Panda ni aina ya wanyama adimu wanaoishi nchini China, kwa hiyo wanajulikana kama tunu la taifa la China. Huko Fuzhou, mji wa pwani uliopo kusini mashariki mwa China, kuna panda mmoja maarufu, anayeitwa Basi. Basi ana umri wa miaka 26, kwa mujibu wa wanasayansi mwaka mmoja wa panda unalingana na miaka minne ya binadamu, kwa hivyo hivi sasa umri wa Basi unalingana na mzee mwenye umri wa miaka zaidi ya 100.
Mzee Basi ana umbo mzuri, nywele safi, siku zote anaonekana kama ni mweye heshima zaidi. Siku hiyo alitembelewa na mgeni Mama Li Xingyu ambaye aliwahi kumwokoa maisha ya Basi. Mama huyo alikuwa akimsalimia "Basi, mama amekuja kukuona, hujambo? Njoo kula. Unaona, jamaa kutoka maskani amekuja kukutembelea."
Ingawa miaka zaidi ya 20 imeshapita, mama Li Xingyu bado anakumbuka siku ambayo alimkuta panda huyo na jinsi alivyomwokoa. Siku moja katika mwezi wa Februari, mwaka 1984 mama Li Xingyu na mpwa wake walikuwa wakipanda mbegu za mboga kando ya mto, wakivutiwa na kitu chenye rangi ya nyeupe na nyeusi kilichokuwa kinaelea mtoni, kumbe ni panda mmoja. Walimkimbilia na kumchukua panda huyo kwenye mashamba ya mboga, wakiwasha moto na kumzungusha kwa kutumia nguo zao nzito ili panda apate ujoto. Baada ya saa tatu hivi, panda alirudishwa ufahamu hatua kwa hatua. Mama Li alichukua uji wa mahindi kumlisha panda. Panda akila akashiba na kurudishwa nguvu, akapanda juu ya mti mmoja na kubaki pale pale. Wanakijiji wengine na kada wa serikali ya kata wakipata habari hiyo walikuja, ili panda asiumie na baridi wakati wa usiku, waliwasha moto karibu na mti na kumlinda panda usiku kucha.
Siku ya pili walimpeleka panda kwenda kwenye eneo la hifadhi lililopo umbali wa kilomita 40. Kwa vile mahala alipoelea panda huyo panaitwa Mto wa Basi, mwaka huu ulikuwa mwaka wa 84, ambao kwa Kichina pia unaitwa mwaka wa "Basi", panda huyo alipewa jina la
Basi. Baada ya kupimwa afya, ilifahamika kuwa panda Basi alikuwa na umri wa miaka minne wakati huo huo.
Mwaka 1985 Basi alipelekwa hadi kituo cha utafiti wa panda kilichopo mjini Fuzhou, kituo hicho sasa ni maskani yake, ambapo panda Basi alitunzwa vizuri na watafiti wa kituo hicho na madaktari na wauguzi wa hospitali moja ya jeshi iliyopo huko Fuzhou. Alipata nafuu kwa haraka. Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Chen Yucun alisema "Panda Basi alipotakiwa kupimwa afya au akiugua kwa dharura, mkuu wa hospitali hiyo ya jeshi alisema, hamna matatizo toa agizo lako tu. Kupima afya kwa panda kunahitaji kuwashirikisha wakurugenzi wa vitengo 7 hadi vinane vya hospitali, ambao wanatakiwa kuacha kazi walizo nazo na kumhudumia panda, kila mara inachukua saa 5 hadi 6, na wanatoa huduma hizo za tiba bila malipo."
Pande huyo alijifunza michezo mbalimbali kama vile kucheza mpira wa kikapu na kunyanyua uzito, pia alijua kuiga mfano wa binadamu kupiga simu. Hatua kwa hatua panda huyo alianza kufahamika kwa watu wengi. Mwaka 1987 alikwenda Marekani na kufanya matembezi ya nusu mwaka, katika kipindi hicho aliwavutia Wamarekani wengi. Mwaka 1990 panda Basi alishiriki kwenye maonesho ya sanaa ya michezo ya 11 ya Asia iliyofanyika hapa Beijing, na picha yake ikawa ishra ya michezo hiyo.
Watu wengi wanampenda sana panda huyo Bw. He Weitian ni mkuu wa shirika la kuhifadhi panda la Macao, alikuja Fuzhou mwaka jana kwa ajili ya kumpa hongera panda huyo alipotimiza umri wa miaka 25. Mbali na hayo Bw. He pia alichangisha fedha kuchapisha vitabu vizuri vya picha vinavyomhusu panda Basi. Alisema "Kwa kawaida panda anaishi kwa miaka 12 tu. Lakini Basi ameishi maisha marefu ya namna hii, hii inaonesha kuwa China inaongoza katika utafiti wa panda duniani. Na China ingeeneza uzoefu huo duniani."
Mkazi wa mji wa Fuzhou mzee Lu Weixie mwenye umri wa miaka 64 ni mshabiki mmoja wa panda. Tokea miaka mingi iliyopita, alianza kukusanya vitu mbalimbali vyenye picha za panda, hivi sasa idadi ya vitu hivyo imefikia elfu kadhaa. Hivi karibuni mzee Lu alitoa vitu hivyo vikiwemo stampu, kadi na mabahasha kwa jumba la makumbusho la panda la Fuzhou. Alieleza kuwa watu wengi walichangia uanzishwaji wa jumba hilo la makumbusho. Alisema "Mathalan, katika jumba hilo kuna jiwe moja lenye umbo maalumu liitwalo panda asiye na mdomo, jiwe hilo lilifadhiliwa na mchoraji maarufu wa China Bw. Chen Dawei. Yeye akipata habari ya kuanzishwa kwa jumba hilo la makumbusho linalohusu panda, alisema 'Chukua jiwe hilo. Wewe umetoa vitu vyako vyote kwa jumba hilo, kwa hiyo nakupa jiwe hilo kama zawadi.' Wachoraji wengine wengi pia waliguswa na mimi, wakakubali kutoa mchango wa vitu vya sanaa wanavyohifadhi."
Bw. Lu Weixie aliongeza kuwa, panda ni majivuno ya watu wa China. Na panda Basi mwenye umri wa miaka zaidi ya 100 ni majivuno ya wakazi wa mji wa Fuzhou, kwa hiyo anajikita katika shughuli za kueneza utamaduni unaohusu panda.
Idhaa ya kiswahili 2006-11-16
|