Nchini China mamilioni ya vijana wanahitimu masomo ya vyuo vikuu kila mwaka. Miongoni mwao kuna vijana wa makabila madogomadogo ambao maskani yao yako mbali na miji. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alizungumza na wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu wanaotoka kwenye makabila madogomadogo ambao wanatarajiwa kuhitimu mwakani.
Bieke ni mvulana wa kabila la Wakhazak, hivi sasa anasomea kozi ya lugha na fasihi ya Kikhazak katika Chuo kikuu cha makabila cha China, hapa jijini Beijing. Maskani ya kijana huyo yapo katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Ugyur, kaskazini magharibi mwa China. Mwezi Julai mwakani Bieke atahitimu. Je, yeye angependa kufanya kazi wapi? Kijana huyo alisema "Nina mpango wa kuanza kufanya kazi hapa Beijing mara baada ya kuhitimu chuo kikuu, kwani Beijing ni mji wenye mazingira mazuri yanayofaa kwetu kujiendeleza. Hata hivyo hapa Beijing ushindani pia ni mkubwa."
Kijana Bieke anafahamu lugha mbili za Kikhazak na Kichina. Kutokana na uwezo huo, tangu alipokuwa mwaka wa pili kwenye chuo kikuu alianza kufanya kazi ya ukalimani katika kampuni kadhaa za kigeni hapa Beijing. Zaidi ya hayo kijana huyo alisomea lugha nyingine mbili, Kirussia na Kiingereza, pia anashika wadhifa fulani kwenye baraza la wanafunzi. Sifa hizo zinamfanya awe na nafasi kubwa katika kutafuta ajira. Bieke alieleza kuwa kuna kampuni nyingi zinazoendeshwa na Warussia na Wakhazakstan mjini Beijing, na kampuni kadhaa zilishamwalika ajiunge nazo.
Kwa kulinganishwa na kijana Bieke, mwenzake wa kabila la Wamongolia kijana Bai Lan anaonekana kukosa bahati. Bai Lan anasomea lugha na fasihi ya Kimongolia. Kwa sababu anaongea Kimongolia tangu utotoni mwake, kijana huyo anashindwa kuongea Kichina sanifu, na alianza karibuni tu kujifunza lugha ya Kiingereza baada ya kuingia kwenye chuo kikuu. Kuhusu suala la ajira Bai Lan alisema "Naona ni vigumu kwangu kupata ajira hapa Beijing. Nikirudi maskani yangu nadhani itakuwa rahisi zaidi."
Aliongeza kuwa atajaribu kutafuta ajira mjini Beijing, akishindwa atarudi nyumbani kwao. Alieleza maoni yake kuwa, kufanya kazi katika mji wowote hakuna tofauti kubwa, bali jambo muhimu ni kupata ajira anayopenda. Kuendelea na masomo ya shahada ya pili vile vile ni chaguo moja. Ibrahim ni kijana wa kabila la Waugyur, ambaye ameamua kushiriki kwenye mitihani ya kusoma shahada ya pili itakayofanyika mwanzoni mwa mwakani. Hivi sasa zimebaki siku 50 hivi kabla ya kufanyika kwa mitihani, Ibrahim amejikita kwenye masomo kiasi kwamba hapumziki mpaka usiku wa manane. Kijana huyo alisema "Nataka kuendelea na masomo na kupata ujuzi mwingi zaidi, halafu nitarudi kwenye maskani yangu, ambapo nitafanya utafiti kuhusu masuala ya jamii, kutafiti historia na utamaduni wa kabila letu kwa kutumia nadharia za sayansi ya jamii."
Ibrahim ana mpango kabambe, hata hivyo wazazi wa kijana huyo hawakubaliani naye. Wao wanamtaka arudi kwenye maskani yake mapema baada ya kuhitimu chuo kikuu, atafute ajira huko kwao na kuishi pamoja na jamaa zake, lakini yeye anashikilia mpango wake. Alieleza kuwa hata kama atashindwa kufaulu mitihani ya kusoma shahada ya pili, angetaka aweze kupata nafasi ya kusoma nchini Uturuki, ambapo atasoma zaidi kabla ya kurudi nyumbani.
Wei Chenxi ni kijana wa kabila la Wamulao wanaoishi kwenye mkoa unaojiendesha wa Guangxi, kusini mwa China. Hivi sasa anasomea uhandisi wa software. Alieleza kuwa kuna wanafunzi wenzake wa kabila la Wamulao wanaosoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali hapa Beijing. Kuhusu suala la ajira, Wei Chenxi alisema "Marafiki zangu karibu wote wanataka kubaki mjini Beijing. Wakishindwa kupata ajira nzuri hapa Beijing, wanaweza kufikiria miji mingine mikubwa, kama vile Shanghai na Guangzhou, lakini mimi sikuwahi kufikiri suala la kurudi mkoani Guangxi, jamaa zangu pia wanapenda kuona kuwa nitafanya kazi katika sehemu nyingine na kuona maisha tofauti na ya maskani yetu."
3Vijana wenye wazo la namna hii wapo wengi miongoni mwa vijana wa makabila madogomadogo watakaohitimu kutoka kwenye vyuo vikuu. Miji mikubwa ya China ikiwemo Beijing, Shanghai na Guangzhou, ina uchumi wa kisasa, kampuni nyingi za kigeni, shughuli mbalimbali za kiutamaduni, na inawaandalia vijana nafasi nyingi za kujiendeleza. Vijana wengi kutoka sehemu zilizoko mbali na miji wakisoma vyuo vikuu kwenye miji hiyo mikubwa, wanapata mawazo ya kisasa na kuzoea maisha ya miji mikubwa, kwa hiyo ni hali ya kawaida kwao kupendelea kutafuta ajira katika miji hiyo. Hali hii inasaidia maendeleo ya miji hiyo mikubwa, lakini je, inaziathiri sehemu zilizo nyuma kimaendeleo?
Kuhusu hoja hii, wanafunzi wengi wa makabila madogomadogo walieleza kuwa, hatimaye watarudi kwenye maskani yao. Kijana wa kabila la Wakhazak Bieke alisema (sauti 5) "Naona sisi vijana tungekaa hapa Beijing ili kujifunza vitu vingi zaidi, mpaka tutakapozeeka ndipo tutarudi nyumbani kuendelea na shughuli zetu, hii ni njia nzuri kwa sisi binafsi, maskani yetu na makabila yetu."
Kijana huyo aliongeza kuwa, hata kama wanakwenda mbali sana, wanafuatilia hali ya maskani yao kila wakati, na hatimaye watarudi nyumbani, jambo ambalo linafanana na majani kuanguka na kurudi kwenye mizizi.
Idhaa ya kiswahili 2006-11-30
|