Katika karne mpya, kutokana na kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ushirikiano wa sekta za utamaduni na elimu unaendelea kupanuliwa, hivi sasa makubaliano ya mawasiliano na ushirikiano wa elimu yaliyosainiwa kati ya China na Afrika yanatekelezwa, na wanafunzi wa Afrika wanaosoma nchini China wanaongezeka mwaka hadi mwaka.
Mwanafunzi wa Tanzania Morris Hiji anasoma shahada ya pili ya uhandisi wa madawa katika Chuo Kikuu cha Kemia cha Beijing, yeye ni mmoja wa wanafunzi wanaonufaika na ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika. Alisema,
"Nimekuja China kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na China. Kwa Kweli kusoma China ni mahali pazuri, kwa sababu uchumi wake unakimbia sana."
Mwanafunzi mwingine wa Chuo Kikuu cha Kemia cha Beijing Thomas Odhiambo kutoka Kenya hivi sasa anasoma shahada ya tatu ya kozi ya mazingira. Yeye pia ni mwanafunzi anayenufaika kutokana na ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika. Anaridhika na mazingira ya masomo nchini China, alisema,
"Mimi vilevile nimekuja China kutokana na uhusiano kati ya Kenya na China. Kila mwaka kuna wanafunzi kumi kutoka Kenya wanafika hapa China. Nilipata fursa hiyo kutokana na bidii yangu kule Kenya. Sasa China inakimbia sana kiuchumi, China imefungua vyuo vikuu, wanafunzi wengi kutoka Afrika wanasoma nchini China kwa pesa zao binafsi. Wanafunzi wengi wanakwenda India na Russia kwa masomo, lakini wamesahau kuna masomo mazuri hapa China, bei ya masomo hapa ni bei nafuu."
Kwa wanafunzi wa Afrika wanaosoma nchini China, kabla ya kuanza masomo, kwanza ni lazima wajifunze Kichina, kwani wanahitaji kujifunza masomo sawa na wanafunzi wa China. lakini kujifunza kichina hakukuwa tatizo kubwa kwa wanafunzi hao ambao hawajatumia Kichina hata kidogo. Baada ya kujifunza masomo ya kichina kwa mwaka mmoja, kimsingi wanaweza kuzungumza na watu wengine kwa Kichina kwa urahisi. Mwanafunzi wa Tanzania anayejifunza udaktari kwenye Chuo Kikuu cha Beijing Alfred Nguma alisema,
"Tulisoma kichina kwa mwaka mmoja tu. Kichina cha kawaida baada ya mwaka mmoja tunaweza kuelewa vizuri. Kutokana na kuwa tulipokuja hapa Chuo Kikuu cha udaktari tulikuwa hatujafundishwa na Kichina cha udaktari, kwa hiyo ni ngumu. Lakini katika mwaka wa pili hakukuwa matatizo."
Hivyo wanafunzi wa Afrika wote wanaona kuwa, ingawa Kichina ni kigumu, lakini wakijifunza kwa bidii, bila shaka watafanikiwa. Katika miaka kadhaa ya kuishi nchini China, wanafunzi wa Afrika wanavutiwa na mambo mengi kuhusu China. Morris alipolinganisha mambo alivyoyajua kuhusu China kabla ya kuja hapa China na hali halisi aliyoikuta, alisema,
"Vyombo vya habari vya nchi za magharibi havisemi ukweli kuhusu China. China hivi sasa inakimbia, ongezeko la GDP ni karibu asilimia 10, uchumi wa China ni nzuri. Bidhaa nyingi zinatengenezwa nchini China, hata zinauzwa Ulaya na Marekani. Kwa hivyo ilivyotangazwa na nchi za magharibi kuhusu China si hali halisi ya China. China inafanya vizuri sasa."
Thomas pia aliyasifu maendeleo ya China, na kuwashukuru wananchi wa China kwa urafiki wao na Waafrika. Alisema,
"China ina mambo mengi yanayonivutia. Naona wachina ni wenye hesima. Halafu wanchina wanapenda kazi, wanatupia macho siku za mbele. Nilifika hapa mwaka 2003, Beijing ya mwaka 2003 na Beijing ya sasa ni tofauti sana. Inanivutia sana kuwa wanafanya kazi kwa bidii sana."
Alfred ambaye ameishi nchini China kwa miaka mitano anavutiwa na mandhari ya miji mbalimbali nchini China. Aliwahi kutembea sehemu nyingi nchini China, ikiwemo miji kadhaa mikoani Shandong na Shanxi, mji wa Dalian na mji wa Nanning. Alisema miji mikuu ya mikoa iliyoko kaskazini mwa China inapata maendeleo mazuri, na haina tofauti kubwa na Beijing. Na alipotaja mandhari nzuri ya mkoa wa Hainan, alisema,
"Mkoa wa Hainan ni mzuri sana. Uko pwani na unapendeza sana. Na ile mandhari inafanana sana na mandhari ya Dar es Salaam. Baada ya kukaa China kwa miaka mitano, nikakumbuka sana nyumbani, kutokana na mandhari niliyoiona kule."
Wanafunzi hao wanaridhika na maisha yao nchini China, wana marafiki wengi wa China, ambao wanawasaidia sana katika maisha na masomo yao. Morris alisema yeye na marafiki yake wanajifunzana na kusaidiana. Mazingira mazuri ya kujifunza nchini China yamewatia moyo wanafunzi hao, wote walisema watatoa mchango kwa maendeleo ya Afrika kwa ujuzi ambao wanajifunza nchini China. Morris alisema,
"Nitafanya kazi nchini Tanzania, nataka kuijenga nchi yangu, hivi sasa nasoma uhandisi wa madawa, kwa hiyo nafikiri nitakaporudi Tanzania, nitatoa mchango kwa uchumi na maendeleo ya nchi yangu."
Thomas Odhiambo ambaye kabla ya kuja China alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu cha Moi, Kenya alisema,
"Kabla ya kuja China nilikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi, kule Eldoret, nchini Kenya. Baada ya kumaliza masomo yangu, nitarudi kule Chuo Kikuu cha Moi, nitaendelea kuwa mhadhiri. Nimesomea mazingira hapa, nikirudi kule naweza kuisaidia Kenya kuboresha mazingira."
Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika limefanyika nchini China. Wanafunzi hao wanapozungumzia uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika wote wana imani kubwa kuhusu ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya pande hizo mbili. Thomas alisema,
"Uhusiano kati ya China na Afrika unapata maendeleo mazuri. Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika linaweza kuendeleza uhusiano huo. Afrika inategemea sana Ulaya, naona Waafrika wangejaribu kubadilisha uelekeo wao, wangekuja China. China ina viwanda vingi kule Afrika. Waafrika wanaweza kujifunza kutoka kwa China."
Idhaa ya Kiswahili 2006-11-15
|