishi wa habari, matangazo ya redio, filamu, televisheni, utafiti wa vitu vya kale na kutoa mafunzo kwa watu wenye ujuzi.
Naibu meneja mkuu wa Kituo cha China cha Kufanya Maonesho katika Nchi za Nje Bw. Wan Jiyuan aliwahi kuandaa maonesho katika nchi za Afrika kwa mara nyingi na kuleta maonesho ya Afrika nchini China. Alisema,
"Kuna maingiliano mengi ya kiutamaduni kati ya China na Afrika. Tumeiwahi kutuma makundi mengi ya michezo ya sanaa barani Afrika, na pia tumewahi kuleta maonesho mengi ya vitu vya sanaa vya Afrika na ngoma za Afrika nchini China, maonesho hayo yanawavutia sana Wachina.."
Mwaka 1997 profesa Yue Yu alitumwa na serikali ya China kufundisha uchoraji nchini Eritrea, katika muda wa mwaka mmoja na nusu alikuwa na urafiki mkubwa na wanafunzi wa huko. Baada ya kurudi nyumbani China, kwa msukumo mkubwa alichora picha moja yenye kimo cha mita mbili kwa kalamu, aliipatia picha hiyo jina la "Maskani ya Disco". Hiyo ni picha kubwa kabisa duniani kati ya picha zilizochorwa kwa kalamu. Alisema,
"Sababu ya mimi kuchora picha hiyo ni kuwa, mimi na wanafunzi tulikuwa na urafiki mkubwa. Nilipoondoka, wanafunzi walilia na mimi nililia. Urafiki wetu naukumbuka daima, nilitumia nusu mwaka kwa kuchora picha hiyo. Kwenye picha nilichora mchunga ng'ombe anayecheza ngoma akiwa ng'ombe wake pembeni. Kwa kweli sikuchora picha hiyo kwa kalamu bali kwa hisia zangu."
Baada ya kuingia karne mpya, uhusiano wa kiutamaduni kati ya China na Afrika umepiga hatua kubwa. Ofisa mmoja wa utamaduni wa China Bw. Xie Fei alipozungumza na waandishi wa habari alisema,
"Maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika yanaendelea bila kusita, hasa miaka kadhaa baada ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika kuanzishwa, ambapo maingiliano yamekuwa mengi ambayo kwa wastani makundi ya wasanii kutoka pande mbili yanaongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko zamani, na mengi ni ya serikali, nyanja za maingiliano ya kiutamaduni zimepanuka. Kwa mfano, utafiti wa vitu vya kale ambao zamani haukuwepo umeanza, na mafunzo ya kitaalamu ya usimamizi na utunzaji wa vitu vya kale pia yanatolewa.
Imefahamika kwamba hivi sasa China imeanzisha vituo sita vya utamaduni katika nchi za nje, kati ya vituo hivyo vituo tatu viko mjini Misri, Benin na Mauritius. Vituo hivyo vimekuwa jukwaa la mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Afrika kwa kufanya semina, maonesho ya michezo ya sanaa na maonesho ya aina mbalimbali kuhusu utamaduni.
Bw. Xie Fei ana uhakika kwamba baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, uhusiano kati ya pande mbili utakuwa mzuri zaidi katika pande zote ikiwa ni pamoja na maingiliano ya kiutamaduni.
Idhaa ya kiswahili 2006-11-13
|