Waziri wa biashara na viwanda wa Namibia Bw. Immanuel Ngatjizeko hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China alisema kuwa, China siku zote ni rafiki wa dhati wa Namibia na nchi nyingine za Afrika, ongezeko la uchumi la China halitakuwa tishio kwa Afrika, bali litaleta manufaa kwa Afrika na dunia nzima.
Bw. Ngatjizeko alisema uhusiano kati ya Afrika na China ni uhusiano wa kunufaishana. Alisema tofauti na nchi kadhaa za magharibi, misaada inayotolewa na serikali ya China kwa Afrika haina masharti, na serikali ya China inaheshimu matakwa ya nchi za Afrika. Hivyo serikali ya Namibia baada ya kujipatia uhuru mwaka 1990 ilianzisha mara moja uhusiano wa kibalozi kati yake na Jamhuri ya Watu wa China.
Bw. Ngatjizeko alisifu sana mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana nchini China. Alisema China imewaonesha walimwengu maendeleo yake ya uchumi, na nchi nyingi zinafahamu hadhi muhimu ya China katika uchumi duniani.
Kuhusu kauli inayotolewa na baadhi ya nchi kuhusu ati "tishio la China", Bw. Ngatjizeko alidhihirisha kuwa maendeleo ya China, hasa ongezeko lake kasi la usafirishaji wa bidhaa za viwanda na matumizi limezisaidia sana nchi za Afrika. Siku zamani nchi za Afrika zilipaswa kutumia fedha nyingi kuagiza bidhaa za viwanda na matumizi kutoka kwa nchi za magharibi, lakini hivi sasa zinaweza kupata bidhaa hizo kwa bei nafuu zaidi kutoka China.
Namibia ina rasilimali nyingi za madini yakiwemo madini ya vito, uranium, shaba, na dhahabu, na asilimia 90 ya madini yanayochimbwa nchini humo yanasafirishwa nje, ushirikiano kati ya Namibia na China katika sekta ya uchimbaji madini unanufaisha pande zote mbili. Alisema uwekezaji wa makampuni ya China katika sekta hiyo unaweza kuleta teknolojia mpya na kuongeza ajira kwa wakazi wa nchi hiyo, na kutoa mchango ipasavyo katika kupunguza umaskini, kuleta utulivu wa kijamii na kustawisha uchumi wa nchi hiyo. Kwa hivyo Namibia inayakaribisha sana makampuni ya China kuwekeza nchini humo.
Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia pia aliyakaribisha makampuni ya China kuwekeza nchini Namibia hasa katika sekta za uchimbaji wa madini, kilimo na utalii. Rais Pohamba aliwaambia waandishi wa habari wa China kuwa, hivi sasa makampuni mengi ya China yamewekeza nchini Namibia, hasa katika sekta ya ujenzi. Hii inamaanisha kuwa uhusiano kati ya Namibia na China unaendelea siku hadi siku katika sekta mbalimbali, ushirikiano kati ya pande hizo mbili hauna kipingamizi chochote. Alisema makampuni ya China yaliyoko nchini humo yametoa mchango mkubwa katika kustawisha uchumi wa Namibia, na China inasaidia kubadilisha hali ya Namibia.
Rais Pohamba alisema Namibia inatumai kuwa makampuni ya China yatakwenda nchini Namibia kutafuta fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali. Alisema Namibia ilijipatia uhuru miaka 16 iliyopita, katika muda huo mfupi nchi hiyo haikuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya kitaalam kwa watu wanaoshughulikia sekta mbalimbali, hivyo inapaswa kutegemea marafiki wa nje kama wachina kujiendeleza.
Rais Pohamba alisema kukuza na kupanua sekta mpya za ushirikiano kati ya Namibia na China kutakuwa muhimu sana katika kuleta ongezeko la kasi la kiuchumi, kama vile kutafuta na kuchimba rasilimali za mafuta na gesi ya asili, ujenzi wa bandari, barabara na reli, usindikaji wa chakula na mazao ya kilimo, utengenezaji wa vipuri vya magari na mawasiliano ya simu.
Thamani ya biashara kati ya China na Namibia imeongezeka haraka, mwaka jana ilifikia dola za kimarekani milioni 140, ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili umefanyika katika sekta nyingi kama vile ujenzi wa reli na mawasiliano ya simu. Alisema, biashara kati ya China na Namibia ina uwezo mkubwa wa kukuza katika sekta za kilimo, utoaji huduma, utalii, utengenezaji wa bidhaa za viwanda na kadhalika.
Tangu China na Namibia zianzishe uhusiano wa kibalozi, ushirikiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili umeimarishwa siku hadi siku, ziara za viongozi wa ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili zimesukuma mbele ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.
Viongozi hao wa Namibia wameeleza imani yao kuwa, mkutano huo wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika utaimarisha zaidi ushirikiano na mshikamano uliopo kati ya China na nchi za Afrika, na kutoa maelekezo kwa utatuzi wa matatizo yanayozikabili nchi za duniani hasa nchi zinazoendelea.
Idhaa ya Kiswahili 2006-11-17
|