Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-24 17:09:03    
China imezisaidia nchi za Afrika kutoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi zaidi ya elfu kumi

cri

Kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara ya biashara ya China, ushirikiano wa kutoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi kati ya China na nchi za Afrika umeingia katika kipindi kipya, na unahusu mambo ya uchumi na biashara, matibabu na afya, mambo ya kiutawala, mawasiliano ya simu, jiografia, elimu na mazingira. Ilipofika mwezi Agosti mwaka huu, serikali ya China kwa jumla ilikuwa imetoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi zaidi ya elfu 11 wa nchi zaidi ya 50 za Afrika.

China siku zote inatilia maanani kufanya maingiliano ya watu na ushirikiano wa kutoa mafunzo kati yake na nchi za Afrika, imeandaa semina mbalimbali kwa kuzisaidia nchi za Afrika ziimarishe ujenzi wa uwezo wao ili kuleta maendeleo endelevu ya uchumi na jamii. Mwezi Desemba mwaka 2003, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alitangaza kwenye mkutano wa pili wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika nchini Ethiopia kuwa, katika miaka mitatu ijayo China itatoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi zaidi ya elfu 10 wa sekta mbalimbali kutoka nchi za Afrika.

Tokea mwaka 2004, China iliongeza nguvu katika kutoa mafunzo kuzisaidia nchi za Afrika kuwaandaa watu wenye ujuzi. Takwimu zinaonesha kuwa, katika mwaka 2004 watu 2,963 kutoka nchi za Afrika walishiriki katika semina mbalimbali zilizoandaliwa na serikali ya China nchini China au katika nchi za Afrika, idadi hiyo ilikuwa mara 1.4 kuliko jumla ya idadi ya watu wa Afrika walioshiriki katika mafunzo yaliyoandaliwa na China katika miaka 20 iliyopita. Yaani kuanzia mwaka 1983 hadi mwaka 2003 idadi ya watu wa Afrika waliopewa mafunzo kwenye semina zilizoandaliwa na serikali ya China ilikuwa 2,167.

Mwaka 2005 idadi hiyo ilikuwa 4,887 na iliweka rekodi ya kihistoria. Mwaka 2006 serikali ya China imepanga kutoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi 3900 kutokana na mahitaji ya nchi za Afrika.

Wataalamu husika wanachukulia kuwa, China na nchi za Afrika zote ni nchi zinazoendelea, uzoefu na teknolojia za China za kuleta maendeleo ya jamii na uchumi zinafaa sana kwa nchi za Afrika. Nchi za Afrika zimeimarisha ujenzi wa uwezo wao, kuzidisha ufahamu juu ya China na kuongeza urafiki wa jadi baada ya kutuma watu wa sekta mbalimbali kushiriki kwenye semina zilizoandaliwa na serikali ya China.

Mwanafunzi kutoka Cote d'Ivoire Bwana Donald baada ya kushiriki katika semina ya kimataifa ya teknolojia ya ufugaji wa viumbe baharini aliandika shairi lisemalo "Nakushukuru China" kueleza hisia zake kwa msaada wa serikali ya China.

Ofisa wa afya kutoka Mauritania baada ya kushiriki kwenye semina ya kinga na tiba ya ugonjwa wa Ukimwi hapa China alisema, semina hiyo imetoa fursa nzuri kwa watu wa Afrika kufahamu jinsi watu wa China wanavyoshughulikia kinga na tiba ya ugonjwa wa ukimwi, uzoefu wa China wenye mafanikio katika sekta hiyo utazisaidia nchi za Afrika katika kinga na tiba ya ukimwi.

Zaidi ya hayo semina za aina mbalimbali zilizoandaliwa na China zimeweka madaraja ya mawasiliano kati ya watu wa China na wa nchi za Afrika, na kuchangia kusukuma mbele uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta mbalimbali.

Takwimu zilizotolewa na idara za forodha za China zinaonesha kuwa, mwaka 2005 thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola za kimarekani 40 hivi, hili ni ongezeko la asilimia 34.9 kuliko mwaka uliotangulia, ambalo lilizidi ongezeko la thamani ya biashara kati ya China na mabara mengine duniani.

Mhusika wa idara inayoshughulikia msaada na nje ya wizara ya biashara ya China alisema, katika miaka kadhaa ijayo serikali ya China itaweka mkazo katika kutekeleza hatua mpya kuzisaidia nchi zinazoendelea kutoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi kufuata mahitaji na umaalum wa ushirikiano wa pande mbili mbili kati ya China na nchi za Afrika, kuimarisha ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika kuendeleza kazi ya kutoa mafunzo ya kuwaandaa watu wenye ujuzi, kuanzisha njia mpya za ushirikiano, na kupanua sekta za ushirikiano, ili kuendelea kuzisaidia nchi za Afrika kuleta maendeleo ya uchumi na jamii.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-24