Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-14 10:38:23    
Utalii waleta maisha mapya kwa wakazi wa mkoani Xinjiang

cri

Mkoa unaojiendesha wa Uygur wa Xinjiang ulioko kaskazini magharibi mwa China una maliasili nyingi za utalii, sehemu za kiutamaduni, mandhari ya kimaumbile na mila na desturi pekee za makabila madogo madogo. Baada ya maendeleo ya miaka miongo kadhaa, utalii umetoa mchango mkubwa kwa uchumi wa mkoa huo.

Ziwa la Kanas lililoko kaskazini mwa mkoa wa Xinjiang ni sehemu yenye vivutio vya utalii vinavyojulikana nchini China na duniani, mzee Tuwa wa kabila la wamongolia anayeishi kando ya ziwa Kanas alianza kujifunza kupiga ala maalum ya kikabila iitwayo "Chu'er" alipokuwa na umri wa miaka 13. Jambo linalomfurahisha mzee huyo ni kwamba, baada ya miaka 50, maisha yake yamebadilika kutokana na ustadi wake wa kupiga ala ya "Chu'er".

"Chu'er" ni ala ya aina moja ya muziki inayofanana na filimbi, inatengenezwa kwa bua la tete lililoota pembezoni mwa ziwa Kanas. Kwa sababu kitu kinachotumiwa katika kutengeneza filimbi hiyo ni maalum sana, hivyo muziki huo umeenea tu kati ya watu wa kabila la watuwa.

Inasemekana kuwa, mzee Yerdexi ni hodari zaidi kuliko wengine katika kupiga filimbi hiyo. Kutokana na maendeleo ya utalii wa sehemu ya Ziwa Kanas, watalii wengi zaidi wa nchini China na wa ng'ambo wanamiminikia huko, na kuleta biashara nzuri kwa familia ya mzee Yerdexi. Miaka kadhaa iliyopita, waligeuza nyumba yao kuwa kituo cha kuwapokea watalii, na jambo linalowavutia watalii zaidi ndiyo kusikiliza mzee Yerdexi kuipiga filimbi ya "Chu'er".

Binti ya mzee huyo alisema kuwa, zamani familia yake iliishi kwa kutegemea ufugaji na uwindaji, lakini mtindo huo wa maisha umebadilika kutokana na maendeleo ya utalii. Akisema:

"Familia yangu imeishi hapa kwa vizazi vingi, zamani tuliishi kutokana na ufugaji. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, tulianza kuwapokea watalii kutoka nchi mbalimbali, ambao wanapenda sana kumsikiliza baba yangu akipiga filimbi."

Binti huyo alisema kuwa, katika majira yenye watalii wengi, pato la familia yake linazidi Yuan elfu 20 kwa mwezi, ambazo zinawawezesha kununua vyombo vingi vya umeme kama vile televisheni ya kupokea vipindi kutoka kwenye satilaiti, simu na friji, na mwaka huu wamepanga kununua gari dogo.

Mabadiliko ya familia ya mzee Yerdexi yamewahamasisha watu wengine wa kijiji hicho pia wajishughushe na mambo ya utalii, kama vile kuendesha mikahawa, kuuza vyakula vya maziwa, na kuuza vitu vya kumbukumbu. Hivi sasa asilimia 70 ya wanakijiji wanajishughulisha na fani hiyo.

Kama sehemu ya vivutio vya utalii ya Ziwa Kanas, katika sehemu nyingine nyingi za vivutio vya utalii, wakazi wengine pia wamebadilisha maisha yao kwa kukuza utalii. Mmojawao ni Mzee Abulizi wa kabila la wahui anayeishi katika sehemu ya Turufan inayojulikana kwa kuzalisha zabibu.

Mzee Abulizi alisema kuwa, kabla ya kuwapokea watalii pato la familia yake lilitokana na kulima zabibu tu. Katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, familia yake ilianza kushughulikia mambo ya utalii. Akisema:

"Kila mwaka tunawapokea watalii zaidi ya 1000. Idadi hiyo ya mwaka huu itakuwa zaidi kuliko zamani. Hadi leo, nimewapokea watalii 1200, na kuleta mapato Yuan elfu 12."

Takwimu zimeonesha kuwa, mwaka jana idadi ya watalii wa nchi za nje waliosafiri mkoani Xinjiang ilizidi laki tatu, na idadi hiyo ya watalii wa China ilizidi milioni 12, pato la utalii lilichukua asilimia 5 ya thamani ya uzalishaji ya mkoa mzima.

Ili kuharakisha maendeleo ya utalii, katika miaka mitano iliyopita, mkoa wa Xinjiang umetenga Yuan zaidi ya bilioni nne kuanzisha shughuli nyingi za utalii kama vile, utalii wa viumbe wa milima na maziwa, utalii wa jangwani, utalii wa mbugani, utalii wa sehemu za kale na utalii unaohusu mila na desturi. Isitoshe, serikali kuu na serikali ya mkoa huo pia zimegharamia fedha nyingi katika ujenzi wa miundo mbinu ya utalii na viwanja vya ndege kwenye sehemu za vivutio vya utalii.

Lakini kuja kwa watalii wengi pia kumeleta athari mbaya kwa hifadhi ya mazingira ya viumbe, kwa mfano hoteli nyingi zisizofaa zimejengwa kwenye sehemu za vivutio vya utalii. Idara husika za sehemu ya vivutio vya utalii ya Kanas zimeamua kubomoa hoteli hizo zisizofaa na kujenga hoteli nyingi kubwa nje ya sehemu hiyo ya utalii yenye umbali wa kilomita 30 kutoka kwa Ziwa Kanas. Mhusika Bi. Zhang Hong alisema:

"Ili kuhifadhi mazingira ya viumbe ya sehemu ya vivutio vya utalii ya Ziwa Kanas, tutatenganisha sehemu wanazoishi watu na sehemu za utalii. Siku zijazo, watalii wakija kutembelea hapa, hawatalala kwenye sehemu ya utalii."

Idhaa ya kiswahili 2006-12-14