Bw. Zhou Jinglong mwenye umri wa miaka 38 alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Xincun, mkoani Anhui uliopo mashariki mwa China. Mkulima huyo pia ni fundi seremala hodari, katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, alikuwa anahangaika kwenye viwanja mbalimbali mjini Hefei, mkoani Anhui ambako miradi mbalimbali ya ujenzi ilikuwa inajengwa, wakati ambapo kulikuwa na pilikapilika mashambani, alirudi kijijini kwao kuwasaidia jamaa zake.
Katika maskani yake ya kijiji cha Xincun, vijana waliokwenda mijini kutafuta ajira wana maisha tofauti na hayo ya Bw. Zhou, ambao wanaonekana kuwa wameacha kabisa shughuli za kilimo. Bw. Zhou aliwasimulia vijana hao kwamba, "Wao wanapata ajira viwandani, inawapasa wafuate nidhamu, hawarudi kijijini katika majira ya shughuli za kilimo."
Hivi sasa nchini China vijana wakulima mfano wa wale waliotajwa na Bw. Zhou, wanachukua sehemu kubwa ya wakulima wanaofanya kazi mijini. Vijana hao wanakwenda mijini kutafuta ajira badala ya kazi za vibarua, hali ambayo inatofautiana na wakulima wa vizazi vilivyopita, na hii ni mojawapo ya mabadiliko yanayotokea miongoni mwa wakulima wa China.
Kwa mujibu wa utafiti uliokamilishwa na baraza la serikali ya China hivi karibuni, mabadiliko makubwa matatu yameibuka miongoni mwa wakulima wanaofanya kazi mijini nchini China. Na mabadiliko mengine mawili ni kwamba, wakulima wameanza kubadilika kuwa wakazi wa miji na wameanza kutetea haki zao kama walivyofanya wakazi wengine wa mijini.
Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2004 miongoni mwa wakulima wa China waliofanya kazi mijini, idadi ya wale waliokaa mjini kwa muda wa zaidi ya nusu mwaka walichukua asilimia 81.3, huku hali halisi ni kwamba vijana wa vijijini wameacha kabisa shughuli za kilimo. Hapo awali wakulima waliingia mijini kutafuta kazi za vibarua wakati ambapo hakuna shughuli nyingi za mashambani, lakini hivi sasa hali hiyo haipo.
Kupata ajira kamili kwenye viwanda vya mijini kunawafanya vijana waliotoka kijiji cha Bw. Zhou wakae mijini kwa muda mrefu. Bw. Zhou ametambua kuwa kuna pengo kati yake na vijana hao wenzake, alisema "wao wanaonekana ni wakazi wa mijini siku hadi siku."
Aidha kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa wapo wakulima wapatao milioni 200 wanaofanya kazi mijini, wana umri wa wastani wa miaka 28.6, theluthi mbili kati yao wamamaliza masomo ya shule za sekondari ya chini, ambao ni wakulima waliopata elimu nyingi zaidi kuliko wakulima wengine wa China.
Mwanachama wa taasisi ya sayansi ya jamii ya mkoa wa Anhui Bw. Wang Kaiyu amebobea katika masuala yanayohusu wakulima wanaofanya kazi mijini. Alisema vijana hao kutoka vijijini wana uwezo mkubwa wa kujifunza mambo mapya, kumiminikia mijini kwao si kama tu ni kwa ajili ya kuchuma pesa, bali pia ni kujitafutia nafasi ya kuishi maisha ya kisasa, kupata heshima na haki sawa za jamii.
Mkulima Zhao Haibo aliondoka maskani yake alipokuwa na umri wa miaka 17, mpaka hivi sasa amekuwa akifanya kazi mijini kwa miaka 13. Bwana huyo sasa ni mkuu wa idara moja ya kampuni ya ujenzi mjini Hefei. Alisema hivi sasa anarudi makwao kuwatembelea jamaa kila baada ya miaka mitatu, na hajui kabisa namna ya kufanya kazi mashambani.
Bw. Zhao anaishi maisha yanayofanana na wakazi wengine wa mijini, ambapo baada ya kazi anakutana na marafiki, wakijiburudisha kwenye mikahawa au kutizama filamu kwa pamoja.
Bw. Zhao na wenzake ni nguvu kazi wenye umri mdogo kabisa katika miji ya China, pia ni nguzo mojawapo ya kutumia pesa na kuweka akiba benkini. Mtaalamu wa mambo ya China Bw. Hu Angang alisema, kama wakulima wanaofanya kazi mijini wanaongeza matumizi mijini, hali hii itachangia ujenzi wa makazi, utoaji huduma za tiba na ujenzi wa miundo mbinu mijini, jambo ambalo linasaidia kupanua soko la China.
Pamoja na kwamba wakulima wanaofanya kazi mijini wamezoea maisha ya mijini, na kutambua umuhimu wa kujitetea haki zao halali kwa mujibu wa sheria na kupigania haki sawa na wakazi wengine wa mijini, lakini kero mbalimbali bado zinawakabili. Kero hizo ni pamoja na elimu ya watoto wao, huduma za jamii n.k., ambazo zinawakwamisha kuishi vizuri mijini.
Bw. Zhao Haibo akikamilisha maelezo ya maisha yake mazuri hapa mjini, alijitetea kuwa, "Familia yangu ni familia ya wakulima, na hivi sasa mimi pia bado ni mkulima mmoja."
Hivi sasa serikali za mikoa kadhaa ya China zimeanza kuandaa sera mpya ili kuwapa wakulima wanaofanya kazi mijini haki sawa na kuondoa kero mbalimbali zinazowasumbua.
Idhaa ya kiswahili 2006-11-23
|